KUFUATIA AGIZO LA RAIS DKT. MAGUFULI, MSD YAPELEKA VIFAA VILIVYOTAKIWA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

Magari ya Bohari ya Dawa (MSD), yakishusha vifaa tiba Taasisi ya Moi kufuatia agizo la Rais Dk.John Magufuli kulitaka Bunge kutumia sh.milioni 15 kwa ajili ya kujipongeza na fedha zilizobaki kuzipeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukabiliana na uhaba wa vifaa tiba na magodoro.
                                                                                           Na Dotto Mwaibale

BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza kupeleka Vifaa Tiba kwenye Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), Vifaa ambavyo vimenunuliwa na Ofisi ya Bunge kwa agizo alilotoa Rais Dk. John Magufuli.

Vifaa hivyo vilianza kupelekwa juzi katika Taasisi hiyo ili kukabiliana na uhaba alioubaini Rais Magufuli baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika mapema mwezi huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu akizungumzia kuhusu vifaa hivyo jijini Dar es Salaam juzi wakati wa usambazaji alisema hivyo vyenye gharama ya sh.milioni .251 ni pamoja na vitanda 300, magodoro 300, viti vya kusukuma (Wheel Chairs) 30, vitanda vya kubebea wagonjwa (Stretchers) 30, mashuka 1,695 na mablanketi 400.

Alisema MSD ilianza kupeleka Vifaa hivyo MOI mwishoni mwa wiki na kuwa itaendelea kutoa vifaa hadi wiki hii inayoanza leo.

Fedha hizo zilizotumika kununulia vifaa hivyo zilitokana na agizo la Rais Dk.John Magufuli alilolitoa wakati akilihutubia bunge mjini Dodoma mwishoni mwa wiki ambapo alilitaka bunge kutumia sh.milioni 15 tu kwa ajili ya kujipongeza na kiasi hicho kilichobaki kitumike kununulia vifaa hivyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni