Imeelezwa
kuwa Tanzania ina vigezo mbalimbali ambavyo vinaifanya nchi ijiamini kwa
asilimia 98 kuwa mradi wa bomba la
kusafirishia mafuta kutoka Ziwa Albert nchini Uganda utapitia Kaskazini mwa Tanzania hadi Bandari ya Tanga
badala
ya nchini Kenya.
Hayo
yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin
Ntalikwa wakati wa kikao chake na wafanyabiashara wa mafuta nchini ambacho
kililenga kujadiliana nao kuhusu fursa za uwekezaji zitakazotokana na mradi huo
endapo utapita nchini.
Profesa
Ntalikwa alivitaja vigezo hivyo kuwa ni uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa
mabomba ya kusafirisha nishati mbalimbali ikiwemo Bomba la Mafuta la kutoka Tanzania hadi Zambia (TAZAMA),
Bomba la kusafirisha gesi kutoka SongoSongo
hadi Dar es Salaam, Bomba la kusafirisha gesi kutoka eneo la Mnazi Bay hadi
Mtwara, pamoja na Bomba kuu la gesi kutoka mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam
lenye kipenyo cha inchi 36 hivyo uzoefu huo utasaidia katika kupunguza muda wa ujenzi wa bomba la mafuta
ambalo kipenyo chake ni inchi 24.
“Tumewaeleza wenzetu kuwa Serikali ya Tanzania pia
ilishajenga uwezo mkubwa katika masuala ya kutwaa, kumiliki na kulipa madai ya
wananchi wanaopisha miradi ya mabomba na shughuli hizi zimekuwa zikifanywa kwa
wepesi na umakini mkubwa ikiwemo umakini katika kufuata kanuni na sheria za
mazingira, hivyo haitatuwia ngumu katika kutekeleza mradi huu,” alisema Profesa
Ntalikwa.
Alitaja
kigezo kingine kuwa ni ubora wa bandari ya Tanga ambayo imeonekana kuwa ni bora
zaidi ukilinganisha na Bandari nyingine Afrika Mashariki kwa kuwa ina kingo za
asili (naturally sheltered) na kina
kirefu hivyo kupunguza muda na gharama
za ujenzi kwa kuwa uchimbaji wa kuongeza kina hauhitajiki na itakuwa na
uwezo wa kupakia mafuta katika kipindi cha mwaka mwaka mzima.
Profesa
Ntalikwa aliongeza kuwa njia ya kupitia Tanzania hadi Bandari ya Tanga ni bora
zaidi kwa upande wa ujenzi wa bomba hilo kwa kuwa haipiti sehemu yenye makazi ya
watu wengi, sehemu za hifadhi na haina miinuko mikali hivyo kupunguza muda wa ujenzi na gharama za
ujenzi.
“ Hivyo ndugu zangu tumewaita wafanyabiashara hawa wa
mafuta nchini ili waweze kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na mradi huo
na kuzichangamkia na wao wamepokea vizuri suala hili na wameahidi kushirikiana
na Serikali katika kuhakikisha kwamba Tanzania inapata mradi huu muhimu,”
alisema Profesa Ntalikwa.
Awali
akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini kutoka Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. Wellington Hudson alieleza kuwa
Uwekezaji wa mradi bomba hilo
unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 4 na kwamba Bomba lote litakuwa
na urefu wa kilomita 1403 na kipenyo cha
inchi 24.
Alisema
kuwa hatua zilizofikiwa hadi sasa ni kuwa Serikali za Tanzania na Uganda
zilishatiliana sahihi Mkataba wa Maelewano (MOU) tarehe 12 Oktoba 2015 ambao
kwa sasa ndiyo mwongozo wa kukamilisha majadiliano ya mikataba mbalimbali
ambayo inayohitajika kisheria.
“Kwa sasa
lengo ni kukamilisha mazungumzo mapema na kusainiwa kwa Mikataba husika, ili kuruhusu
shughuli za upatikanaji wa mkuza na ujenzi kuanza maramoja. Ujenzi unatarajiwa kukamilika
ndani ya miaka mitatu baada ya Mikataba yote muhimu kusainiwa,” alisema Dkt.
Wellington.
Alitaja
baadhi ya faida zitakazopatikana kutokana na mradi huo kujengwa Tanzania kuwa
ni kuchochea shughuli za utafutaji mafuta nchini hususani katika maeneo linapopita
bomba la mafuta, Kuimarisha matumizi ya Bandari ya Tanga na hivyo kuongeza mapato
ya Serikali kutoka katika bandari hiyo pamoja na kupatikana mkuza utakaoweza
kutumika siku za baadaye kwa shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kusafirisha
gesi na mafuta katika mikoa ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na nchi za jirani.
Faida
nyingine zitakazotokana na mradi huo ni Ujenzi wa barabara mpya takriba kilometa
200 na uboreshaji wa barabara zilizopo takriban kilometa 150 na madaraja katika
maeneo linapopita bomba,
Pia kuongezeka
kwa fursa ya Shirika la Reli Tanzania kufanya biashara ya kusafirisha kiwango
cha mabomba yanayokadiriwa kufikia 123,000 kupitia miundombinu ya reli iliyopo,
Fursa za ajira kwa takribani watu 15,000 wakati wa ujenzi na watu wapatao 1,000
wakati wa kuendesha mradi.
Dkt.
Wellington pia aliwaasa Watanzania kuchangamkia fursa zitakazojitokeza endapo
bomba hilo litapita nchini na kuzitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni kazi za
kuunganisha mabomba (welding), huduma
za afya, huduma za mabenki, huduma za usafi na kudhibiti taka, Kandarasi za
kujenga na za umeme, huduma za Bima, Huduma za mawasiliano na mtandao, kandarasi
za ujenzi wa Mabarabara na Huduma za uuzaji mafuta.
Alitaja fursa nyingine zitakazopatikana kuwa ni Karakana
za ukarabati wa mashine mbali mbali na magari, Huduma za sheria, Huduma za
Mawasiliano na Kandarasi za kusamba vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la
Biashara, Dkt. Gideon Kaunda akiongea kwa niaba ya wafanyabiasahara hao
aliishuukuru Serikali kwa kuamua kuwashirikisha katika suala hilo muhimu kwa
manufaa ya nchi na kuahidi kushirikiana nayo ili kuhakikisha kuwa lengo la
Serikali la kuhakikisha bomba hilo la Mafuta linapita Tanzania linafanikiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni