WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imetenga sh. bilioni 4.3 ili kujenga vituo vya
kuhifadhi damu (satellite blood banks) kwenye mikoa 12.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni
Manyara, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Njombe. Mingine ni Tanga, Arusha,
Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Ijumaa, Juni 29, 2018) bungeni jijini Dodoma katika hotuba yake
aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge. Bunge
limeahirishwa hadi Septemba 4, mwaka huu.
Amesema lengo la mpango huo ni
kuboresha upatikanaji wa damu hasa kwa akinamama wanaopoteza damu nyingi
wakati wa kujifungua. “Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya
akinamama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika kutekeleza azma hiyo,
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kufanya
ukarabati na ujenzi wa majengo ya upasuaji, maabara, wodi za wazazi,
nyumba za watumishi na wodi za watoto,” amesema.
Amesema kukamilika kwa majengo
hayo, kutaboresha huduma za uzazi kwa akinamama na watoto wachanga.
“Hatua hii itawezesha upatikanaji wa huduma kamili za uzazi na kupunguza
vifo vya mama na watoto. Katika mwaka 2018/2019, eneo litakalopewa
kipaumbele ni kuimarisha upatikanaji vifaa na watumishi katika vituo 208
vinavyoendelea kuboreshwa,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuwasihi watumishi wa afya, waongeze juhudi ya kuhamasisha wananchi
wajitolee damu na pia akawaomba wananchi nao wawe na utamaduni wa
kuchangia damu ili kuwezesha upatikanaji wa damu salama itakayohifadhiwa
kwenye benki hizo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema
Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa nchini kwa kutenga
shilingi bilioni 14 ili kuanzisha huduma ya kuchunguza mwili bila
upasuaji (PET Scan) katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Amesema kuanza kwa huduma hiyo
kutapunguza asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani waliokuwa wanapelekwa
nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hicho na kwamba Serikali itaweza
takribani shilingi bilioni 5 kwa mwaka zilizokuwa zinatumika kwa ajili
ya kulipia wagonjwa waliokuwa wakienda nje ya nchi kwa ajili ya kipimo
hiki.
Amesema Serikali itasogeza huduma
ya tiba ya saratani katika ngazi ya Hospitali za Kanda ikiwa ni pamoja
na Hospitali ya Bugando Mwanza, Hospitali ya Kanda ya Kaskazini KCMC na
Hospitali ya Rufaa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, jijini Mbeya.
“Vilevile, katika mwaka 2018/2019,
Serikali itaimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa katika hospitali
za rufaa za mikoa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya
ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa tiba na madaktari bingwa. Jumla ya
shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha hospitali hizi,”
amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kupitia
Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (Education Performance for Results –
EP4R) itaimarisha miundombinu kwenye shule zenye uhitaji mkubwa.
“Katika mwaka 2018/2019, Serikali
itatumia shilingi bilioni 155.58 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe
25, ununuzi wa vifaa vya maabara, ujenzi wa mabwalo 85, vyumba vya
madarasa 2,000 na motisha kwa Halmashauri kutokana na ufanisi katika
utekelezaji wa vigezo vya EP4R,” amesema.
Amesema kwa sasa, Serikali
inatarajia kuajiri walimu 4,785 wa shule za msingi zenye uhitaji mkubwa
na kwamba tayari imeshatangaza nafasi za ajira kwa walimu 2,000 wa
masomo ya sayansi, hisabati na lugha ambao watapangwa kwenye shule za
sekondari zenye uhitaji mkubwa.
Amesema kuwa Serikali imetangaza
nafasi za ajira kwa mafundi sanifu maabara 160 ambao nao pia watapangwa
kwenye shule zenye uhaba wa wataalamu hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni