Balozi Seif azungumza na wana CCM na Wananchi wa Matawi ya Mangapwani na Mangapwani Bondeni


Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi {CCM } ngazi ya Matawi Nchini wameagizwa kujipanga vyema ili kuhakikisha Viongozi watakaowachagua wakati utakapowadia wa uchaguzi ndani ya chama hicho hapo mwakani wana sifa sahihi zitakazokidhi mahitaji yote ya kuwatumikia wanachama hao katika kipindi cha miaka Mitano ijayo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati za Siasa za Matawi ya Mangapwani na Mangapwani Bondeni katika mkutano wa kuwashukuru wanachama hao baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu uliopita.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda akiambatana  pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Bahati Ali Abeid na Madiwani wa Wadi zilizomo ndani ya Jimbo hilo alisema CCM ikiendelea kujipanga vyema kwenye chaguzi hizo itakuwa na uhakika wa kuendelea kuongoza Dola ya Watanzania katika miaka mingi ijayo.
Alisema wapo baadhi ya wapinzani walijipenyeza kwenye chaguzi za Chama hicho mwaka 2012 na kuomba Uongozi wakitumia hila na ujanja wa fedha na hatimae kuwayumbisha Viongozi na Wanachama wakati  wa kupanga safu ya utekelezaji wa Ilani na Sera za CCM.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwapongeza Wana CCM na Wananchi wa Mangapwani kwa uamuzi wao walioufanya mwezi Oktoba mwaka 2015 na Machi 2016 wa kuipa dhamana CCM iendelee kuongoza Dola ya Tanzania katika chaguzi zote mbili ile ya Zanzibar na ya Tanzania.
Balozi Seif alisema kazi inayowakabili Wananchi kwa hivi sasa ni kuelekeza nguvu zao katika kuimarisha miradi ya Kiuchumi na Maendeleo na kwa upande wa Uongozi wa Jimbo hilo tayari umeshajipanga kuhakikisha changamoto zinazowakabili Wananchi wa Maeneo hayo zinapatiwa ufumbuzi muwafaka.
Alisema yeye pamoja na Mbunge wake Mh. Bahati watashirikiana na viongozi wa Jimbo hilo ngazi ya Jimbo na Matawi katika ujenzi wa Jengo Jipya la Ofisi ya CCM Tawi la Mangapwani Bondeni litakalolingana na hadhi ya Chama chenyewe.
Balozi Seif aliwahakikishia Viongozi na Wanachama wa CCM wa Tawi la Mangapwani Bondeni kwamba yeye binafsi pamoja na Viongozi wenzake atasimamia maandalizi ya kuanza kwa msingi wa ujenzi wa Jengo hilo ili kuondoa kiu ya muda mrefu waliyokuwa nayo Wanachama hao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid aliwathibitishia Wanachama  na Viongozi wa Matawi hayo kwamba juhudi za awali zimeanza kuchukuliwa katika mwanzo wa kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.
Mh. Bahati alisema katika utekelezaji wa ahadi, Ilani na Sera za Chama cha Mapinduzi za kusimamia upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama kwa wananchi wa Matawi hayo Uongozi wa Jimbo hilo umeanza harakati za kuliondosha tatizo hilo sugu linalowakabili Wananchi hao.
Alisema ulazaji wa mabomba ya maji katika mradi maalum ulioanzishwa unatekelezwa katika Vijiji vya Kiomba Mvua, Fujoni na Mangapwani na kilichobakia kwa wakati huu ni Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kukamilisha uwekaji wa Mashine ya kusukumia Maji katika kisima kilichochimbwa kwenye eneo hilo.
Mbunge huyo wa Jimbo la Mahonda alifafanua zaidi kwamba juhudi hizo za uimarishaji wa miundombinu  katika Sekta ya Maji zimechukuliwa kwa makusudi na Uongozi wa Jimbo hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar baada ya kubaini kwamba Kisima kilichokuwa kikisambaza huduma ya maji katika kijiji hicho kiliopo Mfenesini kuzidiwa mara dufu.
Akigusia uhai wa Chama cha Mapinduzi Mh. Bahati aliwakumbusha Wanachama wa Matawi hayo kuhakikisha wanalipa ada zao kama kawaida bila ya kusibiri kusukumwa kufanya hivyo ili kukipa nguvu chama chao kiweze kutekeleza majukumu yake kama kawaida.
Mapema Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa la Wilaya ya Kaskazini “B” Mama Asha Suleiman Iddi waliwanasihi Wazee wa Vijiji hivyo Kuanzisha Kamati ya maadili itakayosaidia kutoa elimu kwa vijana waliojitumbukiza katika matumizi ya Dawa za kulevya.
Mama Asha alisema inasikitisha kuona jitihada kubwa zilizochukuliwa na Uongozi wa Jimbo hilo kwa kutumia fedha nyingi katika kuwapatia ushauri nasaha vijana hao kwenye nyumba za kurekebisha tabia { Sober House } hatimae ziligonga mwamba.
Alisema Kamati itakayoundwa katika Kijiji hicho cha Mangapwani itapaswa kwenda kujifunza kwa Kamati kama hiyo iliyoanzishwa katika Kijiji cha Fujoni ambayo imeleta mafanikio makubwa katika kukabiliana na wimbi la vijana waliojitumbukiza katika wimbi la matumizi ya dawa za kulevya.
Mama Asha alieleza kwamba Vijana wa Fujoni walioamua kuacha dawa hizo     tayari hivi sasa wamekuwa na mafanikio makubwa katika muendelezo wa mradi wao wa Uvuvi unaokidhi mahitaji yao ya kimaisha baada ya kupatiwa msaada wa Boti pamoja na Mashine yake.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
08/10/2016.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni