BALOZI SEIF AFUNGUA JENGO JIPYA LA MADARASA MANNE SKULI YA MSINGI MOGA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Moga mara baada ya kuzindua jengo Jipya la Skuli ya Kijiji hicho la madarasa Manne lililojengwa kwa nguvu za wananachi wenyewe.
Balozi Seif akipokea Risala ya Wananchi wa Kijiji cha Moga Mkoa wa Kaskazini Unguja kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la skuli ya Moja.

                                                                                                Picha na –OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewahimiza wanafunzi Nchini kuongeza bidii katika kujifunza masomo yote na kutilia mkazo zaidi masomo ya Sayansi na Teknolojia ambayo ndio yenye nafasi kubwa katika harakati za kila siku kwenye karne hii ya Sayansi.

Alisema katika kuhakikisha juhudi hizo zinafanikiwa, walimu nao wana jukumu kubwa la kujiendeleza kwa kuwa tayari kujifunza mambo mbali mbali yanayohusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Wazazi, Walimu na Wanafunzi wa Kijiji cha Moga baada ya kulifungua jengo jipya la Madarasa Manne la Skuli ya Msingi Moga iliyopo Wilaya ya Kaskazini “ A ” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema Walimu wanahitaji kupatgiwa msaada mkubwa kutoka kwa Wazazi pamoja na wadau wa Maendeleo katika Sekta hiyo ili skuli zote za hapa Nchini ziweze kupata mafanikio makubwa zaidi.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba juhudi zaidi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuzipatia Skuli vifaa na nyenzo za Kisasa za kufundishia kama vitabu, vifaa vya Maabara, Komyuta na walimu waliobobea katika fani tofauti ili wanafunzi wawe na uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
Alisema Serikali inatambua kuwa mafanikio ya kweli katika utekelezaji wa Mipango ya Taifa inategemea jitihada za pamoja kati ya Serikali nyenyewe na washirika wa maendeleo wakiwemo Wananchi katika kuimarisha Elimu Nchini.

Alisema kwamba Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itaendeleza kutekeleza dhamira yake ya kuifanya Elimu inayotolewa ianzie katika ngazi ya maandalizi hadi Sekondari.

Balozi Seif alifahamisha kwamba lengol ni kuihakikisha kuwa wanafunzi wote wanaweza kupata elimu ya lazima ya miaka 12 kuanzia maandalizi hadi Kidato cha Nne sambamba na kuongeza upatikanaji wa nafasi za kusomea.

Alieleza kuwa Wazazi na walezi hawana budi kuendeleza kwa pamoja utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo katika kuimarisha Taasisi za Uongozi na uendeshaji wa sekta ya Elimu pamoja na kuona rasilmali zilizotengwa kwa ajili ya Sewkta ya Elimu zinatumika kwa ufanisi na kwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza juhudi zinazochukuliwa na Kamati za Skuli Nchini kwa kazi kubwa zinazofanya za kusimamia na kusaidia shughuli za uendeshaji wa Skuli zao.

Balozi Seif aliahidi kwamba Serikali itaendelea kuziimarisha Kamati za Maskuli ili zitekeleze majukumu yake inazojipangia kwa ufanisi mkubwa zaidi kwa vile Maendeleo yoyote ya elimu yanahitaji msukumo wa pamoja kati ya Serikali na wadau wake.

Aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuweka mpango wa kuajiri walimu walio katika maeneo wanayoishi hatua ambayo mbali ya kupunguza gharama za nauli kwa walimu lakini pia itawapa utulivu wanafunzi kuwa karibu na walimu wao kwa muda mrefu.

Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi hao wa Kijiji cha Moga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliahidi kusaidia matofali elfu 2,000 kuchangia ujenzi wa jengo jipya lililoanza kujengwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe.

Balozi Seif pia akaahidi kusaidia Kompyuta moja na Printa yake kwa lengo la kuwajengea mazingira bora wanafunzi wa skuli hiyo ya msingi ya Moga kusoma katika mfumo wa kisasa wa sayansi na teknolojia.

Akitoa Taarifa za ujenzi wa jengo hilo Diwani wa Wadi ya Gamba Ndugu Machano Fadhil Babla alisema uamuzi wa Wananchi wa Kijiji cha Moga wa kuongeza jengo jengine la Skuli umekuja kufuatia matatizo mbali mbali yaliyokuwa yakiwapata Watoto wao kufuata elimu masafa marefu ya Mkwajuni.

Nd. Babla alisema watoto wa Kijiji cha Moga walikuwa waki9ata elimu chini ya Miembe, Madrasa za Quran pamoja na Majengo ya Chama cha Mapinduzi jambo ambalo lilikuwa haliwapi utulivu watoto hao katika masomo yao.

Diwani huyo wa Wadi ya Gamba ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” aliishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kusaidia ujenzi huo katika hatua za awali licha ya kwamba Wizara hiyo ndio mkamilishaji wa majengo yote ya skuli yanayoanzishwa na Wananchi.

Ndugu Babla alisisitiza kwamba katika kwenda na wakati Kamati ya Skuli, Walimu na Wazazi wa Kijiji cha Moga wameamua kuendelea na ujenzi wa jengo jengine Jipya litakalokuwa na madarasa Manne, Maktaba pamoja na Ofisi ya Mwalim Mkuu.

Akitoa salamu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi Mwanaid Saleh aliwapongeza Wananchi wa Wadi ya Gamba kwa uamuzi wao wa kuiunga mkono Wizara ya Elimu katika ujenzi wa Majengo mbali mbali ya Skul.

Bibi Mwanaid alisema hatua hiyo ya maendeleo inayofaa kuigwa na Wadi nyengine hapa Nchini imelenga katika kuwaondoshea changamoto za kupata elimu watoto wa Taifa hili.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu alilishukuru shirika la Maendeleo la Sweden { SIDA } kwa juhudi zake za kusaidia gharama za kukamilisha ujenzi wa jengo hilo licha ya kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Sekta ya Elimu hapa Zanzibar.

Ujenzi wa Jengo jipya la madarasa Manne la Skuli ya Moga lililojengwa kwa nguvu za Wananchi na kuunga mkono na washirika wa maendeleo wa sekta ya elimu hadi kukamilika kwake limegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 50,000,000/-

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni