Wasichana wa Shule ya Sekondari Luchelele wakiwa katika
picha ya pamoja na wawezeshaji toka DidaVitengeWear Foundation mara baada ya
kupokea taulo za usafi (Pedi) na Elimu ya Usafi wa mwili na uzazi chini ya
mradi wa Binti Box unaotekelezwa katika shule za Sekondari na Msingi kanda ya
Ziwa.
Katika
kusheherekea siku ya Wanawake Duniani Machi 08,2016, taasisi ya
kusaidia wanawake na wasichana yenye makao makuu jijini Mwanza,
DidaVitengeWear Foundation, Imefanikisha kugawa taulo za usafi zaidi ya
2,000 kwa wasichana zaidi ya 600 wa shule ya msingi Igombe na Shule ya
Sekondari ya Luchelele zote za Jijini Mwanza kupitia mradi wa kuwasaidia
Mabinti kufikia malengo yao, ujulikanao kama ‘Binti Box’.
Hatua
hiyo pia imefikiwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya taasisi hiyo
pamoja na Mtandao wa Wanawake jijini Mwanza wa ‘Women Roundtable’, na
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM) Mh.Stanslaus Mabula, Mbunge Viti
Maalum Wanawake Mkoani Mwanza Zawadi Kiteto na Mbunge wa Viti Maalum
Vijana Mkoani Mwanza Mh.Maria Kangoye Ndila
Binti
Box ni mradi ulioanzishwa kwa lengo la kuwasaidia watoto wa kike
waliopevuka kubaki shule na kuimarisha mahudhuria ya wasichana shuleni
kwa kuwapatia vifaa vya usafi vitakavyowasaidia wakati wa siku zao za
hedhi. Wasichana wengi hasa wa vijijini hukosa kwenda shule kwa siku 5
mpaka 7 kwa mwezi kwa sababu ya kukosa vifaa vya usafi wakati wa
mzunguko wa hedhi, hivyo mradi huu kwa upande wa kanda ya ziwa ni
mkombozi kwa mabinti wengi kuhudhuria shule na kuinua kiwango cha ufaulu
katika masomo yao.
Akiongea
wakati wa kugawa taulo hizo za usafi mashuleni, Bi. Khadija Liganga,
Mratibu wa Mradi na Mkurugenzi wa DidaVitengeWear Foundation, alieleza
kwamba, elimu ya wasichana ni jambo la msingi katika jitihada za kuleta
maendeleo kwa nchi masikini kwa sababu mafaniko ya wanawake hasa katika
elimu inamaanika kuwa na faida ya muda mrefu na huenda mbali Zaidi
katika kuinua uchumi wa jamii na nchi.
“Kuna
sababu nyingi zinazochangia kudumaa kwa ustawi wa elimu ya mtoto wa
kike hasa wale wa vijijini, tatizo la ukosefu wa vifaa vya usafi kwa
mabinti wakati wa hedhi kwa kila mwezi nayo imeibuka kuwa ni tatizo sugu
linalofumbiwa macho na wadau wengi wa maendeleo katika nchi
zinazoendelea na Tanzania ikiwemo. Wasichana hawa hujawa na uwoga na
kuhofia kupoteza thamani yao na utu wao wawapo shuleni au mbele za watu
na kuwafanya wasihudhurie darasani au kutokwenda shule na matokeo yake
wengi huacha shule,” amesema Bi. Khadija Liganga
Bi.Khadija
aliendelea kusema kwamba “Baada ya kutembelea baadhi ya shule zilizo
pembezoni na miji tumegundua tatizo ni kubwa, tukapata uwelewa wa
kutosha na tukaona ni vyema badala ya kuandaa makongamano ya wanawake
wakati wa sherehe za Siku ya Wanawake Dunaini 2016, kwanini tusiguse
eneo ambalo ndio chimbuko la ukandamizaji wa maendeleo ya Mwanamke,
ambalo ni Elimu. Ndipo tukaja na huu mradi utakaokuwa endelevu wa ‘Binti
Box’ kwa lengo la kutoa taulo za usafi kwa mabinti wa shule za msingi
na sekondari pamoja na elimu ya usafi wakati wa siku za hedhi”
“Tungependa
kuwashukuru watu wote pamoja na taasisi mbalimbali kwa mchango wa o wa
maboksi ya taulo za usafi. Huu ni mwanzo tu, huku mipango ikiwa ni
kuongeza uwezo wa mradi kuweza kutoa huduma hii kwa shule za sekondari
na msingi katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, tuko tayari kushirikiana
na watu binafsi au taasisi yoyote katika kumkomboa mtoto wa kike” alisema Bi. Khadija Liganga
Lengo
la Mradi wa Binti Box ni kuwapatia elimu ya uzazi,afya,kuwajengea uwezo
wa kujiamini na kuwapatia taulo za usafi wasichana wa sekondari na
shule za msingi waliopo katika umri wa kuvunja ungo katika mikoa ya
Mwanza na Mara. Mradi unatekeleza mpango wa taifa kwa vitendo wa
kuhakikisha watoto wa kike hawabaki nyuma bali wanapata fursa sawa na
wenzao wa kiume na kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike.
Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa DidaVitengeWear Foundation
ambae pia ni Mratibu wa Mradi wa Binti Box akijadiliana jambo na Mbunge wa Viti
Maalum Vijana mkoa wa Mwanza kupitia CCM, Mh. Maria Kangoye Ndila (Katikati)
pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Wanawake mkoa wa Mwanza Mh. Zawadi Kiteto
(Kushoto), wakati wa utekelezaji wa mradi wa kugawa taulo za usafi kwa Mabinti
wa Shule ya Msingi Igombe.
Mkufunzi wa Afya ya Uzazi ambae pia ni muuguzi msaidizi
kutoka kituo cha Afya cha Makongoro akitoa elimu ya usafi wa mwili na kuepuka
mimba za utoto kwa wanafunzi wa kike wa shule ya msingi Igombe chini ya mradi
wa Binti Box ulioandaliwa na DidaVitengeWear Foundation kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali jijini Mwanza.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Igombe wakiwa katika picha ya
pamoja huku wakiwa na nyuso za furaha baada ya kupewa vifaa vya usafi
vitakavyowasaidia katika mzunguko wao wa kila mwezi na kuepuka magonjwa
mbalimbali yanayotokana na kutumia vifaa visivyo salama.
Kushoto ni Bi. Khadija Liganga Mkurugenzi wa taasisi ya
kusaidia wanawake na maendeleo ya wasichana yenye makao makuu jijini Mwanza,
DidaVitengeWear Foundation akihimiza jambo juu matumizi mazuri ya vifaa vya
usafi kwa wasichana wa shule ya sekondari ya Bujora (hawapo pichani), Kulia ni
Mbunge wa Viti Maalum Vijana mkoa wa Mwanza, Bi. Maria Kangoye Ndila ambae
aliungana katika mradi huo kuwasaidia mabinti walio shuleni.
Mabinti wa shule ya sekondari ya Bujora iliyopo Wilayani
Magu mkoani Mwanza wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa taulo za
usafi toka taasisi ya DidaVitengeWear Foundation.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni