Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano ya maadhimisho ya kutimia Miaka 40 ya CCM kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja Kichama hapo Ukumbi wa Meli Nne Saccos.
Viongozi wa Juu wa CCM wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Balozi Seif ambae hayupo Pichani, ambapo wa kwanza kutoka Kushoto ni Waziri Kiongozi Mstaafu Mh. Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf Mohamed Yussuf.
Mke wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif , Mama Asha Suleiman Iddi kati kati akiwa shuhuda wa Kongamo hilo la maadhimisho ya kutimia miaka 40 ya CCM, wa kwanza kutoka Kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mjini ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud na wa kwanza kutoka kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani Nd. Ali Shunda.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Mkoa Magharibi Unguja waliohudhuria Kongamano la kutathmini na kujadili miaka 40 ya CCM.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Mkoa Magharibi Unguja waliohudhuria Kongamano la kutathmini na kujadili miaka 40 ya CCM.
Na. Othman Khamis Ame
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Viongozi na Wanachama wa CCM kuanzia ngazi ya chini ya Tawi kujenga utamaduni wa kufanya tathmini ya ratiba ya shughuli zao za kila siku za Chama hicho
kwa lengo la kuongeza nguvu pamoja na uhai wa Chama.
Hata hivyo alisema tathmini hizoili ziweze kuleta tija kwa CCM ni lazima zifanywe na Wataalamu waliomo ndani ya Chama hicho au hata wa kuazima kutoka nje kufanya tathmini hiyo Kitaalamu.
Akizungumza katika maadhimisho ya Miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM katika Mkoa wa Magharibi Unguja Kichama hapo katika Ukumbi wa Saccos Meli Nne Fuoni Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba tathmini isiyofuata taaluma haitakuwa na
maana yoyote bali ni kupoteza muda na rasilmali za Chama.
Alisema Tathmini nzuri ni ile inayowashirikisha Wanachama wa matabaka yote wakiwemo Wazee, Vijana,Wanawake, Wanaume, Viongozi na hata wanachama wa kawaida ikizingatia matokeo ya aina moja hata kama itafanywa na watu tofauti wasiojuwana.
Balozi Seif alisema kwamba tathmini iliyofanywa kwa misingi ya uadilifu na uaminifu mara nyingi husaidia kuwabaini watu waliokuwa vikwazo vya maendeleo ndani ya Chama hicho jambo ambalo lilichangia kuviza utendaji makini wa Chama.
Akizungumzia mabadiliko na Tathmini masuala yanayokwenda sambamba katika utekelezaji wake alisema wanachama wasiposhuhudia mabadiliko baada ya mikutano ya kutathmini changamoto ndani ya kipindi cha miaka 40 ya CCM wanaweza kuvunjika moyo.
Balozi Seif Ali Iddi alielezea faraja yake kutokana na mafanikio makubwa ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM ambapo wanachama na Viongozi watakuwa na fursa za kuzieleza changamoto zitakazojitokeza katika mapendekezo yao
kwenye utekelezaji wa ilani hiyo.
Balozi Seif ambae pia ni Mlezi wa Mkoa huo wa Magharibi Unguja Kichama alitoa wito kwa wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi ndani ya chama hicho wakati muda halisi wa kufanya hivyo pale utakapowadia.
Akigusia tabia ya makundi ya baadhi ya wanachama wa CCM yaliyoanza kuibuka yakijiandaa na uchaguzi Mkuu wa 2020 Balozi Seif alionya kuachwa mara moja kasumba hiyo itakayovuruga utendaji wa Seriali zilizopo madarakani wakati huu.
Balozi Seif alisema yapo makundi yanayotajwa kuongozwa na baadhi ya Viongozi ambayo hayaleti sura nzuri na kuendeleza tabia hiyo ni kukaribisha chuki za wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama.
Alisisitiza kwamba Viongozi na Wanachama lazima wafikie wakati wakuaminiana na kuacha kasumba zitakazokwamisha ushirikiano pamoja na kufanya kazi kwa pamoja na maelewano.
Balozi Seif alipendekeza wazi kwamba wale wanachama na Viongozi wanaoonekana kuwa na sura mbili katika mfumo wa utendaji kazi wao lazima waanze kuwekwa pembeni kabisa.
Akitoa Taarifa ya Mkutano huo Mkuu Maalum wa Mkoa Magharibi Unguja Kichama wa kongamano la kutathmini miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM Katibu wa CCM wa Mkoa huo Bibi Aziza Ramdhan Mapuri alisema maadhimisho hayo yameanza na shughuli za usafi wa maingira katika maeneo tofauti ya Mkoa huo.
Bibi Aziza alisema harakati hizo zilizoanza karibu wiki moja iliyopita ia zikatoa fursa kwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya mbili zilizomo ndani ya Mkoa huo kufanya mikutano ya kutathmini Historia ya CCM Tokea ilipozaliwa mwaka 1977 kwenye uwanja wa Amani Mjini
Zanzibar.
Katibu huyo wa CCM Mkoa Magharibi Unguja Kichana alitumia nafasi ya Mkutano huo kuwanasihi Wajumbe wa Mkutano huo, Viongozi wengine na Wanachama wa CCM kuwachagua Viongozi wenye uzalendo uliotukuka wakati utakapowadia wa kufanya chaguzi ndani ya Chama hicho Kikongwe.
Alisema hatua ya kuwachagua Viongozi wazalendo ndio njia sahihi itakayowa9a uwezo wale watakaochaguliwa kuwa na nguvu za kutekeleza wajibu wao bila ya kuogopa katika uatekelezaji wa Ilani na Sera za Chama cha Mapinduzi.
Akimkaribisha mgeni rasmi kulifungua Kongamano hilo la Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja Kichama Mwenyekiti wa Mkoa huo Nd. Yussuf Mohamed Yussuf alisema mfumo wa Sera na Ilani ya CCM unawezesha Chama hicho kuwa na matarajio ya kuongoza Dola kwa miaka mingi ijayo.
Nd. Yussuf alisema mfano wa hayo ni pale inapotokezea chaguzi ndogo za Jimbo la Serikali za Miataa jinsi CCM inavyoibuka kidedea na kuonyhesha ishara ya kuendelea kuungwa mkono na Wananchi walio wengi katika maeneo mbali mbali Nchini Tanzania.
Mkutano Mkuu huo Maalum wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja Kichama ulijumuisha mada mbili muhimu zitakazotoa fursa kwa wajumbe wa Mkutano huo kuzijadili na hatiame kutoa mapendekezo yao yatakayowasilishwa katika Uongozi wa juu wa chama hicho kwa kufanyiwa kazi.
Mada hizo ni pamoja na Historia ya CCM, mafanikio ya miaka 40 ya CCM, changamoto na sababu zake,mapendekezo ya namna ya kuzishughulikia changamoto hizo.
Mada nyengine ni mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 iliyopata ridhaa ya wananchi walio wengi katika kuongoza Dola.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni