POLISI NCHINI WAPEWA MAFUNZO YA UTUNZAJI MAGHALA NA KUDHIBITI SILAHA NYEPESI



Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha,Naibu Kamshina wa Polisi ,Charles Mkumbo(kulia)akimsikiliza Katibu Mtendaji wa Kanda  ya kudhibiti Silaha nyepesi (Executive Secretary -Regional Centre on Small Arms-Recsa)Theoneste Mutsindashyaka  wakati wa mafunzo ya wiki moja kwa maafisa wa polisi ya kutunza maghala ya silaha na udhibiti wake  jijini Arusha,kushoto ni Meneja Programu wa Kanda ya Afrika kutoka Jeshi la Marekani,Dennis Hadrick

Askari Polisi kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwa katika mafunzo ya utunzaji wa maghala ya silaha na udhibiti wa silaha nyepesi inayofanyika jijini Arusha  kwa uratibu wa taasisi ya Kanda ya Udhibiti wa silaha nyepesi(Recsa)kwa ufadhili wa serikali wa serikali ya Marekani.

Baadhi ya wakufunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki watakaotoa mafunzo kwa askari wa jeshi la Polisi kutoka mikoa mbalimbali kwa wiki moja juu ya umuhimu wa utunzaji wa maghala ya silaha na Udhibiti wa silaha nyepesi yaliyoanza jijini Arusha

Baadhi ya wakufunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki watakaotoa mafunzo kwa askari wa jeshi la Polisi kutoka mikoa mbalimbali kwa wiki moja juu ya umuhimu wa utunzaji wa maghala ya silaha na Udhibiti wa silaha nyepesi yaliyoanza jijini Arusha.


Na Mahmoud Ahmad,Arusha
Jeshi la Polisi nchini litaanza msako mkali wa kuzikamata silaha zilizopo mikononi kwa wananchi bila vibali kutoka kwa mamlaka husika baada ya muda wa kuzitambua na kuziweka alama kukamilika.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha,Naibu Kamishna wa Polisi,Charles Mkumbo alisema hayo wakati akifungua mkutano kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kwa askari polisi kutoka mikoa mbalimbali wanaohudhuria mafunzo ya utunzaji maghala ya silaha na udhibiti wa silaha nyepesi na ndogondogo unaoratibiwa na Kituo cha Kanda(Recsa) chenye makao yake nchini Kenya.

Alisema katika kipindi cha hivi karibuni matukio ya utumiaji silaha umepungua kutokana na udhibiti uliofanywa na jeshi hilo na kuwataka wananchi ambao silaha zao hazijahakikiwa wafanye hivyo kabla hawajakabiliwa na mkondo wa sheria.

"Zoezi la kuhakiki silaha na kuziweka alama lilifanikiwa na ni njia muhimu katika kukabiliana na uhalifu unaosababishwa na matumizi ya silaha kiholela,jeshi halitafumbia macho watu ambao kwasababu zao kuendelea kumiliki silaha zisizohakikiwa vinginevyo wanazitumia kufanya uhalifu,"alisema Mkumbo

Kuhusu mafunzo hayo alisema yatalisaidia jeshi hilo kuwa na umahili katika utunzaji wa maghala ya silaha katika kiwango bora zaidi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza yakiwemo ya milipuko kama iliyowahi kutokea katika vipindi tofauti jijini Dar es salaam.

Katibu Mtendaji wa Kituo cha Kanda cha Kudhibiti Silaha nyepesi na ndogondogo(Recsa)Theoneste Mutsindashyaka alisema  taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2004 kwa Itifaki ya Nairobi kwaajili ya Kuzuia ,Kudhibiti na Kupinguza silaha hizo na kuanza rasmi mwaka 2005 ikiwa na wanachama 12 na sasa wamefikia 15 kwa lengo kudhibiti uzagaaji wa silaha nyepesi ambazo zimekua zikitumika kufanya uhalifu.

Alisema mafunzo kama hayo yameshatolewa katika nchi za Kenya,Uganda,Rwanda na sasa Tanzania na baadaye yatafanyika nchini Burndi na wanachama wengine.

Mutsindashyaka alisema licha ya Tanzania kuwa ni imara na haina matukio ya uhalifu wa kutisha lakini kutokana na ukubwa wake inapaswa kuongeza fedha katika kitengo cha kudhibiti silaha nyepesi.

Naye Meneja Programu hiyo kutoka Jeshi la Marekani katika nchi za Kusini,Kati na Mashariki mwa Afrika linalofadhili mradi huo,Dennis Hadrick alisema serikali yake kwa kutambua umuhimu wa usalama na amani imekua ikitoa fedha kugharamia mafunzo hayo.

Kwa upande wake Mratibu wa Recsa nchini,Kamishna Msaidizi Mwandamiz wa Polisi,Charles Ulaya alisema udhibiti wa silaha nyepesi nchini umekua na mafanikio makubwa na katika sikuza hivi karibuni shehena kubwa ya silaha hizo ziliteketezwa mkoani Kigoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni