VIUMBE WA BAHARINI AINA YA KASA WAKO HATARINI KUPOTEA


Picha ni mnyama aina ya kasa ambaye anapatikana katika hifadhi ya taifa ya saadani iliopo mkoani Pwani 
Na Mahmoud Ahmad Saadan

Viumbe wa baharini aina ya kasa wametajwa kuwa miongoni mwa viumbe wanaoishi katika mazingira hatarishi huku wakitajwa kuwa wako  hatarini kupotea duniani kutokana na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi.

Hayo yamesemwa na mtaalamu wa kasa katika hifadhi ya taifa ya Saadan iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani,Hamis Abdallah wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea katika hifadhi hiyo kujifunza  vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari jana mtaalamu huyo alisema ya kwamba baadhi ya wavuvi wamekuwa wakihatarisha maisha ya viumbe hao wanaopatikana kandokando ya bahari ya Hindi inayopakana na hifadhi hiyo kutokana na kuwavua hovyo .

Alisema kwamba kasa huzaliana nchi kavu na ndiyo maana amekuwa akijijengea  baadhi ya maadui ambapo aliwataja kuwa ni  papa,kenge ambao wamekuwa wakishambulia mayai  yao na kutishia uhai wa viumbe hao.

“Kasa wanaishi katika mazingira magumu sana kwa kuwa wanaishi katika kina kifupi cha maji na hivyo baadhi ya wavuvi huwavua hovyo lakini pia wana tabia ya kuzaliana nchi kavu na sio majini”alisema mtaalamu huyo

Hatahivyo,alisisistiza ya kwamba  kutokana na tishio la kutoweka kwa viumbe hao hifadhi ya taifa ya Saadan imechukua hatua za haraka kuhakikisha wanachukua eneo kubwa la bahari ili kuwahifadhi viumbe hao sanjari na kutunza mazingira katika eneo hilo.

Alisema kuwa hifadhi yao kupitia kitengo cha ujirani mwema kimekuwa kikishirikiana na jamii inayoizunguka hifadhi hiyo kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kuhusu kutunza mazingira kwa lengo la kutoathiri mabadiliko ya tabia nchi kwa maslahi ya viumbe hao.

“Tushirikiane kutunza mazingira ili kuhifadhi hawa viumbe wa baharini kwa kuwa wana faida kubwa sana kwa taifa  endapo tutaendelea kuwatunza  kasa hawa”alisisitiza Abdallah

Hatahivyo,mtaalamu huyo alifafanua kuhusu sheria za utunzaji wa viumbe wanaoishi baharini na kusema kwamba sheria nambari 9 kifungu cha 12 inayohusu utunzaji wa mazingira ya baharini ina sema iwapo mwananchi atahusika na uharibifu wa viumbe walio hatarini kutoweka atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu hadi mine.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni