Mahmoud Ahmad
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,Jaji
Sekela Moshi amesema utoaji haki katika mifumo ya mahakama una nafasi kubwa
katika maendeleo ya nchi iwapo kila mhusika atatimiza wajibu wake kwa wakati.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya sheria mkoa wa Arusha
yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha alisema Katiba ya
Jumhuri ya muungano inaweka misingi ya utoaji haki ambayo Mahakama inapaswa
kuizingatia katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.
Alitaja misingi hiyo kuwa ni kutenda haki kwa wote bila
kujali hali ya mtu kijamii au kiutamaduni,kutokuchelewesha haki bila sababu ya
msingi na kutenda haki pasipo kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi
yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.
Jaji Sekela alisema serikali ya awamu ya tano imejikita
kwenye sera ya kukuza uchumi wa viwanda na mahakama kama chombo pekee cha
utoaji haki hakiwezi kujitenga kwa
vyovyote na sera hiyo ambayo katika hali
ya kawaida ni vigumu sana kuona moja kwa moja jinsi mahakama inavyochangia
ukuaji wa uchumi.
“Kwahiyo ni wazi kwamba utoaji haki kwa wakati unaenda
sambamba na ukuaji wa uchumi hivyo Mahakama ni mdau muhimu katika ukuaji wa
uchumi wa nchi yetu hii itafanyika iwapo Mahakama itashughulikia migogoro
mapema ambayo itavutia wawekezaji wengi kuja nchi wakiamini kwamba endapo kutatokea
mgogoro utatatuliwa mapema,”alisema Jaji Moshi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika
mkoa wa Arusha,Modesta Akida alisema kumekua na changamoto ya ucheleweshwaji wa
kesi kunakosababishwa na upungufu wa idadi ya watendaji katika mahakama na
Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya.
“Hali ya utoaji haki kwa wakati katika mashauri ya madai
bado inahitaji msukumo kwani bado yapo mashauri yenye umri wa miaka zaidi ya
mitano ambayo hayajatolewa maamuzi hadi sasa huku kumbukumbu ya masjala ya
Mahakama Kuu Arusha inaonyesha kuwa shauri la madai lililokaa kwa muda mrefu ni
la mwaka 2008,”alisema Akida
Alisema lengo la kuharakisha kuyatolea mashauri mahakamani
kwa wakati ni kusaidia ukuaji wa uchumi kunakochangiwa na mazingira mazuri ya
kibiashara na uwekezaji.
Naye Wakili Mwandamizi wa serikali,Dionis Makule aliwataka
wadau wote kushirikiana ili kuwezesha kupatikana kwa haki kwa wakati ili
kudumisha amani na utulivu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni