Rais Dkt Magufuli awapa siku 15 Wakuu wa Mikoa kuwaondoa watumishi hewa walio katika orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma katika Mikoa yao

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mbele ya Waku wa Mikoa mara baada ya kuwaapisha leo Ikulu jijini Dar.Rais Dkt Magufuli amewapa siku 15 Wakuu wa Mikoa kuwaondoa watumishi hewa walio katika orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma katika Mikoa yao.Picha na Michuzi Jr-MMG

Na Jacquiline Mrisho- Dar es salaam.     

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapa siku 15 Wakuu wa Mikoa kuwaondoa watumishi hewa walio katika orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa umma katika Mikoa yao.

Rais Dkt. Magufuli amesema hayo leo Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa aliowateua Machi 13 mwaka huu ambapo amewaagiza washirikiane na Wakurugenzi wa Halmashauri kuwaondoa watumishi hewa.

“Nimewapa siku 15 kuanzia leo mkashirikiane na Wakurugenzi wa Halmashauri zenu kuwatoa wafanyakazi hewa, nikigundua kuwa bado kuna wafanyakazi hewa, Mkurugenzi husika atafukuzwa kazi na atapelekwa mahakamani”,

Na kusisitiza “Nimeamua kuwachagua nikiamini kwamba mtaniwakilisha vizuri katika Mikoa yenu, nawaomba mkatimize majukumu yenu bila kuogopa” alisema Dkt. Magufuli.

Aidha, Mhe.  Dkt. Magufuli amesikitishwa na utafiti wa watumishi uliofanywa katika Mikoa ya Singida na Dodoma ambapo imegundulika watumishi 202 wanalipwa mishahara hewa.

Wakati wa utafiti huo, zaidi  ya watumishi 26,900 walioko katika Halmashauri 14 za Mikoa hiyo, watumishi 3,320 hawakuwepo kazini kwa sababu mbalimbali.Kwa mantiki hiyo, ukichukua utafiti huo wa Mikoa miwili ni dhahiri Serikali inapoteza mapato mengi kwa kulipa mishahara ya watumishi hewa nchi nzima.

Vivyo hivyo, Mhe. Dkt. Magufuli amewasisitiza Wakuu wote wa Mikoa wakasimamie ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwakuwa waliahidi kutatua kero za wananchi na wahakikishe wanazitatua ili wananchi waishi vizuri kwa amani ndani ya nchi yao.

Naye Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Majiji na Halmashauri zote nchini wajiandae kupokea na kuzipangia matumizi shilingi milioni 50 za kila Kijiji zilizoahidiwa wakati wa kampeni kwa lengo la kuboresha na kuimarisha shughuli za maendeleo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni