AVIC LASEMA LIPO TAYARI KUSHIRIKIANA NA SHIRIKA LA NDEGE ZANZIBAR

Picha na – OMPR – ZNZ.

Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege la avic kutoka Jamuhuri ya Watu wa China limejitolea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha mradi wa Kiuchumi wa pamoja wa Shirika la Ndege la Zanzibar.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo lenye Makao Makuu yake Mjini Beijing China Bwana Duan Bao Rong alieleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Duan Bao Rong alisema Uongozi wa Shirika hilo hivi sasa uko katika hatua za awali za kuwasiliana na Viongozi Waandamizi wa Taasisi zinazohusika na Sekta ya Mawasiliano na Uwekezaji kwa nia ya kuandaa taratibu zinatakazofanikisha kuanzishwa kwa Shirika hilo katika mfumo wa Ubia na Serikali.

Alisema Wataalamu wa Shirika hilo kwa kushirikiana na wale wa Zanzibar wataendelea kufanya utafiti wa pamoja katika kuona namna gani mradi huo mkubwa unatekelezwa ili kusaidia kuongeza mapato ya Taifa ambapo pia alieleza kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China itakuwa tayari kuunga mkono uanzishwaji wa mradi huo.



Alifahamisha kwamba wakati mafunzo ya kiufundi yakiendelea kutolewa kwa Wahandisi Wazalendo ili kuwaweka tayari wakati utakapoanza mradi huo Mipango itaandaliwa pia katika kuanzisha Kara kana itakayotoa huduma za Matengenezo ya Ndege zitakazopata hitilafu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Naibu Mkurugenzi huyo wa Shirika la Avic Bwana Duan Bao Rong alifafanua kwamba Shirika hilo tayari limeshatengeneza Ndege Mpya kadhaa tokea kuanzishwa kwake karibu Miaka Kumi iliyopita na hivi sasa zaidi ya Ndege 56 kati ya hizo zimeuzwa na shirika hilo katika Mataifa ya Zimbabwe, Zambia, Congo Brazaville,Kenya na Tanzania.

“ Lengo letu tulilopanga katika kuzingatia uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni kuongeza mapato makubwa kwa Zanzibar na pia ifikie hatua ya kujitegemea yenyewe katika kutoa huduma za usafiri wa Anga ”. Alisema Bwana Duan Bao Rong.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada inayoendelea kuchukuwa katika kutoa ushirikiano wa karibu kwa Uongozi wa Shirika hilo la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege la avic.

Akitoa shukrani zake kwa uamuzi uliyochukuwa na Shirika hilo la Ndege la Avic Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba kufanikiwa kwa mradi huo muhimu wa mawasiliano kutatoa fursa pana kwa Wananchi wa Ukanda wa Afrika Mashariki kupata huduma za uhakika za usafiri wa Anga.

Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi huo wa Shirika hilo la Kimataifa la Maendeleo ya usafiri na matengenezo ya Ndege la avic kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari wakati wote kuupa ushirikiano unaohitajika ili kuona azma hiyo mpya inafanikiwa kwa kiwango kinachokusudiwa.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni