| Waziri Membe akiendelea kuzungumza | 
| Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Tunsume Mwangolombe (katikati) naye akifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo. | 
| Sehemu ya wadau wakifuatilia ufunguzi wa Semina hiyo | 
| Semina ikiendelea | 
| Waziri Membe (katikati) na Waziri Maeland kwa pamoja na wajumbe waliofuatana nao wakiwa kwenye mazungumzo mara baada ya kumaliza ufunguzi wa semina. | 
| Waziri Membe (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya faida ya semina hiyo ya wafanyabiashara wa Tanzania na Norway | 
| Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea | 
 TANZANIA NA NORWAY KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Waziri
 wa Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe 
ameisifu Serikali ya Norway kwa kuwa mshirika wa karibu wa maendeleo wa 
Tanzania hususan katika sekta za biashara na uwekezaji.
Waziri
 Membe alitoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, 
Mhe. Abdallah Kigoda wakati akifungua rasmi semina kuhusu kuimarisha 
ushirikiano wa Kibiashara  na Uwekezaji kati ya Tanzania na Norway 
iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam leo.
Katika
 ufunguzi huo ambao ulihudhuriwa pia na Waziri wa Biashara na Viwanda wa
 Norway, Mhe. Monica Maeland ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi, 
Mhe. Membe alisema kuwa Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano wa 
kidiplomasia kwa miaka mingi lakini sasa nchi hizi zimeamua kushirikiana
 zaidi katika masuala ya uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi kwa 
maendeleo ya nchi zote mbili.
Aliongeza
 kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imefaidika na  ushirikiano na Norway 
katika sekta mbalimbali ambapo nchi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa 
katika kuisaidia Tanzania kupambana na umaskini na kukuza uchumi. Hata 
hivyo alisema umefika wakati sasa nchi hizi mbili zinufaike kupitia 
biashara na uwekezaji ambapo nchi zote zina fursa nyingi katika maeneo 
hayo ikiwemo gesi na mafuta, kilimo na madini.
Mhe.
 Membe alisema kuwa kufanyika kwa semina hii itakayowakutanisha 
wafanyabiashara na wawekezaji itaongeza thamani katika uhusiano wa 
kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili ambapo Tanzania ina mengi ya
 kujifunza kutoka Norway ambayo ni miongoni mwa nchi zinazosafirisha 
zaidi gesi asilia na mafuta duniani. Hivyo aliwaasa Watanznaia kutumia 
semina hiyo kujifunza ili kuimarisha sekta ya nishati ya hapa nchini. 
“Semina
 hii ni fursa kwa Kampuni za Tanzania na Norway kujifunza na kubadilisha
 uzoefu na mawazo ya namna bora ya kuboresha sekta za biashara na 
uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili” alisema Waziri Membe.
Akizungumzia
 biashara inayofanyika kati ya Tanzania na Norway, Mhe. Membe alisema 
kuwa Tanzania inatakiwa kuongeza biashara yake nje ya nchi ili 
kuimarisha uchumi wake. Alieleza kuwa kwa sasa biashara kati ya Tanzania
 na Norway imeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2010 hadi 
kufikia shilingi bilioni 6.9 mwaka 2014 kwa bidhaa zilizozwa Norway 
kutokea Tanzania ikiwemo kahawa, chai, viungo, maua, mbogamboga, mbao na
 madini. 
Kwa
 upande wa bidhaa kutoka Norway, Tanzania imenunua kwa ongezeko la 
kutoka bilioni 22.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi bilioni 73 mwaka 
2014. Bidhaa hizo ni pamoja na dawa za binadamu na bidhaa za viwandani.
Kwa
 upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara wa Norway, Mhe. Monica 
aliipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika maendeleo na ukuaji 
wa uchumi ambao umefikia asilimia 7. Alieleza kuwa Tanzania itafikia 
azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa vile 
inayo dhamira ya dhati na imejipanga kupitia uvumbuzi wa gesi na mafuta,
 nguvukazi ya vijana na mageuzi yaliyopo katika sekta ya uchumi.
Alieleza
 kuwa Norway ipo tayari kuendelea kuisadia Tanzania katika sekta ya gesi
 na mafuta kwa vile nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo 
hususan katika masuala ya teknolojia. Aidha, aliongeza kuwa Tanzania ni 
mshirika wa kweli wa Norway katika maendeleo hivyo nchi yake 
itashirikiana kikamilifu na Tanzania.
“Kuna
 msemo maarufu unasema kama unataka kwenda mbio nenda peke yako, lakini 
kama utanaka kufika mbali nenda pamoja na mwenzako. Hivyo Norway inataka
 kwenda pamoja na Tanzania ili kuziwezesha nchi hizi kufika mbali 
kimaendeleo” alisisitiza Mhe. Monica.
Awali
 akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Balozi wa Norway hapa 
nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstad alisema kuwa upo umuhimu mkubwa kwa 
nchi hizi mbili kukuza biashara kwa kuishirikisha sekta binafsi 
kikamilifu kwani ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu. 
Semina
 hiyo ambayo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Norway, 
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirikisho la Wenye Viwanda 
Tanzania (CTI) ilihudhuriwa na Makampuni 34 kutoka Norway na Tanzania na
 pia wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni