MGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR KUPITIA CHAMA CHA CUF, MAALIM SEIF AUNGURUMA KATIKA MAJIMBO YA AMANI NA MAGOMENI

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Kwawazee mjini Zanzibar.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwatambulisha na kuwanadi baadhi ya wagombea wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kwa majimbo ya Amani na Magomeni katika viwanja vya Kwawazee mjini Zanzibar.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwatambulisha na kuwanadi baadhi ya wagombea wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kwa majimbo ya Amani na Magomeni katika viwanja vya Kwawazee mjini Zanzibar.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwatambulisha na kuwanadi baadhi ya wagombea wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kwa majimbo ya Amani na Magomeni katika viwanja vya Kwawazee mjini Zanzibar.
Wafuasi wa CUF wakimsikiliza mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF Maalim Seif Sharif Hamad, katika viwanja vya Kwawazee (Picha na Ali Hamad, OMKR) Na: Hassan Hamad, OMKR

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza, ataifungua Zanzibar kiuchumi na biashara.

Amesema Zanzibar inazo rasilimali nyingi za kiuchumi lakini bado hazijatumiwa ipasavyo kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Kwawazee kwa ajili ya majimbo ya Amani na Magomeni, Maalim Seif amesema CUF kina sera imara za kuweza kuleta mabadiliko kwa kipindi kifupi.

Amesema tayari ameanza kukutana na baadhi ya makampuni ya uchimbaji wa mafuta, na kumuahidi kuwa yatashirikiana nae kuhakikisha kuwa azma ya uchimbaji wa mafuta inatimia muda mfupi baada ya serikali mpya itakayoongozwa na CUF kuingia madarakani.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameahidi kuwa ndani ya siku mia moja za mwanzo za uongozi wake, serikali itakuwa tayari imeshatunga sera na sheria ya mafuta, ili kuanza rasmi kazi ya utoaji tenda kwa ajili ya uchimbaji.

Aidha Maalim Seif amesema atapambana na tatizo la ajira kwa kuwawekea vijana mazingira ya kuweza kujiajiri na kufanya shughuli zao kwa uhuru bila ya kuwepo usumbufu wa aina yoyote.

Amesema iwapo atachaguliwa atatenga na kutengeneza maeneo maalum maalum kwa ajili ya vijana wa Juakali, na wengine wanaotaka kujiajiri ili waweze kuendesha shughuli zao za kibiashara na kuongeza kipato chao.

Akizungumzia mazingira ya uwekezaji, Mgombea huyo wa Urais, amesema ataondosha vikwazo vyote vinavyowakabili wawekezaji vikiwemo urasimu na rushwa, na kwamba watapatiwa fursa za uwekezaji muda mfupi kadri itavowezekana.
Ameeleza kuwa mara nyingi wawekezaji wamekuwa wakipata usumbufu wakati wanapotaka kuwekeza, na hivyo kupoteza muda mwingi na kukata tamaa, jambo ambalo serikali atakayoiongoza itasimamia jukumu hilo kuhakikisha kuwa kila mwenye nia ya kuwekeza anpata fursa hiyo kwa muda muafaka.

Kwa upande wake meneja kampeni wa Urais wa Zanzibar kupitia CUF, Nassor Ahmed Mazrui, amesema Maalim Seif ni kiongozi mkweli anayeweza kusimamia na kutekeleza ahadi zake.

Amesema iwapo wananchi watamchagua Maalim Seif kuwa Rais wao, milango ya kiuchumi itafunguliwa Zanzibar na kuifanya kurejea katika hadhi yake ya kuwa kituo cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema hatua hiyo pia itaongeza ajira na kunyanyua kipato cha wananchi ambacho kitakwenda sambamba na ukuaji wa uchumi.

Mapema akitoa salamu za wanawake, Bi Nunuu Salim Rashid amewashauri
akinamama kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na kuwashajiisha wengine kutekeleza haki hiyo kwa wakati, ili lengo lao la kuteta mabadiliko liweze kufikiwa.

Amesema bila ya kuichagua CUF katika uchaguzi mkuu ujao, Mamlaka kamili ya Zanzibar hayatopatikana, sambamba na kurejea kwa katiba inayopendekezwa ambayo amesema haikuzingatia matakwa ya wananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni