Meneja uhusiano wa shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)Pascal Shelutete akisisitiza jambo wakati akiongea na wanahabari ofisini kwake,picha na maktaba ya manyara leo blog |
Mahmoud Ahmad,Arusha
Shirika la hifadhi za taifa(Tanapa) limetamka ya kwamba ni marufuku kwa askari wa hifadhi za taifa nchini kupiga raia na yoyote atakayethibitika kufanya kinyume na agizo hilo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na afisa uhusiano wa shirika hilo,Paschael Shelutete wakati akihojiwa na gazeti hili kuhusu malalamiko ya baadhi ya raia wanaoishi jirani na hifadhi mbalimbali za taifa hapa nchini ambao kimsingi wanalalamika kunyanyaswa na kupigiwa na askari hao.
Hivi karibuni kumeibuka malalamiko ya baadhi ya raia wanaoishi jirani na hifadhi mbalimbali za taifa za Mkomazi mkoani Kilimanjaro na hifadhi ya Tarangire iliyopo mkoani Manyara ambapo inadaiwa askari hao huwafanyia vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kuwapiga.
Afisa uhusiano huyo alisema kwamba ni marufuku kwa askari wa hifadhi za taifa nchini kuwapiga raia kwa kisingizio cha kuingiza mifugo yao kwenye hifadhi kwa kuwa kuna sheria na taratibu za kukamata mifugo inayoingizwa hifadhini.
“Ni marufuku kwa askari wa hifadhi kupiga raia na hata kama wakikamata mifugo iliyoingizwa ndani ya hifadhi kuna taratibu zake”alisema Shelutete
Hatahivyo,aliwataka wananchi wote wenye ushahidi na malalamiko hayo kuyafikisha mbele ya ofisi zao wakiwa na vielelezo ili waweze kuchukua hatua za kisheria kwa askari husika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni