Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida akiingia katika
ukumbi wa mkutano hoteli ya Double Tree by Hilton kwa ajili ya warsha ya
vijana na ajira iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti ya
Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Na Mwandishi wetu
VIJANA nchini Tanzania wanatakiwa
kujitambua, kuacha kuwa kigeugeu na kufanya papara ya kupata fedha kama
wanataka kuendelea na kufanikiwa kibinafsi na kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewea jana na Meneja
Ajira za Kifundi kwa vijana na Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la
Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga kwenye warsha ya wadau wa kitaifa ya
kujadili suala la ajira kwa vijana Tanzania .
Kauli yake hiyo kwa vijana hao
waliojumuika katika hoteli ya DoubleTree by Hilton, Dar es salaam,
ilitokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika nchini ambazo zinaonesha
kwamba vijana wengi hawana msimamo wa maisha, hawana maono, hawana
malengo binafsi wala kutambua matarajio.
Amesema: “ Usipojitambua, leo nikija
nikakueleza habari za kuanzisha biashara ya matofali utachangamkia.
Kesho akija mtu mwingine akakueleza kuhusu uchimbaji wa madini utaacha
kutengeneza tofali na kukimbilia machimboni”.
Akizungumza kwa ufasaha kabisa kuhusu
vijana na ajira, alisema kila mmoja ana nafasi yake katika kuleta
maendeleo yake na taifa na kwamba lazima kujituma na si kubweteka na
kulalamika tu.
Akizungumza kwa mfano alimzungumzia
kijana mmoja Joseph ambaye alikuwa mwadilifu sana na mwenye kumwamini
Mungu. Anasema Kila siku Joseph aliamka asubuhi na kumuomba Mungu
amsaidie aondokane na umaskini alionao.
Alifanyakazi hivyo kwa miaka 30 lakini maombi yake hayakumsaidia kuondokana na umaskini.
Siku moja, alisema, Mungu alimuona Joseph
akiwa na masikitiko makubwa akamuuliza kulikoni, Joseph akamjibu:
“Mungu ni miaka 30 leo tangu nianzie kukuomba uniwezeshe nishinde bahati
nasibu. Mimi nimeishi maisha yangu kwa uadilifu nawe wajua . Lakini
mbona maombi hayatimii?”
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida akifungua warsha
ya vijana na ajira iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti ya
Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC). Kushoto ni Meneja Ajira za
Kifundi kwa vijana na Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO)
Dk. Annmarie Kiaga na kulia ni Kiongozi Mpango wa Ukuaji na Ajira wa
Taasisi wa Mpango wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka
Canada (IDRC) Dk. Arjan de Haan.
Naye Mungu akatabsamu akamwambia, Joseph, si ununue tiketi basi?
Dk Kiaga alisema kwa kuzingatia hadithi
yake kila mmoja anatakiwa kufanya kitu na Joseph alisahau kwamba huwezi
kushinda bahati nasibu bila kununua tiketi.
“Kumbuka haitoshi kuwa na elimu na ujuzi
kama hutaweza kuweka elimu hiyo au ujuzi ulionao katika vitendo” alisema
na kuongeza kuwa Joseph alikuwa anajua anahaitaji fedha ya kianzio
lakini hakuchukua hatua ya kupata hela hiyo.
Alisema pamoja na ukweli kuwa asilimia 40
ya watu wasio na ajira duniani ni vijana, kwa maana ya kwamba kuna
vijana wapatao milioni 75 duniani kote wanatafuta ajira huku vijana wa
kike wakiwa na changamoto kubwa zaidi, ipo shida kubwa ya vijana kukata
tamaa.
Aidha alisema kwamba hali ya kukata tamaa imewapeleka vijana kuongezeka katika soko la vijana wanaopata kazi zisizo na staha.
Alisema pamoja na sera zilizopo vijana wanatakiwa kuwa na shauku na kazi na pia kujitambua.
“Vijana wa siku hizi hawana mitazamo
sahihi kuhusu ajira. Kwamba vijana hawana shauku na kazi na wana
mitazamo hasi (ili mradi kazi..mkono uende kinywani?) . Matokeo yake ni
kwamba vijana hawatumii ubunifu wowote katika kuboresha uwezekano wao wa
kupata kazi zenye staha” alisema.
Amesema mtaji unahitaji kujiboreshea seti ya ujuzi katika kutafuta kazi ikiwa ni pamoja na uwezo, uzoefu na elimu.
Meneja Ajira za Kifundi kwa vijana na
Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga
akizungumza kwenye warsha ya vijana na ajira iliyofadhiliwa na Mpango
wa Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na
kuratibiwa na ESRF.
Alisisitiza kuwa vijana waliowengi
hawajitambui na kujiuliza ‘mimi ni nani’ au hawana malengo binafsi na
matarajio mimi nataka kuwa nani na kusema bila kuyafanyia kazi mambo
hayo mawili ya shauku ya kazi na kujitambua hakutakuwepo na mabadiliko.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk Tausi Kida, akifungua warsha
hiyo alisema pamoja na taifa kuwa mstari wa mbele kushughulikia ajira
kwa vijana kwa kutunga sera zilizolenga kukidhi haja ya ajira,ikiwemo
Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, Sera ya Taifa ya
Ajira ya mwaka 2008 na na mpango wa utekelezaji wa sera ya taifa ya
ajira kwa vijana iliyo chini ya mtandao wa ajira unaofadhiliwa na
shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, changamoto bado zipo.
Aliwataka washiriki wa warsha hiyo wakiwemo vijana waliofanikiwa kueleza siri za fursa na kujiajiri ili kutoa mwanga kwa wenzao.
Pamoja na warsha hiyo kutoa nafasi kwa
vijana kujadili namna ya kutambua na kutumia fursa za kuichumi zilizopo
nchini, kutoa ujuzi kwa vijana wa namna ya kuingia katika soko la ajira
ikiwa ni pamoja na kujiajiri, kukuza ujasiriamali na kuendeleza
biashara, Dk Kida aliwasihi vijana kujitafutia riziki yake na kushiriki
ipasavyo katika shughuli za kiuchumi na maendeleo.
Aliwataka kujijengea uwezo wa kufanyakazi pamoja na kubaini na kuzitumia fursa za kiuchumi na kibiashara zilizopo nchini.
Warsha hiyo iliyofadhiliwa na Mpango wa
Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC)
ilikutanisha vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania na
kuwezeshwa kwa sehemu kubwa na Taasisi ya tamasha ambapo Mkurugenzi wake
Mtendaji Richard Mabala alikuwa Mchokozaji mkuu.
Akiwasilisha salamu kutoka IDRC, kiongozi
Mpango wa ukuaji na ajira wa taasisi hiyo. Dk Arjan de Haan alisema
kwamba taasisi hiyo ya serikali ya Canada imekuwa ikitoa ushirikiano
katika tafiti zilizolenga kuangalia utatuaji wa tatizo la ajira kwa
namna inavyofaa.
Mtafiti Mwandamizi ESRF, Dk. Georgina Ole Saibul akiwasilisha mada katika semina ya vijana na ajira.
Alisema kwamba kwa kawaida taasisi yake
husaidia pale inapoona utafutaji wa mbinu za kutatua tatizo
unashirikisha na wahusika ili kupata suluhu endelevu ya tatizo husika.
Alisema ameridhishwa na kuona kwamba
warsha hiyo imezingatia kanuni za IDRC za kutaka kutatua tatizo la ajira
kwa kushirikisha vijana wenyewe, kuangalia na kushauri namna bora ya
kukabili tatizo la ajira ambao kwa sasa ni changamoto kubwa duniani.
Alisema kwamba ipo haja ya kubadili baadhi
ya sera kulingana na mahitaji ya sasa ili kuwezesha vijana wengi zaidi
kuingia katika soko la ajira.
Wakati wa utambulisho na kuelezea kero zao
katika ajira wengi wa vijana waligusia kuwapo kwa sera ambazo si
rafiki zinazotengeneza urasimu mkubwa katika kusaidiwa.
Ingawa wengi walisema fursa zipo,
walizungumzia kutopata ushirikiano kutoka kwa wazazi , viongozi na
taasisi mbalimbali zinazodai kupambana na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Aidha vijana wengine walisema kwamba ni
kweli kuna mtazamo hasi kwa vijana hasa kukata tamaa na pia kutaka
maendeleo ya kasi huku wakikosa ubunifu.
Joachim Fanuel kutoka singida Youth
Entrepreneurs and Consultants Cooperative Society (SYECLOS) alisema
kwamba ingawa wao wanaendesha miradi ya kuku wa kienyeji na asali kama
fursa zilizopo wanakabiliwa na tatizo la kukata tamaa kutokana na kuona
kwamba inachukua muda mrefu kupata vitu wanavyotaka.
Aidha alisema kwamba wamekuwa
hawasikilizwi na serikali na taasisi mbalimbali kwa kuwa hawana mali za
kuwakilisha kama dhamana katika mambo mbalimbali.
Johari A. Sadik kutoka kampuni
inayotengeneza nguo za kitamaduni Binti Africa, akitoa ushuhuda kwamba
vijana wanaweza kama watajitambua katika warsha ya siku mbili vijana na
ajira inayofanyika hoteli ya DoubleTree by Hilton.
Kijana Musa Mohammed kutoka Zanzibar
alisema kwamba japo wana fursa za usindikaji wa vyakula, mizizi na
matunda wamekuwa na tatizo la ujuzi katika uchakataji, sera duni
zisizojibu mahitaji yao na kuwalinda katika soko.
Binti mmoja kutoka Binti Africa Kampuni
inayotengeneza nguo za kitamaduni alisema kwamba kuna shida ya kukata
tamaa miongoni mwa vijana lakini pia hawajali kutafuta taarifa
wanazohitaji wakisubiri kutafuniwa.
Vijana wengine walizungumzia ugumu wa
mitaji, ukosefu wa taaluma na mfumo wa elimu kwuatengeneza kupata ajira
katika serikali na taasisi zake.
Mshiriki Leticia Mango kutoka Kigoma
alisema kwamba ipo shida ya vijana wenye vipaji ambao hawana elimu
vijijini kudharaulika na kutothaminiwa kwa kile kinachoonekana sio
wasomi.
Alisema vijana wasomi wakiunganika na
wenye vipaji wanaweza kuwa mbali zaidi na kusisitiza ipo haja vijana
kuwa pamoja kwa maendeleo yao.
Joachim Fanuel kutoka Singida Youth
Entrepreneurs and Consultants Cooperative Society (SYECCOS) akionesha
chupa ya asali kutoka kwa mradi wa kikundi cha vijana ambao waliamua
kujiajiri katika warsha ya vijana na ajira.
Joachim Fanuel kutoka Singida Youth
Entrepreneurs and Consultants Cooperative Society (SYECCOS) akizungumza
na washiriki wa warsha ya vijana na ajira.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida (kushoto) akiwa na
Kiongozi Mpango wa Ukuaji na Ajira wa Taasisi wa Mpango wa Shirika la
Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC), Dk. Arjan de
Haan wakiwa katika warsha ya vijana na ajira.
Vijana wakishiriki kazi za vikundi kwenye warsha hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida akiwa katika picha
ya pamoja na vijana walioshiriki warsha ya vijana na ajira hoteli ya
Double Tree by Hilton jijini Dar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni