PICHA NA IKULU
………………………………………………………………………….
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemwapisha Mkuu wa mkoa mpya wa 
Songwe Luteni Mstaafu Chiku Gallawa, ambaye hakuapishwa pamoja na wakuu 
wa mikoa wenzake Machi 15, 2016.
Uapisho huo umefanyika leo tarehe 
28 Machi, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, na kuhudhuriwa na Makamu wa 
Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim 
Majaliwa.
Luteni Mstaafu Chiku Gallawa 
anakuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kwa Mkoa mpya wa Songwe, ulioanzishwa kwa
 kuugawa mkoa wa Mbeya, Kusini mwa Tanzania.
Wakati huo huo, Rais Dkt. John 
Pombe Magufuli amepokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za serikali kutoka 
kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa 
Assad, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli amepokea taarifa 
hiyo yenye ripoti tano, ikiwa ni utaratibu wa kikatiba unaomtaka Mkaguzi
 na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, kukabidhi kwa Rais taarifa ya 
ukaguzi kabla ya mwisho wa mwezi Machi.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, 
Rais Magufuli ataikabidhi mbele ya bunge katika siku saba za mwanzo za 
kikao kijacho cha Bunge kitakachofanyika Mjini Dodoma.
Rais Magufuli amempongeza Mkaguzi 
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali na timu yake kwa kuandaa taarifa 
hiyo, na ametoa wito kwa chombo hicho kuendelea kufanya kazi kwa uhuru 
na ufanisi, huku akiahidi kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha 
kufanikisha kazi zake.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
28 Machi, 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni