SHULE YA MSINGI MBAGALA MAJIMATITU YACHIMBIWA VISIMA VYA MAJI.

Msimamizi wa mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala majimatitu kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela akiangalia maendeleo ya kisima kimoja kati ya viwili vinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.
Wataalam kutoka Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) wakiendelea kuchimba kisima chenye urefu wa mita 130 katika shule ya Msingi Mbagala majimatitu, Temeke jijini Dar es salaam. Msimamizi wa mradi wa uchimbaji wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Mbagala majimatitu kutoka DAWASA Muhandisi Abel Chibelela na Mhandisi Elizabeth Kingu, Katibu Tawala Msaidizi Huduma za Maji (kushoto) wakiangalia maendeleo ya moja ya kisima kinavyochimbwa na Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) katika shule hiyo kwa gharama ya shilingi milioni 24.5.

Na. Aron Msigwa –Dar es salaam.

Walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbagala Majimatitu iliyoko Temeke jijini Dar es salaam watanufaika na huduma ya maji safi kufuatia Serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 24.5 kwa lengo la kufanikisha mradi wa uchimbaji wa visima viwili kwa lengo la kuboresha taaluma na mazingira ya shule hiyo.
Akizungumzia uchimbaji wa visima hivyo leo jijini Dar es salaam msimamizi wa mradi huo kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) Muhandisi Abel Chibelela amesema kuwa kuchimbwa kwa visima hivyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali kuitaka DAWASA kutafuta vyanzo vya maji katika shule hiyo ili kuwaondolea adha ya uhaba wa Maji.

Amesema shule hiyo imekuwa na tatizo hilo kufuatia kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 6000 inayozidi uwezo wa miundombinu iliyopo sasa ikiwemo kisima kinachotumiwa na wanafunzi hao kinachozalisha lita 8000 kwa siku wakati mahitaji halisi ya maji ni Lita 40,000 kwa siku.

Amesema Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kupitia Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa ( DDCA) ilipewa jukumu la kuchimba visima viwili  vya shule hiyo kwa thamani ya shilingi milioni 24.5 zikiwa ni gharama za uchimbaji, usafishaji wa visima hivyo na gharama za vipimo vya maabara ili kuangalia ubora wa maji hayo.

" Kazi ya uchimbaji wa visima hivi vyenye urefu wa mita 130 na 140 imeanza rasmi na itachukua siku 14, tunafanya haraka ili tuweze kujua wingi wa maji yaliyopo na ubora wake kama inafaa kwa matumizi ya binadamu"

Pia amesema DAWASA itasimamia ujenzi wa minara mirefu ya matenki na kuongeza matenki makubwa yatakayokidhi mahitaji ya shule hiyo yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 20 kwa kila shule.

Kwa upande wake Mtaalamu kutoka Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA) ambayo ndiyo iliyopewa jukumu la kuchimba visima hivyo na DAWASA Bw. Nungwe Gwaga akizungumzia uchimbaji wa visima hivyo amesema kuwa wao kama wataalam wa kuchimba visima walifanya utafiti katika eneo hilo na kujiridhisha kuwa eneo la shule ya Msingi Mbagala Maji Matitu lina Maji ya kutosha.

" Sisi kama wataalam tulifanya utafiti (Physical Survey) katika eneo hili ili kujua kama kuna maji na miamba inayopita pale pamoja na umbali wake, sisi tumejiridhisha tutachimba mita 130 ambazo tayari zimetupa majibu ya kuwepo kwa Maji "

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bw. Abdul Mgomi akifafanua kuhusu visima hivyo amesema vitawezesha shule yake kuondokana na adha ya uhaba wa huduma ya maji inayowakabili wanafunzi shuleni hapo kufuatia mwitikio wa wazazi kuwaandikisha watoto wao shuleni hapo kwa mwaka 2016.

Amesema kwa sasa shule hiyo inatumia kisima kidogo chenye uwezo wa kuzalisha lita 8000 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji halisi ya lita 32000 kwa wanafunzi 6000 wanaosoma shuleni hapo.

Mwalimu Mgomi ameshukuru jitihada zilizofanywa na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo Mhe. Said Mecki Sadiki kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuchimbia visima hivyo.

Ameeleza kuwa mara baada ya visima hivyo kukamilika  uongozi wa shule utaweka utaratibu wa matumizi ya maji hayo kwa shule na ziada itakayopatikana na maji itauzwa kwa majirani wanaoishi kuzunguka shule hiyo ili mradi uweze kujiendesha wenyewe.

Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuifanyia kazi changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo kwa kujenga mapya 10 ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi 6000 waliopo shuleni hapo pamoja na ujenzi wa shule nyingine 2 zitakazoondoa kabisa tatizo la mrundikano wa wanafunzi.

Naye mmoja wa Wazazi na Mjumbe wa Kamati ya Miradi ya shule hiyo Bi.Happiness Mgulambwa akizungumza katika eneo vinapochimbwa visima hivyo ameishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha wazazi na wanafunzi hao kwa kuamua kuwachimbia visima hivyo huku akiongeza  kuwa upatikanaji wa huduma ya maji shuleni hapo utaongeza ufanisi kwa walimu na wanafunzi.

Amesema wao kama Wazazi kupitia kamati ya miradi ya shule hiyo waliiomba Serikali kuwasaidia kupata maji kwa wanafunzi shule hiyo  ili kuondoa kero ya maji jambo ambalo lilikubaliwa.

" Kweli wanafunzi wa shule hii walikua wanapata shida,uhaba wa maji hapa shuleni uliwalazimu kuja na maji kwenye madumu jambo liliowafanya wakati mwingine kufika wamechoka na hata kuchafuka, tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya tano kwa kutusaidia" Amesema Bi.Mgulambwa. 

MIWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni