Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe Rosemary Staki Senyamule
Na Mathias Canal
Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe Rosemary Staki Senyamule amewaagiza walimu wakuu Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro kusimamia zoezi la upandaji miti kwa kumkabidhi kila mwanafunzi mti mmoja ambao atautunza katika kipindi chake cha masomo.
Dc Senyamule ametasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa elimu Wilayani humo kilichohudhuriwa na walimu wote wa shule za msingi na sekondari, Waratibu elimu, Maafisa Tarafa, Wazazi, Wanafunzi wawakilishi pamoja na baadhi ya Viongozi wa dini.
Kikao hicho kilichokuwa na lengo la kukubaliana na kupata namna bora ya kuboresha elimu na kiwango cha ufaulu Wilayani Same, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwepo kwa namna maalumu kwa ajili ya wanafunzi kufundishwa kwani mafanikio ya jitihada zao pekee katika kujisomea na kufundishwa darasani haitoshi bali wanahitaji kuongezewa msukumo na utaalamu zaidi kwa masomo ya ziada.
“Sote hapa kwa umoja wetu ni lazima tutambue kuwa matokeo bora ya wanafunzi waliopo darasa la saba, wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita yapo mikononi mwa walimu hivyo njia bora ni kutatua matatizo yanayowakabili walimu ili tuweze kufikia lengo” Alisisitiza Mhe Senyamule
Ameeleza kuwa endapo Changamoto za makundi yote zitatekelezwa kwa kufuata utaratibu ikiwemo kila mmoja kutumia nafasi yake ipasavyo katika kufuatilia mwenendo wa wanafunzi kwa kuanzia Walimu, Serikali, Wazazi, na Wanafunzi Wilaya hiyo itakuwa na matokeo makubwa katika matokeo yajayo.
Staki alisema kuwa Wilaya ya Same imeanza imeanza kukua kielimu kupitia matokeo ya kidato cha pili na cha nne kwani Wilaya hiyo imeshika nafasi ya 62 kati ya Halmashauri 184 ambapo kwa Mwaka uliopita ilikuwa nafasi ya 103.
Aidha katika matokeo ya kidato cha pili Wilaya ya Same imeshika nafasi ya 37 kati ya 184 kwani mwaka uliopita ilikuwa nafasi ya 47.
Pia amewataka viongozi wote katika kada mbalimbali kutumia vyema uongozi wao kwa kuwatumikia wananchi huku akiwasihi kutumia lugha nzuri pindi wanapozungumza nao kwani kiongozi yeyote atakayetumia lugha mbaya anapaswa kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
Sambamba na hayo pia Mkuu huyo wa Wilaya ya Same amepinga vikali matumizi ya Dawa za kulevya ambapo amesema kuwa kwa Wilaya hiyo baadhi ya wananchi wake ni wazalishaji wakubwa wa zao aina ya Mirungi ambalo pia limepelekea vijana wengi kutumia huku wakijiweka kando na elimu kwa kuamini kulima zao hilo sehemu ya mafanikio yao ya haraka.
Dc Staki amesema uongozi wa Wilaya hiyo unaendelea na oparesheni ya kuteketeza matumizi ya mirungi ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika na matumizi ama uuzaji wa zao hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni