JAFO-FEDHA ZA MIRADI YA AFYA ZITUMIKE KIKAMILIFU ILI KUJIBU CHANGAMOTO ZILIZOPO



Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Selemani Jafo,amesema mkoa wa Pwani umepokea Bil.2.340 zitakazotumika kugawanywa kwenye vituo vya afya na zahanati 234 zilizopo mkoani hapo ili kuboresha na kutatua changamoto zilizopo.

Amesema fedha hizo zimetolewa kutoka katika mpango wa malipo kwa ufanisi unaotekelezwa kwa ushirikiano baina ya bank ya dunia na serikali ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.Aidha Jafo amewasihi wakurugenzi,wenyeviti wa halmashauri na mganga mkuu wa mkoa huo,kusimamia fedha hizo ili ziweze kuleta tija .

Katika hatua nyingine,ametoa wiki moja hadi kufikia februari 21 mwaka huu,kwa waganga wakuu wa mikoa (RMO)na makatibu tawala wa mikoa (RAS)kote nchini,kuhakikisha wanapeleka account za bank zinazotumiwa katika vituo na zahanati zote.Alhaj Jafo,aliyasema hayo wakati akizungumza na wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri pamoja na waganga wakuu wa wilaya mkoani Pwani.

Alisema kati fedha hizo kila zahanati na kituo cha afya kitapatiwa kiasi cha sh.mil 10 ili kuboresha na kutatua kero sugu zilizokuwa zikiwasumbua.“Kuna zahanati na vituo vya afya ambavyo havina magodoro,mapaa yamebomoka,,hakuna vyoo huku nyumba za mganga wa kituo nayo ikiwa haina choo”“Kuna maeneo mengine hayana hata vitanda vya kujifungulia,akinamama wanapata shida yaani unahofia wanaweza kuondoka hata na magonjwa mengine,hivyo kwa mazingira haya fedha hizi endapo zitatumika kikamilifu zitaondoa matatizo hayo”alisema Jafo.

Alisema katika miaka iliyopita fedha hizo zilikuwa hakuna hivyo kutokana na mpango huo kuanza,wahakikishe wanaleta matokeo chanya kwa kujibu changamoto zilizokuwa zikiwakabili.Jafo alisema hatofurahishwa akisikia mradi huo haujafanikiwa katika mkoa wa Pwani na mikoa mingine 8 ambayo ipo kwenye mradi huo kwa majaribio hapa nchini.

Akizungumzia suala la utoaji huduma bora za kiafya,alieleza kuwa ni tatizo kubwa na aibu kwani katika mkoa huo jumla ya vituo 153 vina nyota 0(0 star)kati ya vituo 234 vilivyopo .Alifafanua kuwa vituo vinavyokosa star kubwa ndivyo vinavyokosa mapato zaidi kwani endapo hospitali inafanya vizuri inapata mil.360,kituo cha afya mil.79.8 na zahanati mil.19.

“Hili ni tatizo la nchi nzima,niwaombe waganga wakuu wa wilaya na mikoa kusimama kidete,kuhakikisha mnaondoa hizi 0,sifuri hizi hazina maana ,zinashusha mapato,kuanzia sasa mfanye juhudi mpate nyota 4 hadi 5”alisema Jafo.Alimtaka mganga mkuu wa mkoa wa Pwani,dk Beatrice Byarugaba,kuacha kukaa ofisini badala yake atoke kutembelea vituo na zahanati mbalimbali ili kujiridhisha na huduma inayotolewa.

Wakati huo huo, Jafo alitoa wiki moja kwa makatibu tawala wa mikoa na waganga wakuu nchini kupokea account zote za vituo na zahanati zilizopo kwenye mikoa yao .Waziri huyo alisema endapo mkoa wowote utashindwa kutekeleza agizo hilo basi katibu tawala na mganga mkuu wa mkoa husika watatakiwa kutoa maelezo.

Nae mchumi idara ya afya kutoka TAMISEMI,Nassoro Shemzigwa,alisema mpango huo unatekelezwa katika mikoa tisa ikiwemo Pwani,Shinyanga,Mwanza,Simiyu,Geita,Kagera na Mara .Alielezea kuwa lengo la mradi ni kuboresha huduma za afya ya msingi kuanzia hospital ya wilaya,zahanati na vituo vya afya.Shemzigwa alisema mpango huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2020 na utakuwa ni endelevu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibiti,Khatibu Chaurembo,alibainisha wamepokea maagizo na maelekezo waliyopewa na wataenda kuyafanyia kazi.Chaurembo aliiomba serikali kuangalia tatizo la uhaba wa watumishi katika zahanati mbalimbali hasa maeneo ya vijijini ambako zipo zahanati zenye mtumishi mmoja hivyo kusababisha huduma kuzorota.
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Selemani Jafo,akizungumzia na wakurugenzi,wenyeviti wa halmashauri,waganga wakuu wa wilaya mkoani Pwani,jana.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni