NAMNA YA KISHERIA YA KUZUIA MSHAHARA WA MFANYAKAZI KULIPIA DENI LAKO.

NA  BASHIR  YAKUB - 
Unapomdai  mtu  kupitia  mahakanma  na  hukumu  ikatolewa  kuwa  ni  kweli  unamdai  na  anastahili  kukulipa basi  mtu  huyo  hustahili  kulipa.  Lakini  mara  kadhaa  hutokea  mtu  kusema  sina  hela  ya  kulipa  au  vinginevyo  ilimradi  tu  asilipe  deni.

Lakini  pia  madai  hapa  si  lazima  iwe  hela  tu  inayotokana  na  kukopeshana.  Yapo  pia  madai  ambayo  hutokana  na  mtu  kushinda  kesi. Kwa  mfano   mwanamke  alifungua  kesi  dhidi ya mme  wake  akitaka  matunzo  yake  na  ya mtoto/watoto. Au shauri  limekwisha  na  mtu  aliyeshindwa  ametakiwa  na  mahakama  kulipa  gharama. Au malipo  ya  fidia  na  mengineyo  yote  ambayo  huamuliwa  na  mahakama  kuwa  yalipwe. Haya  yote  unaweza   kuyafanya  yalipwe  kwa  kukamata  mshahara  wa  mhusika  kwa  njia  za  kisheria .

Hatua  hii imeelezwa  katika amri  ya 21  ya kanuni  ya 47  ya  sura  ya  33  ya  sheria  ya  mwenendo  wa  mashauri  ya  madai.

1.HATUA  YA  KUKAMATA  MSHAHARA  WA  MTUMISHI.

Mahakama  inapotoa  hukumu  ikimtaka  mtu  fulani  kutekeleza  jambo  fulani  au  kulipa  kiasi  fulani  kwa  mtu  fulani   amri  hiyo  hutakiwa  kutekelezwa  kwa  hiari  na  si  vinginevyo.  Yule  aliyeamrishwa  hutakiwa kutekeleza  kama  alivyoagizwa  na  ndani  ya  muda  alioelezwa.  Ikiwa  atatekeleza bila  kukosa  basi  hatua  hizi  za  kukamata  mali  zake  ikiwemo  hii  ya  kukamatwa  kwa  mshahara  wake  hazitachukuliwa.  Hii  ni  kwakuwa  atakuwa  ametekeleza  kwa  hiari.  Hatua  za  kukamata  mali  zake  ikiwemo  mshahara  wake  huchukuliwa  ikiwa  kama  njia   ya  kumlazimisha  mtu  kutekeleza  kile  alichokataa  kutekekeza  kwa  hiari .

2.  KUKAMATA  MSHAHARA  WA  MTUMISHI  WA  SERIKALI.

Watumishi  wa  serikali  huwa  na  taratibu  za malipo   ambazo  zipo  tofauti na  taasisi  binafsi.  Lakini  pia hata  ndani  ya  serikali  yenyewe  idara  na  taasisi  nazo  huwa  na taratibu tofauti katika  malipo.  Kwa  mfano wapo  watumishi   ambao  mishahara  yao  huanzia  hazina  na  wapo  ambao  utaratibu  wao  wa  mishahara  hauanzii  huko.  Hivyo  basi  ikiwa  malipo  ya  mtumishi  huanzia  hazina  basi  mamlaka  za  hazina  zitapewa  taarifa  ya  kimahakama  itakayoeleza  kile  alichofanya  mtumishi   ikiwa  ni  pamoja  na  ile  amri  ya  kukamata  mshahara  wa  mtumishi  kulipia  deni  kwa  mujibu  wa  hukumu  na  tuzo(decree) .  Wahasibu   na  watoa  malipo(cashier)  watalazimika  kufuata  vilevile   kama  ilivyoamriwa  na  mahakama  .

3.  KUKAMATA  MSHAHARA  WA  MFANYAKAZI  ASIYE  WA  SERIKALI.

Ikiwa  mshahara  unaotakiwa  kukamatwa  kufidia  deni  ni  wa  mfanyakazi  asiye  wa  serikali  basi  taarifa  rasmi  itatolewa  kwa  mwajiri  wake  kama  ni  kampuni,  asasi   ya  kiraia  au  vinginevyo.  Mwajiri  atatoa  taarifa  hiyo  kwa  afisa  anayehusika   na  malipo   ili  kuanzia  hapo  mshahara  wa  mhusika utumike  kulipia  deni  kwa  mujibu  wa  agizo  la  mahakama.

4.  KUKAMATA  MSHAHARA  NUSU  AU WOTE.

Kwa  mujibu  wa  sheria  niliyotaja  hapo  juu mshahara  wa  mfanyakazi  unaweza  kukamatwa  wote  kwa  ujumla  wake  au  sehemu  yake  kutegemea  na  maamuzi  ya  mahakama.  Ikiwa  deni ni kubwa  sana  basi   inaweza  kuamuliwa   kuwa  kiasi  fulani  kiwe  kinakatwa  kila  mwezi   labda  kwa  kipindi  cha  miaka  miwili  au  mmoja  kutegemea  na  deni lenyewe.  Au  kama   mshahara  ni  mkubwa  na  upo  uwezekano  wa  kulipa  deni  kwa   mkupuo  mmoja(single installment)  na  likaisha  basi  inaweza kuamuliwa   mshahara  ukamatwe  wote  na  ulipie  deni  kwa  mkupuo  mmoja  ili  deni  liishe  kabisa.  

Hata  hivyo  katika  mashauri  yanayohusisha   familia  kama  matunzo  ya  watoto,  ada,  mavazi, malazi  na  matunzo  ya  mwanamke  mara  nyingi huwa inaamriwa  kiasi  fulani  kila  mwezi  kikatwe  na kiingie  katika  akaunti  ya  mwanamke   au  kipelekwe  mahakamani kwa  ajili  ya  matunzo  kwa   familia hiyo.

5.  MALIPO  KUFANYIKA  HATA  KAMA  MFANYAKAZI  YUKO  NJE  YA  MKOA.

Ikiwa  kesi  imefunguliwa  mkoa  fulani  na  mfanyakazi  anakofanyia  kazi  ni  mkoa  mwingine   bado  hili  halizuii  mshahara  kukamatwa.  Popote  anapofanyia  kazi   na  popote  ofisi  yake  ilipo  mshahara  utatakiwa  kukamatwa   na  kulipia  kile  anachostahili  kulipia. Yote  hayo   ni  kwa  mujibu  wa  amri  ya 21  ya kanuni  ya 47  ya  sura  ya  33  ya  sheria  ya  mwenendo  wa  mashauri  ya  madai.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·         
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA  KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·         
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                  WANASHERIA  WETU.
·         
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA HARAKA  BURE.
·         
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
0784482959.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni