Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
akiwasilisha hoja katika mkutano wa Tano wa Bunge linaloendelea Mjini
Dodoma.
Na. Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
amesema kuwa Serikali imejipanga kusaidia vijana kutambua na
kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira zilizopo nchini ili kutatua
changamoto ya ukosefu wa ajira na kutimiza adhma ya kuleta maendeleo
hususani kwa vijana.
Mhe. Mhagama ameyasema hayo jana
wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Kinondoni Mhe. Maulid Mtulia
iliyohoji juu ya jitihada za Serikali katika kutatua tatizo la
ukosefu wa ajira kwa vijana wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge
unaoendelea Mkoani Dodoma.
Katika Mkutano huo Mhe. Waziri
alisisitiza kuwa Serikali ina mipango na mikakati madhubuti
inayokusudiwa yakusaidia vijana wa Kitanzania ili kujiletea maendeleo
yao wenyewe na kuondokana na umasikini.
“Serikali ya Awamu ya Tano
imeendelea kuweka mikakati ikiwemo uwanzishwaji wa programu
mbalimbali zitakazo saidia kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kwa
kuangalia matokeo ya tafiti mbalimbali ambazo zimepelekea kuwa na
programu zinazolenga kukabili tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana”
Alisema Waziri.
Alisisitiza kuwa programu hizo ni
pamoja na; kurasmisha ujuzi usio rasmi kuwa rasmi, mfumo wa mafunzo
kwa vitendo, mfumo wa uanangezi pamoja na kukuza mafunzo kwa
watanzania kulingana na soko lililopo kwa sasa.
Pamoja na juhudi hizo zinazotarajiwa
kuzaa matunda bado Waziri aliwatoa hofu wananchi wote kwa kuwepo kwa
fursa hizo za ajira zitakazo jali hali za watu pasipo kuangalia
makabila yao, rangi wala dini.
“Katika kutatua changamoto ya
ajira kwa vijana hatuta angalia kabila, rangi wala dini ya mtu bali
kutakuwa na haki na usawa”.Alisisitiza Waziri
Aliongezea kuwa, Serikali pia
inajitihada za kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali na
urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ili kupunguza kiwango cha ukosefu
wa ajira.
“Serikali itatumia sekta zenye
uwezo wa kutoa ajira kwa wingi ikiwemo zile za Kilimo, majenzi,
Mawasiliano na Utalii ili kuzitumia kuweka mazingira mazuri kwa
vijana kupata fursa za ajira”.
Mhe. Mhagama alisisitizia bungeni
kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika zitatumika kama
chachu ya kuangalia maeneo yanayohitaji kusaidia kwa haraka na
kupunguza changamoto hiyo kwa vijana.
“Kwa kuangalia tafiti ya Hali ya
Ajira Nchini ya mwaka 2014 imeonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa
ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3
mwaka 2014 na ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua kutoka asilimia
14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014”,alisema.
Hata hivyo, Waziri Mhagama alieleza
kuwa pamoja na jitihada hizo Serikali bado ina wajibu wa kuongeza
jitihada zaidi ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa ajira na kuboresha
maisha ya vijana.
=MWISHO=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni