Na Mahmoud Ahmad,Dodoma.
ZAIDI ya asilimia 90 ya watanzania wanaokana kuishi kwa kutegemea nishati ya mkaa na kuni kama chanzo kikuu cha kupikia .
Hata hivyo nishati hiyo inategemewa zaidi na wananchi wenye kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini suala ambalo linapelekea ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa kuwa mkubwa na kusababisha umaskini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake Afisa misitu wa halmashauri ya jiji la Dodoma Alexandra Kabado ametoa agizo kwa wananchi mkoani hapa kutojihusisha na uchomaji misitu na kwamba sheria itafuata mkondo wake kwa yeyote ambaye atabainika kujihusisha na uharibifu wa misitu.
,afisa misitu huyo alisema kumekuwa na tabia sugu kwa baadhi ya watu kujihusisha na uchomaji misitu kwa shughuli za kibinadamu hali ambayo haikubaliki.
“Niwaambie wazi kuwa sheria itafuata mkondo wake kwa yeyote atakaye husika na uharibifu wa misitu kwa kuwa elimu imetolewa vya kutosha kama watu kusikia wamesikia kinachofanyika ni uzembe tu”alisisitiza.
Hata hivyo alisema,licha ya kuwepo faini ya shilingi elfu Hamsini kwa waharibifu wa misitu watu bado wanaendelea kujihusisha na uchomaji mkaa katika misitu na kukata miti kwa matumizi mengine.
Akieleza zaidi Kabado aliongeza kuwa ukataji wa miti hovyo katika misitu kunaweza kuleta majanga mbalimbali ikiwemo ukame na kusababisha uhaba wa mvua hali inayoleta uhaba wa chakula kwa baadhi ya maeneo.
Aidha alisema asilimia 75% mpaka 80% ya watanzania wanategemea kilimo na ufugaji na sehemu kubwa ya kilimo inategemea mvua hivyo kunapotokea uhaba wa mvua shughuli za kilimo zinakuwa duni.
“ Uhaba wa mvua unasababisha mavuno kuwa haba na kusababisha njaa pamoja na umasikini hivyo kama maafisa misitu tunasisitiza watu kutumia nishati mbadala ili kuondokana na dhana ya ukataji misitu hovyo”alisema.
Hatahivyo, Afisa misitu huyo amewataka wananchi hususani wakazi wa mkoa wa Dodoma kutumia nishati mbadala kama vile gesi na ikishindikana kabisa watumie majiko ambayo yanatumia mkaa kidogo pamoja na kuni ili kunusuru misitu kwa maendeleo endelevu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni