SERIKALI IMEPIGA MARUFUKU UZALISHAJI NA UUZAJI WA POMBE KALI MAARUFU KAMA VIROBA.


1
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Januari Makamba (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo la kupiga marufuku uzalishaji na uuzaji wa pombe aina ya viroba leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano Profesa Faustine Kamuzora na Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi hiyo Richard Muyungi.
2
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Januari Makamba (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo la kupiga marufuku uzalishaji na uuzaji wa pombe aina ya viroba leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano Profesa Faustine Kamuzora na Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi hiyo .
Picha na: Mahmoud Ahmad
………………………………………………..
Na: Mahmoud Ahmad – Manyara leo Dar es Salaam
SERIKALI imepiga rasmi marufuku matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki maarufu kama viroba kuanzia tarehe 1 Machi 2017.
Hayo yamebainishwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano Januari Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
“Dhamira ya Serikali siyo kupiga marufuku vinywaji vya pombe kali bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi katika mazingira yaliyo safi, salama na yenye afya,” alisema Makamba.
Aliongeza kuwa uamuzi huo wakusitisha matumizi ya pombe hizo, Serikali itatumia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza utaratibu wa utekelezaji wa maamuzi hayo.
Alizitaja taratibu hizo kuwa ni pamoja na kutungwa kwa kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio vya plastiki kwa mujibu wa kifungu 230 (2) (F) CHA Sheria ya mazingira ya 2004.
Aidha Waziri Makamba ametoa wito kwa wazalishaji wa pombe kali wanaohitaji muda wa ziada wa kuhamia katika teknolojia ya chupa kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya kupewa kibali cha kuendelea na uzalishaji huku wakihama kabla ya tarehe 28 Februari.
Makamba alisema kuwa maombi hayo yaambatanishwe pamoja na ushahidi wa barua ikionyesha mwenendo wa ulipaji wa kodi, nyaraka kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) kuhusu usalama wa kinywaji, uthibitisho wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS),cheti cha tathmini ya athari za mazingira, uthibitisho kuwa atatumia teknolojia ya kudhibiti utengenezaji wa vifungashio bandia na uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini kuendesha operesheni kwa ajili ya kudhibiti uingizwaji wa pombe kali zinazotoka nje na kuzuia matumizi ya pombe haramu aina ya Gongo.
Utekelezaji wa uamuzi huo unafuatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kusitisha matumizi ya vifungashio vya plastiki ikiwemo pombe za viroba iliyotolewa bunge mwezi Mei 2016, Agosti na Desemba 2016 na kufuatiwa na agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa ziarani mkoani Manyara aliagiza kusitishwa kwa utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zunazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni