Hivi ndiyo Helkopta ilivypkuwa ikionekana baada ya kupata Ajali. |
Mbunge Joshua Nassari mara baada ya kunusurika katika ajali ya ndege hiyo. |
Mbunge Nassari akiwa amelazwa katika Hosptali ya Seliani mkoani Arusha. |
Baadhi ya watu waliofika kumjulia hali Mbunge Nassari. |
Mchungaji akifanya maombi kwa ajili ya majeruhi wa ajali hiyo. |
Mbunge Nassari akiwa amekaa sehemu ya mapokezi katika Hosptali ya Seliani baada ya kuruhusiwa kutoka wodini. |
Mbunge Nassari akitoka katika Hosptali ya Seliani mara baada ya kuruhusiwa. |
Wakati
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akisema anashindwa kuamini
kilichotokea na kunusurika katika ajali ya helikopta juzi, mmiliki wa
chopa hiyo, Philemon Ndesamburo amesema atanunua nyingine haraka kabla
ya kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Kauli
hizo zilitolewa jana ikiwa ni siku moja baada ya helikopta hiyo
inayomilikiwa na Ndesamburo kupitia kampuni yake ya Keys Aviation kupata
ajali wakati ikitumiwa na Nassari na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Wakati ikipata ajali, ilikuwa imekodishwa na Kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd inayomilikiwa na Kapteni William Slaa.
Katibu
wa Ndesamburo, Basil Lema alisema ilipata ajali baada ya kupigwa na
kimbunga wakati anga likiwa limefunikiwa na wingu zito.
“Mheshimiwa
Ndesamburo amemshukuru Mungu kwa kuwanusuru watu waliokuwa kwenye ndege
hiyo ambao ni pamoja na Mbunge Joshua Nassari.
“Ameweka
wazi kwamba atalazimika kununua nyingine mapema kwa ajili ya kuongeza
nguvu kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu,” alisema Lema akimnukuu
Ndesamburo.
Lema
alisema rubani aliyekuwa akiendesha helikopta hiyo alifanikiwa
kuielekeza juu ya miti alioutumia kupunguza kasi ya kushuka chini na
kusaidia abiria kutoka salama.
“Imeharibika
lakini abiria wote ni wazima. Walikuwamo wanne,” alisema na kuongeza
kuwa helikopta hiyo ndiyo iliyotumiwa na Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa
2010 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana na chama hicho
kilitegemea kuitumia katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Pia,
imewahi kutumiwa na makada mbalimbali wa CCM akiwamo Naibu Katibu Mkuu
wa CCM, Mwigulu Nchemba na kada maarufu wa Moshi mjini, Buni Ramole.
Kauli ya Nassari
Akizungumza
na waandishi wa habari katika wodi alikolazwa kwenye Hospitali ya
Seliani – Arusha, Nassari alisema waliporuka kutoka Leguruki, hakukuwa
na dalili zozote za kuchafuka kwa hali ya hewa, lakini dakika chache
baada ya kuruka angani wingu zito lililoambatana na upepo mkali
liliwafunika ghafla.
“Wingu
lile na upepo ule sijawahi kuona katika maisha yangu yote zaidi ya
kusoma kwenye vitabu vya simulizi vya mambo ya ushirikina. Namshukuru
Mungu wote tuko salama kwani hatukuwa na matumaini ya kupona ajali ile,”
alisema Nassari.
Mbunge
huyo aliyekuwa katika ziara ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha
kwenye Daftari la Wapigakura, alimwagia sifa rubani Slaa kwa uwezo na
ustadi aliouonyesha hadi wakanusurika.
“Kama
siyo ustadi wake, naamini watu wangeokota vipande vya nyama tu kwenye
eneo la ajali, ila Mungu ni mkuu leo tuko hai wote licha ya madhara
madogo,” alisema.
Nassari
alisema muda mfupi kabla ya kuruka saa kumi na moja jioni, wakati
akihutubia mkutano huko Leguruki, alipokea simu kutoka kwa mchungaji
mmoja akimtaarifu kupata maono kuwa anakabiliwa na hatari ya kukutwa na
jambo kubwa na baya akimtaka adumu katika sala.
“Dakika
15 baadaye nikaruka na kupata ajali. Naamini kilichotuokoa ni nguvu ya
sala niliyosali baada ya kupokea ujumbe wa mchungaji na maombi ya
wachungaji wangu wanaoniombea kila siku,” alidai Nassari.
Rubani
Slaa alisema alishangaa lilipotokea wingu na upepo uliosababisha ndege
kuanguka ikiwa njiani kuelekea Ndoombo na Ngureserosambu.
“Kabla
ya kurusha ndege nilijiridhisha na hali ya hewa. Hakukuwa na kiashiria
chochote cha hali ya hatari kama maeneo mengine ambako tulishindwa kutua
kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha.
Kaimu
Mkurugenzi wa Hospitali ya Seliani, Dk Paul Kisanga alisema hali za
majeruhi si mbaya, isipokuwa Eva Kayaha aliyevunjika mbavu mbili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni