Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika moja ya kikao na wakandarasi wanaosambaza Umeme
Vijijini vilivyoanza tarehe 29 Machi na kumalizika tarehe 31 mwezi
huu.Wa Tatu kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), Dkt. Lutengano Mwakahesya na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Ufundi kutoka
REA, Mhandisi Bengie Msofe. Wengine ni watendaji kutoka kampuni ya
Angelique International inayosambaza umeme mkoani Arusha, Wizara na REA.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika kikao na kampuni ya
Engineering & Construction inayosambaza umeme vijijini mkoani
Kagera katika wilaya za Ngara, Biharamulo, Misenyi, Karagwe, Kyerwa,
Bukoba vijijini na Muleba kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya
Nishati na Madini jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Lutengano Mwakahesya na
anayemfuatia ni Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Mhandisi Amos
Maganga.Wengine ni watendaji kutoka kampuni hiyo, Wizara na REA.
Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana
Pallangyo (wa kwanza kushoto), Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Mhandisi
Amos Maganga (wa pili kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Dkt. Lutengano Mwakahesya (wa Tatu kushoto) wakiwa
katika moja ya vikao vilivyojumuisha wakandarasi wanaosambaza umeme
vijijini vilivyoanza tarehe 29 Machi na kumalizika tarehe 31 Machi, mwaka huu.
Na Teresia Mhagama
Imeelezwa kuwa wakandarasi wenye tuhuma za kutolipa mishahara wafanyakazi wao, kuomba rushwa kwa wateja wanaotaka kuunganishiwa umeme na kutolipa fedha za watoa huduma waliokuwa wakifanya nao kazi katika usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili, hawatapewa kazi husika katika miradi ya REA Awamu ya Tatu.
Hayo
yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na kampuni mbalimbali
zinazotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili
inayotarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.
“Kampuni
zitakazopewa kipaumbele ni zile zilizofanya vizuri katika miradi ya REA
Awamu ya Pili na kuonekana kuleta ushindani kwa kampuni nyingine za
ndani na nje ya nchi kwa kufanya kazi waliyopewa kwa bidii na kutokuwa
na tuhuma mbalimbali ikiwemo rushwa,” alisema Profesa Muhongo.
Awali Meneja Operesheni wa kampuni ya Engineering & Construction, Julius Kateti inayosambaza
umeme vijijini mkoani Kagera katika wilaya za Ngara, Biharamulo,
Misenyi, Karagwe, Kyerwa, Bukoba vijijini na Muleba alimweleza Profesa
Muhongo kuwa kazi ya usambazaji umeme katika mkoa huo imehusisha vijiji
451 na wanatarajia kuunganisha wateja 30,000 kabla ya muda wa ukomo
uliowekwa na Serikali.
Alisema
kuwa katika wilaya za Ngara na Biharamulo jumla ya wateja 4385 wa njia
moja ya umeme waliunganishwa kati ya wateja 4554 na wateja 49 wa njia
tatu za umeme waliunganishwa ambapo jumla ya transfoma 47 zilifungwa na
kwamba kwa wilaya za Ngara
na Biharamulo wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo Aprili 20 mwaka
huu na kuukabidhi mradi huo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Aidha alisema kuwa katika wilaya ya Karagwe
jumla ya transfoma 82 zilifungwa na wateja wa njia moja ya umeme
wapatao 3507 waliunganishwa kati ya wateja 5480 na wateja 95 wa njia
tatu ya umeme wameunganishwa ambapo wanatarajia kukamilisha kazi mwezi
Mei mwaka huu.
“Mheshimiwa Waziri, kwa
upande wa wilaya ya Kyerwa tumeshafunga transfoma 63 ambapo lengo la
awali lilikuwa ni kufunga transfoma 53, na kwa wilaya hii wateja 2044 wa
njia moja ya umeme wameunganishiwa umeme kati ya wateja 3228 na wateja
30 wa njia tatu za umeme waliunganishwa na tunatarajia kuendelea
kuunganisha wateja hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu,” alisema Kateti.
Vilevile alisema kuwa katika wilaya ya Misenyi jumla ya transfoma 52 zimefungwa ambapo wateja 1345 wa njia moja waliunganishwa kati
ya wateja 4308 na wateja waliounganishwa kwa njia tatu za umeme ni 17
huku wakitarajia kukamilisha kazi mwezi Juni mwaka huu.
Aliongeza kuwa kwa upande wa wilaya za Muleba na Bukoba Vijijini jumla ya transfoma 118 zimefungwa ambapo
wateja 5649 wa njia moja ya umeme waliunganishwa na huduma hiyo kati ya
wateja 12,703 huku wateja waliounganishwa katika njia tatu za umeme
wakifikia 22 na wanatarajia kukamilisha kazi mwezi Mei mwaka huu.
Kwa upande wa kampuni ya JV State Grid, Meneja Mradi wa kampuni hiyo Mhandisi A. Mwaipaja alisema kuwa kampuni hiyo inasambaza umeme vijijini katika wilaya za Rungwe, Kyela na Ileje mkoani Mbeya ambapo kazi ya kusambaza umeme katika wilaya hizo imekamilika
kwa asilimi 92 hadi kufikia katikati mwa mwezi Machi mwaka huu na
wateja wapya 2,244 wameunganishwa katika vijiji 65 na kufunga transfoma
90 kati ya 133 wanazopaswa kufunga.
Aidha katika wilaya ya Mbarali mkoani humo, JV State imeshakamilisha kazi kwa asilimia 92 hadi
kufikia tarehe 15 Machi, 2016 ambapo wateja wapya 1724 kati ya 4505
katika vijiji 27 wameunganishwa na transfoma 35 kati ya 56 zimefungwa.
Alisema kuwa kampuni hiyo pia inafanya kazi ya kusambaza umeme vijijini katika mkoa wa Kigoma katika wilaya Sita za Kigoma Vijijini, Buhigwe,
Kasulu, Kibondo, Kakonko na Uvinza ambapo kazi imekamilika kwa asilimia
93 hadi kufikia Machi 2016 na jumla ya vijiji 63 na wateja 2,647 kati ya 8773 wameunganishwa na umeme katika wilaya hizo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Wizara ya Nishati na Madini, Dkt.
Mhandisi Juliana Pallangyo aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi
ya usambazaji umeme vijijini kujiepusha na masuala ya rushwa katika
utekelezaji wa miradi hiyo hasa katika zoezi la uunganishaji umeme kwa wateja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni