*Ataka apewe majina ya watakaokiuka agizo hilo
*Akataza magari ya Serikali kulala nyumbani kwa mtu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaagiza watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma
wanaoishi nje ya eneo lao la kazi wawe wamehamia ifikapo Julai 30, mwaka
huu.
“Tunataka watumishi wa umma
wawajibike na waishi katika vituo vyao vya kazi. Nawataka watumishi wote
wa wilaya hii wanaoishi Dodoma wawe wamehamia hapa ifikapo Julai 30
mwaka huu na wasiohamia nipewe majina yao,” amesisitiza.
Pia ameagiza magari yote ya
Serikali baada ya kuisha muda ya kazi yawe yameegeshwa kwenye ofisi za
halmashauri na ni marufuku kwa magari hayo kulala nyumbani kwa mtu.
Ametoa maagizo hayo leo
(Jumatano, Juni 27, 2018) wakati akizinduavituo 51 vya kufuatilia
taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya taarifa
za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya
dharura wilayani Bahi, Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali
inataka watumishi wote wa umma nchini waishi kwenye vituo vyao vya kazi
ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ukaribu katika maeneo husika.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bahi, Bibi. Rachel
Chuwa aanzishe mradi wa upimaji wa viwanja na viuzwe kwa watumishi na
wananchi kwa gharama nafuu.
Waziri Mkuu amesema ni vema
wilaya hiyo ikachangamkia fursa ya Serikali kuhamia Dodoma kwa kuboresha
miundombinu mbalimbali ikiwemo nyumba za kuishi, hoteli na sehemu za
burudani ili watumishi waliohamia Dodoma wapate sehemu za kujipumzisha
pindi wamalizapo majukumu yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni