*Ni kutokana na juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo cha pamba
ZAO la pamba ni miongoni mwa
mazao makubwa ya biashara yaliyokuwa yakiliingizia Taifa fedha nyingi za
kigeni na kuchangia kukuza uchumi wa wananchi miaka ya 1970.
Kwenye miaka ya 1970 kulisheheni vyama vingi vya ushirika wa zao la Pamba
na viwanda vya kuchambua nyuzi na kukamua mafuta, ambavyo
vilibadili hali halisi ya kipato cha wananchi wa eneo linalolimwa zao
hilo na kulifanya kujulikana kama dhahabu nyeupe.
Kilimo hicho kilianza kudorora
miaka ya hivi karibuni kutokana na kulegalega kwa vyama vya ushirika na
matokeo yake pamba iliuzwa ikiwa chafu bila kuzingatia ubora na
madaraja yaliyopo.
Kutokana na sababu hizo Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, iliamua kufufua
zao hilo ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi ya viwanda vya nguo
na mafuta yatokanayo na mbegu za pamba zinapatikana pamoja na kuinua
uchumi wa wakulima nchini.
Katika kufanikisha suala hilo Serikali
ilianza kwa kuwaagiza viongozi wa mikoa yote inayolima pamba
kuhakikisha wanawahamasisha wakulima kufufua mashamba yao na
ilihakikisha inafuatilia jambo hilo kuanzia hatua za awali za
utayarishaji wa mashamba, ugawaji wa pembejeo hadi utafutaji wa masoko.
Baada ya kutoa agizo hilo ambalo
lilifanyiwa kazi na tayari mafanikio yameanza kuonekana katika msimu wa
mwaka huu, kwa wakulima kuanza kuvuna na kuuza kwa mafanikio.
Akizungumzia kuhusu hali ya zao
hilo mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella, anasema msimu
wa mwaka huu umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na hamasa iliyotolewa
na viongozi wakuu wa Serikali.
Bw. Mongella anasema kutokana na hamasa hiyo, mwaka huu wanatarajia kupata mavuno makubwa kutoka katika kilimo hicho kwa sababu wakulima wengi wamelima na baadhi yao tayari wameshaanza kuvuna.
Anasema Rais Dk. Magufuli na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, walitoa maelekezo mahususi na walifanya
ufuatiliaji wa karibu wa kilimo cha mazao makuu matano ya biashara
nchini, likiwamo na zao la pamba.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya
zao hilo jijini Mwanza hivi karibuni, Bw. Mongella amesema zao la pamba
litasaidia kufufua viwanda vya mafuta ya kula, nguo pamoja na kuongeza
ajira.
Amesema baada ya Rais Dkt.
Magufuli kuhamasisha kilimo cha zao hilo, ambacho kilianza kusuasua
nchini, viongozi waliitikia na kuwahimiza wakulima wachangamkie fursa
hiyo, ambao walikubali.
“Tunashukuru kwa hamasa na
miongozo iliyotolewa na viongozi wetu kwa sababu iliongeza ari kwa
wakulima kulima zao la pamba kwa wingi na mwamko kwa wananchi kulima
mazao mengine, likiwamo la mpunga,” anasema.
Hata hivyo, kiongozi huyo
ameishukuru Serikali kwa kuagiza pamba itakayovunwa iuzwe kupitia minada
itakayosimamiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) katika kila
eneo, jambo ambalo limesaidia kufufuka kwa vyama hivyo.
“Tunashukuru kwa maelekezo na
miongozo iliyokuwa inatolewa na viongozi wetu wakuu. Sasa AMCOS zetu
zimefufuka na huu ni mwanzo tu mapinduzi makubwa katika biashara ya zao
la pamba na yajayo yanafurahisha zaidi,” anasisitiza Bw. Mongella.
Bw. Mongella anatarajia
kuwahamasisha wakulima wote wa mkoa huo pamoja na wafugaji na wavuvi
wajiunge katika AMCOS zilizoko katika maeneo yao, ili kuweza
kuirahisishia Serikali kufanyanao kazi.
Mkuu huyo wa mkoa pia anatumia fursa hiyo kuwapongeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi
wa Halmashauri, Maofisa Kilimo kuanzia ngazi ya wilaya hadi kijiji na
wakulima kwa kuhakikisha kilimo cha zao la pamba kinapata mafanikio.
Bw.Mongella anaamini ushirikiano
wao kupitia vikosi kazi mbalimbali vilivyoundwa kuanzia ngazi ya mkoa
ambapo alikuwa Mwenyekiti watendaji hao walitoa ushirikiano mkubwa
ulichangia mafanikio ya zao hilo.
Hata hivyo, Bw. Mongella
amewashauri wakulima watumie taasisi za kifedha kuhifadhi fedha zao na
wajijengee nidhamu ya matumizi, ambayo itawapa fursa ya kuwekeza kwenye
miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja kujenga nyumba bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya
ya Misungwi, Mkoani Mwanza, Bw. Juma Sweda anasema anaishukuru Serikali
kwa uamuzi wake wa kulifufua zao hilo pamoja na kuwahamasisha wananchi
kulima na kutoa maelekezo ya uuzwaji wake.
“Naishukuru Serikali kwani baada
ya kuwahamasisha ufufuaji wa kilimo cha zao la pamba nasi tuliungana na
wananchi kuhakikisha maelekezo hayo tunayatekeleza kwa vitendo, lengo
letu kubwa ni kuona zao hili linarudi kama zamani.
‘’Mbali na kuwahamasisha
wananchi kulima zao la pamba, pia Watumishi wa Halmashauri nao wamelima
jumla ya ekari 306 za zao la pamba kwenye kijiji cha Ikoma katika Kata ya Kijima. Mashamba yaliongeza hamasa kwa wananchi,’’ anasema Sweda.
Bw. Sweda anasema kabla ya
wakulima kuanza kuanda mashamba ya kilimo cha pamba, Wilaya ya Misungwi
yenye vjjiji 113 ilitoa mafunzo kwa wakulima wawili kila kijiji, ambao
wameshirikiana na vikosi kazi vya vijiji husika na Maafisa Ugani
kusimamia kilimo cha zao hilo.
Anasema kwa sasa wapo katika
hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga kukagua kikamilifu ili
kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote inayopokelewa na vyama
vya ushirika ni ile iliyo katika ubora unaohitajika.
Anasema baada ya Serikali
kuhamasisha kilimo cha zao la pamba kwa mikoa yote inayolima zao hilo,
pia iliagiza kuanzishwa kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) katika
maeneo yote, ambapo AMCOS 50 zilianzishwa wilayani Misungwi.
Bw. Sweda anasema AMCOS
zimesaidia kuimarisha ubora wa pamba, ambapo viongozi wake hukagua pamba
kabla ya kuipokea na iwapo mkulima atabainika kupeleka pamba chafu
hulazimika kuisafisha kwanza kwa kutenga safi pembeni kabla ya kupima na
kulipwa.
Mkuu huyo wa Wilaya anaongeza
kuwa, mbali na kukagua usafi na ubora wa pamba ili kuhakikisha hakuna
pamba chafu inayouzwa, pia wanasimamia zoezi la malipo kwa wakulima na kwamba wanaouza wote wanalipwa hapo hapo na ni marufuku mnunuzi kumkopa mkulima.
Pia, anasema wilaya yao
imeanzisha mikakati mbalimbali ya kutoa motisha kwa Maafisa Kilimo na
wakulima waliofanya vizuri, ambapo hutoa zawadi za pikipiki kwa mkulima
na afisa aliyeongoza katika kata yake.
Anaongeza kuwa Maafisa Kilimo
Wasaidizi wapo nchini Brazil kwa mafunzo ya miezi mitatu, ambapo
wanajifunza namna ya kilimo bora cha zao la pamba. Viongozi hao ambao ni
John Choto, Haika Kimambo na Bahati Mchele walichaguliwa kuhudhuria
mafunzo hayo baada ya kuonyesha jitihada kubwa katika kusimamia zao
hilo.
Mkuu huyo wa wilaya anasema
wilaya ina Maafisa Ugani 90 ambao wamesambazwa kuanzia wilayani hadi
vijiji, lengo likiwa ni kupata nafasi ya kusimamia vizuri na kwa ukaribu
zao la pamba.
Anasema wilaya ina jumla ya kata 27 ambapo Maafisa Kilimo wake wote walipatiwa
pikipiki ili ziwawezeshe kuwafikia wakulima kwa urahisi na kuwahudumia
kwa wakati lakini atakayeshindwa kuwajibika atanyang’wanywa pikipiki.
Sambamba na hayo, Bw. Sweda
aliwashauri wakulima kutumia vizuri fedha wanazozipata baada ya kuuza
mazao yao. Anasema ni vema wakatumia fedha hizo kujiletea maendeleo
katika familia zao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora za kisasa na
kuwaendeleza watoto wao kielimu.
Anasema kwa sasa wapo katika
hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga kukagua kikamilifu ili
kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote inayopokelewa na vyama
vya Ushirika ni ile iliyo katika ubora unaohitajika.
Anasema viongozi wa Vyama vya
Msingi vya AMCOS, hukagua pamba kabla ya kuipokea na iwapo mkulima
atabainika kupeleka pamba chafu hulazimika kuisafisha kwanza kwa kutenga
safi na chafu ndipo hupima na kulipwa.
Mkuu huyo wa wilaya anaongeza
kuwa zao la pamba mbali ya kuwapatia wakulima kipato, pia litaimarisha
hali ya usalama wa chakula kwa sababu fedha watakayoipata baada ya kuuza
pamba itawawezesha kumudu ununuzi wa mahitaji mengine katika familia na
hawatouza vyakula walivyonavyo.
Hata hivyo, Bw. Sweda aliwaomba
wadau wa sekta binafsi wasaidie katika kuliongezea thamani zao hilo kwa
kufanya uwekezaji mkubwa wa viwanda vya nyuzi, nguo na vya kukamua
mafuta ya pamba badala ya kuuza malighafi.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa
Kata ya Mondo, Bw. Sebastian Mbandi anasema mafanikio ya zao hilo kwa
mwaka huu ni makubwa ukilinganisha na miaka iliyopita, hata hivyo
wameshindwa kufika lengo walilojiwekea kutokana na mazao mengi
kushambuliwa na wadudu aina ya thrips.
Bw. Mbandi anasema walitarajia
kuvuna wastani wa tani 1.5 kwa ekari moja lakini kutokana na changamoto
ya ugonjwa iliyosababishwa na mdudu huyo wanatarajia kuvuna wastani wa
kilo 800 kwa ekari hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia wakulima kwa
kuwatafutia dawa itakayowawezesha kupambana na thrips msimu ujao.
Kwa upande wao, wakulima
wakizungumza kwa nyakati tofauti, walitumia fursa hiyo kumshukuru Rais
Dk. Magufuli kwa kuhamasisha wananchi walime zao la pamba, ambapo nao
waliitikia wito huo na sasa wameanza kuona mafanikio.
Miongoni mwa wakulima hao ni
pamoja na Bw. Hoja Ngole mkazi wa Kijiji cha Mondo ambaye amelima ekari
sita na tayari ameshavuna na ameenda kuuza na anatarajia kutumia fedha
atakazozipata kwa kujenga nyumba ya kisasa.
Bw. Ngole na mkewe Bibi Sara
waliahidi kuongeza ukubwa wa shamba katika msimu ujao na wamewaomba
wananchi wengine kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo kwa kuwa ni
mkombozi wa maisha yao. ’’Tumehamasika kuongeza ukubwa wa shamba baada
ya Waziri Mkuu kututembelea na tunataka akija tena akute tumebadilika,
tuwe na nyumba bora,’’ anasema.
Mkulima mwingine,mkazi wa kijiji
cha Mondo Bw. Michael Masalamunda ambaye alikuwa amepeleka pamba yake
katika kituo cha mauzo cha Mwanimo AMCOS amesema anatarajia kutumia
fedha atakazozipata baada ya mauzo hayo kwa kuongeza mtaji wa biashara
ya ng’ombe.
Bw. Masalamunda naye amemshukuru
Rais Dkt. Magufuli kwa kuwahamasisha walime zao la pamba pamoja na na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye naye aliwahamasisha na kufuatilia
maendeleo ya zao hilo.
Mkulima huyo anaishukuru Serikali
kwa kuagiza mauzo ya zao hilo yasimamiwe na vyama vya ushirika kwa
sababu vimewezesha wakulima kuwa na soko la uhakika la pamba yao na
wakiuza tu wanalipwa fedha zao hakuna anayekopwa. “Mimi leo nakuja kuuza
kwa awamu ya pili na fedha zote nimelipwa.”
Naye mkulima mwingine, mkazi wa
kijiji cha Maganzo Bw. Swalala Nteminyanda anaiomba Serikali kuwatafutia
dawa nzuri itakayoweza kuwaangamiza wadudu aina ya thrips ambao
wameonyesha usugu baada ya kupuliziwa dawa mbalimbali bila ya kufa.
Nteminyanda pia anawashauri
wakulima wenzie wafuate maelekezo yanayotolewa na Maafisa ugani
wanaowatembelea katika mashamba yao ili waweze kupata mavuno mengi na
yenye viwango vya ubora vinavyotakiwa. Mkulima huyo amelima ekari saba
na anatarajia kujenga nyumba bora kwa fedha atakazozipata.
Kwa upande waowanunuzi wa zao
hilo wanaishukuru Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa zao
hilo, ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada inayosimamiwa
na AMCOS.
Miongoni mwa wanunuzi hao ni
pamoja Meneja Mkuu wa Kampuni ya NGS Investment LTD, Bw. Emmanuel Dandu
alipokuwa akizungumzia kuhusu kuanza kwa uchambuaji wa pamba kwa msimu
wa mwaka huu.
Bw. Dandu ambaye kampuni yao ya
NGS Investment LTD, licha ya kujishughulisha na biashara nyingine, pia
inamiliki kiwanda cha kuchambua pamba cha Majahida kilichopo wilaya ya
Bariadi mkoani Simiyu, ambayo tayari imeshaanza zoezi ya uchambuaji
pamba.
Anasema pamba inayochambuliwa
katika kiwanda hicho wanainunua kupitia AMCOS walizopangiwa, ambapo
alipongeza mfumo huo kwa sababu unawawezesha kupata malighafi kwa
urahisi na kwa wakati.
“Wanunuzi wote tunanunua pamba
kupitia AMCOS. Serikali imeweka mfumo mzuri unaotuwezesha wote kununua
pamba kadiri ya uwezo wetu. AMCOS zimeagizwa kuuza pamba kwa wanunuzi
wote bila ya ubaguzi, tofauti na miaka ya nyuma” anasema Bw. Dandu.
Anasema awali kabla pamba
haijaanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora lilikuwa halizingatiwi
sana na wakulima kwani pamba yake ikikataliwa na kampuni moja alikuwa
na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine jambo ambalo lilichangia
kuishusha thamani.
Hata hivyo, wanunuzi hao
wanaiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na maghala makubwa na ya
kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni kuhakikisha pamba
inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya isipoteze ubora.
Mbali na maombi hayo, pia
wameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa Ushirika ili waweze
kutekeleza majuku yao kikamilifu na pia isaidie kutoa elimu kwa
wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima wengi waweze
kujiunga.
Akizungumzia kuhusu uwezo wa
kiwanda hicho, anasema kina uwezo wa kuchambua tani 40,000 za pamba kwa
mwaka, lakini wanalazimika kuchambua wastani wa tani tano hadi 12
kutokana na changamoto ya upatikanaji wa pamba ya kutosha pamoja na
changamoto ya umeme wa uhakika.
Pia anaiomba Serikali iwasaidie
wakulima kwa kuwapatia pembejeo kwa wakati pamoja na kuwapa elimu ya
mara kwa mara juu ya kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la
pamba, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa wakati ili waweze kujiongezea
tija.
Anasema kwa sasa kiwanda hicho
kina jumla ya wafanyakazi 300, ambao kati yao 62 ni waajiriwa wa kudumu
na waliosalia ni vibarua.
Bw. Dandu anasema marobota
yanayotengenezwa kiwandani hapo yanakuwa na uzito wa kilo 200 hadi 220,
huku wateja wao wakubwa ni Cotton Distributors Inc (CDI) ya nchini
Uswisi, Saurashtra Cotton and Agro Product PVT LTD ya nchini India.
Wengine ni Awatac Impex PTE LTD
ya nchini Singapore pamoja na viwanda vya nguo vya ndani ya nchi
kikiwemo cha Mwatex cha jijini Mwanza. Alisema matarajio ya kampuni hiyo
ni kuanzisha kiwanda cha kutengeza nyuzi ili kuongezea thamani ya pamba
kabla ya kuiuza.
Aidha, Meneja huyo anasema mbegu
zinazopatikana baada ya pamba hiyo kuchambuliwa zinapelekwa moja kwa
moja katika kiwanda cha kukamua mafuta ya kula na mashudu huuzwa kama
chakula cha mifugo na mabaki yanayopatikana baada ya mafuta kuchujwa,
anasema yanatumika kwa kutengeneza sabuni za kufulia, ambazo wanaziuza
kwa wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni