Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiongozana
na Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga, baada ya dua hiyo.
Mufti
Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, akisoma dua kabla ya kuanza
kisomo maalum cha kuiombea nchi amani, katika viwanja vya Maisara mjini
Zanzibar. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad, OMKR
Waislamu mbali mbali wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, leo wamekusanyika katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar kwa ajili ya kuomba dua ya kuiombea nchi amani na utulivu katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Sheikh Abdallah Talib, amesema mara nyingi amani ya Zanzibar hutoweka kutokana na sababu za kisiasa hasa inapofika wakati wa uchaguzi mkuu, hivyo juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa katika kuendeleza amani ya nchi wakati wote.
Amesema suala la kudumisha amani na utulivu ni mchakato unaopaswa kuendelezwa, ili kuinusuru nchi kuingia katika machafuko yasiyokuwa ya lazima, na kwamba kila mwananchi ana jukumu la kuhakikisha kuwa amani ya nchi haichezewi.
Naye Amir wa Taasisi za Kiislamu Zanzibar Sheikh Ali Abdallah amesema dua hiyo ya kitaifa imefanyika nchi nzima katika viwanja mbali mbali Unguja na Pemba.
Dua hiyo iliyotanguliwa na sala ya Alasiri viwanjani hapo, imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini ya kiislamu, serikali na vyama vya siasa wakiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe. Abdallah Mwinyi Khamis na Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha ADC Mhe. Hamad Rashid Mohammed.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni