WAWEKEZAJI UTURUKI WAALIKWA KUWEKEZA HIFADHI ZA TAIFA


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa)Allan Kijazi  akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini, Yasemin Eralp(katikati)aliyefika makao makuu ya Shirika hilo leo,kulia ni Katibu Msaidizi wa Ubalozi wa Uturuki,Berat Colak.

Balozi wa Uturuki nchini, Yasemin Eralp(kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Tanapa,Allan Kijazi alipotembelea Makao Makuu ya shirika hilo  jijini Arusha.   

Katibu Msaidizi wa Ubalozi wa Uturuki,Berat Colak(kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa),Allan Kijazi alipotembelea Makao Makuu ya shirika hilo  jijini Arusha.   





Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Yasemine Eralp amesema atawaalika wawekezaji kutoka Uturuki ili waweze kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika Hifadhi za Taifa nchini. Balozi Eralp alitoa ahadi hiyo alipotembelea Makao Makuu ya TANAPA jijini Arusha na kukutana na viongozi wa shirika.

Balozi Eralp amesema kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa vipaumbele vyake na kwamba atatumia muda wake mwingi kuhakikisha kuwa sekta hiyo inastawi na kuvutia watalii wengi nchini kutoka Uturuki.

Katika mazungumzo yake na viongozi wa TANAPA, Balozi Eralp alitoa nafasi kwa TANAPA kutangaza katika Jarida la Shirika la Ndege la Uturuki Skyline Magazine,
na kwamba  fursa hii itasaidia  kuvutia wageni wengi zaidi nchini kutoka nchi zaidi ya 60 zinazofikiwa na shirika hilo la ndege ulimwenguni.

Balozi Eralp alikubaliana na TANAPA kuwa atafanya mazungumzo na Turkish Airline ili waweze kuandaa safari za kutembelea vivutio vya utalii katika hifadhi kwa waandishi wa habari na mawakala wa wageni kutoka Uturuki ili waweze kuzitangaza Hifadhi za Taifa katika Bara la Ulaya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi aliahidi kuwa TANAPA itatoa ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha kuwa malengo ya Mhe. Balozi Eralp yanatimizwa ikiwa ni pamoja na  shirika kutumia fursa ya kupata watalii kutoka Uturuki ambayo ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa na kuwa fursa za kupata wageni wengi zaidi  kutoka Uturuki zinaonekana dhahiri.


Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni