Taarifa
ya makubaliano toka kwa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imetolewa
leo Ikulu Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha Mkutano wa siku mbili wa
Wakuu wa Nchi za Jumuiya hiyo ambapo baadhi ya maadhimio waliyokubaliana
ni kwamba Rais Museveni wa Uganda awe msimamizi wa juhudi za upatanishi
wa makundi nchini Humo.
Akizungumza
wakati wa Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
Dkt. Richard Sezibera alisema kuwa Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni
apewe jukumu la usimamizi katika kupatanisha makundi nchini Burundi,
pia Serikali ya Burundi iwanyang'anye silaha kikundi cha vijana cha
Imbonerakure pamoja na makundi mengine ya vyama vya siasa ambayo
yanamiliki silaha hizo, Umoja wa Afrika (AU) ipeleke waangalizi wa
kijeshi kuhakikisha kuwa vikundi hivyo vinanyang'anywa silaha hizo,
Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu kutuma Timu ya Wakaguzi na Wataalam wa
mambo ya intelijensia kujua kama FDLR wapo nchini Burundi.
Sezibera
aliongeza kuwa Upande wowote utakaoshinda uchaguzi unapaswa kuunda
Serikali ya Kitaifa ambayo itashirikisha Vyama vilivyoshiriki pamoja na
vile visivyoshiriki uchaguzi nchini humo, pia upande wowote utakaoshinda
uchaguzi uheshimu makubaliano ya Arusha na kuhakikisha kuwa hautobadili
Katiba ya nchi hiyo.
"Umoja wa Afrika Mashariki unaombwa kupeleka Wakaguzi wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini humo", aliongeza Sezibera.
Naye
Waziri wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Harisson Mwakyembe alieleza kuwa
Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki
wa nchi zote tano zinazounda Jumuiya hiyo wamekuwa wakikutana jijini
Dar es Salaam ili kuweza kuandaa Mkutano wa Wakuu wa nchi huku lengo la
mikutano yote miwili likiwa ni kutafakari na na kutathmini hali iliyopo
ya kisiasa ndani ya Burundi.
Dkt.
Mwakyembe alisema kuwa viongozi hao waliwahi kufanya mkutano mnamo
tarehe 13 mwezi Mei mwaka huu licha ya mkutano huo kutokuwa na mafanikio
makubwa maana ni siku hiyo ambapo jaribio la kuipindua Serikali ya
Burundi lilitokea lakini viongozi hao walichukua msimamo wa kukemea
jaribio hilo la mapinduzi, ambapo pia waliiomba Serikali ya Burundi
kusogeza mbele tarehe ya kufanyika Uchaguzi mkuu nchini humo ambayo
ilipangwa iwe tarehe 25 Mei, 2015 hivyo badala yake wameishauri Serikali
hiyo kufanya uchaguzi huo tarehe 30 Julai mwaka huu.
"Huu
ni mkutano wa tatu ambapo tumechukua maamuzi makubwa sana kwa upande wa
viongozi wetu wanaoongoza Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa upande wa
Marais, kwanza kwa mara ya kwanza tumeamua kumteua moja ya viongozi
wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Museveni kuongoza
juhudi za kupatanisha haya makundi maana kwa sasa tunaamini utatuzi wa
mgogoro wa Burundi hauwezi kupatikana kwa njia yoyote isipokuwa kwa njia
ya mazungumzo", alisema Mwakyembe.
Aidha,
aliongeza kuwa Rais Museveni atakuwa akisimamia mchakato wa mazungumzo
ili kuweza kuifikisha Burundi mahali pazuri, lakini pia makubaliano
mengine yalifikiwa katika mkutano huo ni kwamba Serikali ya Burundi
imeombwa kusogeza tarehe ya uchaguzi mpaka tarehe 30 mwezi Julai mwaka
huu ili makundi mbalimbali yaweze kukutanishwa na kusuluhishwa.
Kwa
sasa Serikali ya Burundi inahangaikia suala kukusanya silaha toka kwa
vijana ambapo nguvu ya ziada inahitajika ndipo Umoja wa Afrika umeona
kuna haja ya kupeleka wataalamu wa kijeshi kuhakikisha kuwa zoezi hilo
la ukusanyaji wa silaha linakamilika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni