MKUTANO NO. 69 WA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA WAMALIZIKA KWA KISHINDO

Rais wa Baraza Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa, Bw. Sam Kutesa akigonga nyundo maalum kuashiria kukamilika kwa Mikutano ya Baraza hilo ambalo ameliongoza kwa mwaka  mzima. Kushoto kwake  ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akiwa mwenye furaha wakati wa kuhitimishwa  Baraza la 69 ambapo alimpongeza Bw. Sam Kutesa kwa kuliongoza  Baraza kwa uhodari  uliopelekea kupitishwa kwa maazimio mbalimbali.
Na Mwandishi Maaalum New York
Mkutano wa  69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  uliokuwa chini ya urais wa  Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Bw, Sam Kutesa   umefikia ukingoni siku ya jumatatu  kwa kupitisha maamuzi  ya kihistoria ambayo pamoja na mambo mengine yanatoa mwelekeo wa majadiliano kuhusu marekebisho na mageuzi ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Maamuzi hayo ambayo kwa mara ya kwanza yanaingizwa rasmi katika nyaraka muhimu za  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  na yaliyopewa namba A/69/L.92 yalipitishwa kwa kauli moja  na wajumbe  kutoka nchi 193 wanaounda  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Maamuzi hayo ambayo baadhi ya wazungumzaji waliyapachika  jina kama maamuzi ya Kutessa ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kusimamia kidete   majadiliano kuhusu mageuzi ya  Baraza Kuu la Usalama la Umoja  wa Mataifa  yanatoa msingi  au maandishi  ambayo kwayo   yatawawezesha nchi wanachama kujadiliana kwa  kupitia maamuzi hayo.
Ingawa  maamuzi hayo yamepita   bila  la kupigiwa kura na kupongezwa kwa kufungua  ukursa mpya  katika  kuendeleza mchakato wa majadiliano ya   mageuzi na upanuzi wa  Baraza Kuu la Usalama,  baadhi ya nchi  zimeyaelezea  maamuzi hayo   kuwa na  ni ya kiufunzi zaidi na hivyo yasikuchukuliwe kama   maamuzi ya mwisho   kwa madai kwamba ,maandalizi na majadiliano ya   maamuzi hiyo hayakuwa jumuishi na hivyo hayawakilishi maoni na hisia za makundi yote.
Akiungana  na wazungumzaji wengi waliounga mkono kupitishwa kwa maamuzi hayo  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manoni, amesema , majadiliano yaliyopelekea kupatikana kwa maamuzi hayo   hayakuwa rahisi, lakini  yameasisi hatua mpya ya mwendelezo wa ajenda  ya  kulifanyia mageuzi  Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liwe jumuishi kuendana   mazingira ya sasa.
Akasema  hapana shaka kwamba    majadiliano   Zaidi yanapashwa kuendelea ili kijibu kiu ya kila upande na kwamba nchi wanachama wanapashwa kujivunia hatua hiyo muhimu  hataka kama ni  hatua ndogo.
 Akatumia  fursa hiyo kuwapongeza Bw.Sam Kutesa na Mwakilishi wa kudumu wa Jamaica Balozi Rattray  kwa kazi nzuri , kubwa na iliyokuwa na changamoto  nyingi lakini iliyofanikisha kupatika kwa  maamuzi hiyo.
Majadiliano kuhusu namna ya kuboresha  na kupanua wigo wa  wajumbe wa Baraza Kuu la  Usalama la Umoja wa Mataifa, ni majadiliano  yaliyoanza  mwaka 2008 lakini  ni  katika  Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Maifa ambapo  matokeo ya majadiliano  miongoni  mwa wanachama yameweza kupitishwa rasmi katika Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa.
Muundo wa sasa wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa  ambalo linawajumbe wa kudumu  na wenye kura ya turufu watano na wajumbe  10 wanaoingia kwa mzunguko wa  uwakilishi wa kikanda haujaitendea haki Afrika  bara ambalo licha ya kwamba  asilimia kubwa ya maamuzi yanayofanywa na Baraza Kuu la  Usalama yanaihusu Afrika lakini  Afrika si mwanachama wa kudumu na hiyvo imekuwa ikipigania kupata  nafasi ya uwakilishi wa kudumu   pamoja na  kura  ya turufu.
Kumalizika kwa Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  kunafungua kuanza kwa Mkutano wa Baraza Kuu la 70 ambalo kwa mwaka mzima  litakuwa chini ya  Urais wa  Bw.Monges Lykketoft

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni