Maji kutoka katika kisima hicho yakitiririka kufuatia kufanyika kwa majaribio ya kuyatoa maji kutoka ardhini.
Kiongozi wa waendesha mitambo ya uchimbaji visima wa kampuni ya ZENTAS Bw. Sima Teodor ( kushoto) akitoa maelezo kwa wandishi wa habari kuhusu kazi ya uchimbaji wa kisima hicho katika eneo la mradi wilayani Mkuranga.
Mtaalam wa mitambo wa
Kampuni ya ZENTAS Sahtn Topal ( katikati) akifafanua teknolojia na vifaa
vilivyotumika kuchimba kisima hicho.Picha na Aron Msigwa/ MAELEZO.
Na.Aron Msigwa- MAELEZO
Wananchi
wa wilaya ya Mkuranga,mkoa wa Pwani wanatarajia kunufaika na mradi
mkubwa wa usambazaji wa maji kufuatia kukamilika kwa zoezi la uchimbaji
wa kisima cha maji chenye urefu wa mita 541 ambacho kina uwezo wa
kuzalisha lita milioni 1.8 kwa siku.
Akitoa
taarifa za kukamilika kwa kazi ya uchimbaji wa kisima hicho mwakilishi
wa kampuni ya kuchimba visima ya ZENTAS kutoka Uturuki nchini Tanzania
Dkt.Mohammed Akbar amesema wao kama wataalam wanaendelea na majaribio ya
kuyatoa maji kutoka ardhini jambo ambalo limeonyesha mafanikio
makubwa.
Amesema mtambo wa kuchimba kisima
hicho uliwasili eneo la mradi Julai 9 mwaka huu na kuongeza kuwa mara
baada ya kuwasili katika eneo la mradi kazi ya uchimbaji ilianza na
kubainisha kuwa sasa kisima hicho kinazalisha kiasi cha lita 76,000
kwa saa na lita milioni 1.8 kwa siku.
Dkt.
Akbar amesema endapo maji hayo yataunganishwa kwenye miundombinu ya maji
ya mji huo yatakidhi mahitaji ya maji ya mji wa Mkuranga ambayo ni lita
laki Sita na Elfu mbili kwa siku (602,000).
"
Kwetu Haya ni mafanikio makubwa ukizingatia mradi wenyewe haujaanza
kusambaza maji kwani visima hivi vilikuwa ni kwa ajili ya utafiti,
kiwango cha maji kilichopatikana ni kikubwa, kilichobakia sasa ni kwa
mamlaka husika na Serikali kukamilisha mipango iliyobaki ili maji haya
yawafikie wananchi" Amesema.
Ameongeza kuwa
chini ya mradi huo wamechimba visima 9 na kati ya hivyo visima 7
vinafanya vizuri na 2 vimeharibika na kueleza kuwa matarajio yao ni
kuona visima vitano ambavyo sasa vimekamilika vizuri vikizalisha lita
milioni 55.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Mkuranga
mjini (MKUWASA) Muhandisi Filbert Pius akiuzungumzia mradi huo amesema
kuwa utakapokamilika utawasaidia wananchi kupata maji safi na kuondoa
tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali ya mji
huo.
Amesema mahitaji ya maji katika mji huo ni
makubwa kuliko uwezo wa sasa wa kuzalisha maji ambapo vyanzo vilivyopo
vina uwezo wa kuzalisha lita 135,000 kwa siku ikilinganishwa na
mahitaji ya sasa ya lita 602,000 kwa siku kwa wakazi wapatao 25,847.
"
Wananchi sasa watapata nafuu, tofauti kabisa na mwanzo, maji
yanayozalishwa hapa ni mengi lita 1,800,000 kwa siku hii inakidhi mara
mbili mahitaji yote ya wananchi wa mji wa Mkuranga " Amesisitiza
Muhandisi Pius.
Ameiomba Serikali kuendelea
kutoa fedha za kufanikisha ujenzi wa miundombinu yenye urefu wa kilometa
2 inayotarajiwa kukamilika ndani ya mwezi huu ili Mkuranga ambao sasa
ni mji wa viwanda upate huduma ya uhakika ya maji,
Pia
amesema kukamilika kwa ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhia maji
eneo la Mkwalia ulipo mradi huo pamoja na eneo la Kurungu kutaiwezesha
hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kupata huduma ya uhakika ya maji ambayo
imekuwa kero ya muda mrefu kwa wagonjwa wanafika kupata huduma.
Meneja
Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA)
Bi.Nelly Msuya akifafanua kuhudsu mradi huo amesema unajengwa
unatekelezwa na DAWASA kwa niaba ya Serikali na akifafanua kuwa maeneo
yote yenye miundombinu ya maji katika wilaya ya Mkuranga yanatarajiwa
kuanza kupata huduma hiyo ifikapo Oktoba mwaka huu.
Amesema
mradi huo sasa uko katika hatua za majaribio na unatarajiwa
kuwanufaisha wananchi wote mara kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu
kwenye maeneo ambayo hayakuwa na mabomba ya kusambazia maji , ujenzi wa
matenki makubwa ya kuhifadhia maji na kukamilika kwa taratibu za
kitaalam ili maji hayo yawafikie wananchi.
"Nachoweza
kusema kwa upande wa wilayanya Mkuranga tumefika pazuri, sisi kama
DAWASA watekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji kwa niaba ya Serikali
tutahakikisha kero ya maji katika wilaya hii na maeneo mengine
inapatiwa ufumbuzi, tumeshatoa mamlaka kwa miji na wilaya kubuni,
kusimamia na kuendeleza miradi ya maji ili wananchi wengi zaidi
wanufaike" Amesisitiza.
Aidha, amebainisha kuwa
mradi wa ujenzi wa visima 8 eneo la Mkuranga umegharimu kiasi cha
shilingi bilioni 7.4 na kufafanua kuwa awamu inayofuata ni kuyapeleka
maji hayo yakaunganishwe na mfumo wa kusambazia maji uliopo, ujenzi,
uongezaji wa matenki makubwa ya kuhifadhia maji na ununuzi wa pampu ya
kusukuma maji hayo kutoka kwenye chanzo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni