NAIBU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Bw.
Luhaga Mpina amesema mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa nane hapa
nchini ambayo inakabiliwa na tishio la kugeuka jangwa kutokana na tatizo
la ukataji miti hovyo.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Simiyu, Mwanza, Mara, Singida na Arusha. Mingine ni Kilimanjaro, Dodoma na Manyara.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumanne, Machi 2, 2016) alipopewa nafasi na waziri Mkuu Kassim Majaliwa
awasalimie wananchi waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi
kwenye jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani
Simiyu.
Alisema kila wilaya imepewa agizo
la kupanda miche milioni 1.5 kwa mwaka na kwa sababu hiyo watawapima
wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurudenzi wa halmashauri na
Manispaa ambao hawatafikisha idadi hiyo ya miche na kuwasilisha majina
yao kwa Waziri Mkuu.
“Ilani ya Chama cha Mapinduzi
imeagiza kila wilaya ipade miche milioni 1.5 kwa mwaka. Kwa hiyo kuanzia
Machi 3, mwaka ambayo ni siku ya upandaji miti, tutawamoniter Wakuu wa
Mikoa na Wakuu wa Wilaya wote ili kubaini ni nani hajatekeleza agizo
hili. Tutakuletea mezani kwako majina ya wale ambao watashindwa
kutekeleza agizo hili ambalo liko kwenye Ilana ya CCM,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
huyo alisema amekuja na miche 7,000 ya matunda aina ya miembe, michungwa
na mifenesi ambayo ameahidi kuigawa kwa kila wilaya. “Tunataka katika
ziara yako hii tusambaze miche 5,000 kwa kila jimbo la mkoa huu na
wakati unamaliza ziara yako tutakuwa tumesambaza miche 35,000,” alisema.
Naibu waziri Mpina alisema
kupandwa kwa miti mbalimbali ya matunda, kutawasaidia wananchi kupata
matunda ya kula, ya kuuza na kupata fedha lakini pia itawasaidia kuwa
chanzo cha mali ghafi kwenye viwanda vya kusindika matunda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni