Baada ya Kuanika Ukweli Juu ya Bifu Lake na Askofu Mkuu Anglikana ,Askofu Mkiwa Azuiwa na Polisi Kuingia Ibadani..!!!


Polisi jana waliingilia mvutano ndani ya Kanisa la Anglikana baada ya kumzuia Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa kushiriki ibada ya kumsimika askofu mpya wa Dayosisi ya Lweru.

Askofu Mokiwa amekuwa katika mvutano na Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya tangu alipotangaza kumvua  uongozi wa Dayosisi ya Dar es Salaam, akidai mkuu huyo hakufuata utaratibu na kwamba hana mamlaka ya kuchukua uamuzi huo.

Askofu Mokiwa aliwasili makao makuu ya Dayosisi ya Lweru mjini Muleba mkoani Kagera juzi jioni na jana alitarajiwa kuungana na maaskofu wengine kumsimika Godfrey Mbelwa kuwa askofu mpya wa dayosisi hiyo.

Lakini taarifa zilizopatikana asubuhi zilisema Askofu Mokiwa alichukuliwa na polisi na kuhojiwa katika kituo cha Muleba, kutokana na kuhofu kuwa kuwapo kwake kungeweza kusababisha vurugu katika ibada iliyokuwa iongozwe na Dk Chimeledya kutokana na mvutano uliopo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi aliliambia Gazeti la Mwananchi kuwa, jeshi hilo halikumkamata Askofu Mokiwa na kumhoji, badala yake alisema walichukua hatua haraka baada ya kupata taarifa za kiintelijensia kuhusu masuala ya usalama.

“Ni wajibu wetu kufuatilia. Tulimuonya; kuhusu suala la kuhudhuria au kutohudhuria, huo utakuwa ni uamuzi wake,” alisema Ollomi.

Kamanda Ollomi alisema walimuita Askofu Mokiwa juzi saa moja usiku kwa ajili ya kumpa ushauri wa kutohudhuria sherehe hizo kwa kuwa mgogoro uliopo katika kanisa hilo ungeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni