mkuu wa mkoa wa Manyara Joel Bendera |
Na Mahmoud Ahmad,manyara
Mkoa wa Manyara unatarajia kutumia sh202.1 bilioni kwa ajili ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017, ambapo mishahara itakuwa ni sh5.5 bilioni, matumizi ya kawaida sh2.1 bilioni na sh2.7 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katika
mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 mkoa umekadiriwa kukusanya mapato
ya ndani ya sh18 bilioni ambapo sh17.9 bilioni ni kwa ajili ya serikali za
mitaa na sh192 milioni ni za sekretarieti ya mkoa.
Akisoma
mpango wa bajeti ya mkoa huo juzi, Katibu Tawala wa mkoa huo Eliakim Maswi
alisema kijiografia Manyara yenye kilomita za mraba 50,921 ni kubwa kuliko
baadhi ya mikoa, hivyo inahitaji gharama kubwa za uendeshaji.
Maswi
alisema katika mpango huo wa bajeti, Babati mjini wanatarajia kutumia sh25
bilioni, Babati vijijini sh37 bilioni, Hanang’ sh33 bilioni, Kiteto sh30
bilioni, Mbulu vijijini sh38 bilioni, Mbulu mjini sh6 bilioni na Simanjiro sh19
bilioni.
“Pia
tunakabiliwa na changamoto ya kuchelewa au kutopatikana kwa fedha za ruzuku za
matumizi ya kawaida na ruzuku ya miradi ya maendeleo, ufinyu wa bajeti wa
kuboresha na kujenga miundombinu ya zahanati na shule,” alisema.
Alisema
umbali kutoka makao makuu ya halmashauri ya wilaya hadi makao makuu ya mkoa
ambapo ni lazima upitie wilaya nyingine kama Kondoa, Monduli na Arusha ili
ufike mkoani wakati wa kufuata huduma mkoani pia ni kikwazo.
Hata
hivyo, mkuu wa mkoa huo Dk Joel Bendera alizitaka halmashauri zote saba
kuhakikisha zinachangia bajeti zao kwa asilimia 60 ya mapato ya vyanzo vya
ndani kama serikali kuu ilivyoagiza ili kutekeleza miradi ya maendeleo yao.
“Nitakuwa
mkali katika kuhakikisha hilo linatekelezeka hivyo kila halmashauri ihakikishe
inakusanya mapato yao na kufikia asilimia 60 kwani mimi ndiye ninayekwenda
kuomba kupitishwa kwa bajeti yetu,” alisema Dk Bendera.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni