Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimesitisha shughuli za
mazishi ya aliekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani Geita marehemu
Alphonce Mawazo, baada ya jeshi la polisi Mkoani Mwanza kuzuia zoezi la
kuuaga mwili wake lililokuwa limepangwa kufanyika juzi jumamosi Jijini
Mwanza.
Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe
alibainisha hayo jana wakati akizungumza na Wanahabari Mkoani Mwanza,
ili kutoa msimamo wa Chama baada ya kuwepo kwa mazungumzo baina yake na
familia ya marehemu Mawazo.
Alisema kuwa baada ya mazungumzo
hayo, Chadema pamoja na familia ya marehemu Mawazo wamekubaliana kwenda
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kufungua shauri la kuomba tafsiri ya
Kimahakama juu ya zuio hilo la jeshi la polisi kuzuia mwili wa marehemu
Mawazo kuagwa Jijini Mwanza kabla ya Kwenda kuzikwa Kijijini kwake
Chikobe katika Wilaya ya Busanda Mkoani Geita.
Nae Mchungaji
Charles Lugiko ambae ni baba mlezi wa marehemu Mawazo, alisema
anasikitishwa na hatua iliyochukuliwa na jeshi la polisi ya kuzuia mwili
wa marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza ambapo ameeleza kuwa na
matumaini makubwa ya kwamba mahakama itatenda haki juu ya suala hilo.
Frederick
Sumaye pamoja na Edward Lowasa ambao ni Viongozi Waandamizi wa Chadema,
walisema hatua ya jeshi la polisi kuzuia mwili wa Mawazo kuagwa Jijini
Mwanza si sawa na kwamba inaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Mwishoni
mwa wiki iliyopita, Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kupitia kwa Kamanda
wake Charles Mkumbo, lilizuia zoezi la mwili wa marehemu Mawazo Kuagwa
Jijini Mwanza, kwa madai kwamba limepokea taarifa za kiitelejensia za
kuwepo baadhi ya vikundi vya watu kutumia mwanya huo kufanya fujo na
hivyo kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
Aidha Kamanda
Mkumbo aliitaja sababu nyingine kuwa ni uwepo wa mlipuko wa Ugonjwa wa
Kipindupindu Mkoani Mwanza, ambao umesababisha jeshi hilo kutoruhusu
mikusanyiko ya aina yoyote inayoweza kusababisha ugonjwa huo kuenea
zaidi kwa mjibu wa wataalamu wa afya ambapo lilishauri zoezi la kuaga
mwili huo kufanyika Mkoani Geita ambapo mazishi ya marehemu Mawazo
yatarajiwa kufanyika.
Katika uchaguzi uliomalizika hivi
karibuni, marehemu Alphone Mawazo alikuwa mgombea ubunge Jimbo la
Busanda Mkoani Geita kupitia Chadema, akiwa pia ni Mwenyekiti wa chama
hicho mkoani humo ambapo aliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na mashoka
na watu wasiojulikana jumamosi iliyopita ya Novemba 14 mchana huku kifo
chake kikihusishwa na uhasama wa kisiasa.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni