MIRADI 7 YAKAGULIWA NA KUZINDULIWA NA MWENGE WA UHURU JIJINI MBEYA‏

Vijana wa Skauti wakimvalisha skafu kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Juma Khatibu Chum kama ishara ya kumkaribisha jijini Mbeya.

WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu kwa kuwachagua viongozi wazalendo na kuwakataa wanaotoa rushwa.

Wito huo ulitolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa, Juma Khatibu Chum, alipokuwa akitoa salamu kwa wakazi wa Jiji la Mbeya waliojitokeza kuushuhudia Mwenge huo  katika viwanja wa shule ya Msingi Ruandanzovwe baada ya kumaliza kukagua miradi ya Jiji la Mbeya.

Kiongozi huyo alisema Wananchi hawapaswi kufanya majaribio katika uchaguzi kwa kuchagua viongozi wala rushwa na wanaopinga maendeleo hususani wanaobeza uwepo wa Mwenge wa Uhuru bila kujua umuhimu wake katika kukagua na kuzindua miradi mbali mbali.

Alisema njia pekee ya kuwakataa viongozi hao ni katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutowapigia kura ya ndiyo pamoja na wananchi kujitokeza katika uchaguzi huo na kukipitisha Chama cha mapinduzi ili kiendelee kuwaletea maendeleo na sio kuwachagua wanaowalazimisha kufanya fujo.

Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa jijini Mbeya na kuzindua, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba pamoja na kutoa hati na tuzo kwa vikundi mbali mbali vilivyofanya vizuri katika shughuli za maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Munasa aliitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa jengo la maabara katika shule ya Sekondari ya Hayombo na ufunguzi wa Klabu za kupambana na Rushwa uliogharimu shilingi 69,140,000.

Aliongeza  kuwa lengo ni kuboresha mazigira ya wanafunzi kufanyia mazoezi kwa vitendo masomo ya sayansi na kuongeza ufaulu pamoja na kujenga misingi  bora  kwa vijana na wanafunzi kukataa rushwa.

Aliutaja mradi wa pili kuwa ni mradi wa kikundi cha wanawake wajasiliamali cha usindikaji cha Mshikamano uliogharimu shilingi 20,800,000 wenye lengo la kuwasaidia wanawake kujiajiri, kujengana maadili na kuinua kipato na kuboresha mazingira ya uwekezaji shughuli za kiuchumi za wanawake na kuongeza thamani ya bidhaa zinazosindikwa  kutoka kwa mazao ghafi.

Miradi mingine ni ujenzi wa barabara ya Isyesye kwa kiwango cha lami utakaogharimu shilingi 1,027,604,000 wenye lengo la kupunguza foleni ya magari katikati ya Jiji,  Mradi mwingine uliofunguliwa ni mradi wa maji Mwasanga uligharimu shilingi 303,338,500 lengo ukiwa kupunguza vihatarishi vya matumizi ya maji yasiyosafi.

Mwenge wa Uhuru pia  ulifungua mradi wa jengo la kituo cha kukusanyia na kuhifadhia mazao cha mWsanga uliogjarimu shilingi 64,147,700, mradi wa ujenzi wa kituo cha matibabu na vipimo kwa wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi uliogharibu shilingi Milioni 27.

Mkuu wa Wilaya aliutaja mradi wa saba kuwa ni uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha polisi Ilomba ambao uligharimu shilingi Milioni 24.8 wenye lengo la kupunguza uhalifu katika jamii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni