Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
zinaendelea kujadiana kuhusu namna bora ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa
kero ya ulipaji kodi ya mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.
Hayo
yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge
wa Wingwi, Mhe. Juma Kombo Hamad (CUF)M aliyetaka kujua kama Serikali
ipo tayari kuunda Kamati Ndogo ya Bunge kwa ajili ya kushughulikia mfumo
wa ulipaji kodi za mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.
Katika
sawli hilo Mhe. Hamad alieleza kuwa mfumo wa ulipaji kodi za
kusafirisha bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara umekuwa
ukilalamikiwa kwa muda mrefu kwamba unawakwaza na kuvunja harakati za
biashara Zanzibar na hivyo kusababisha uchumi wa Zanzibar kushuka.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji, alisema kuwa Serikali hizo mbili zinaendelea
kujadiliana ili kuona kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu na
kuongeza kuwa Serikali hizo hazijashindwa kutatua changamoto hiyo na
hakuna sababu ya kuunda kamati ya kushughulikia suala hilo.
Alisema
chimbuko la malamiko hayo linatokana na kuwepo kwa mifumo tofauti ya
kutathmini bidhaa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara hali inayosababishwa
na viwango tofauti vya ushuru wa forodha vinavyopaswa kulipwa kwa
bidhaa ya aina moja kutoka nje ya nchi na kusafirishwa kwenda sehemu ya
pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa Mfumo wa uthaminishaji bidhaa zote zinazoingia
Tanzania Bara unafanyika kwa kutumia mifumo ya TANCIS na Import Export
Commodity Database (IECD) inayoratibiwa na kituo cha Huduma za Forodha
kilichopo Dar es Salaam, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
haitumii mifumo hiyo na kusababisha kuwepo na tofauti ya kodi kati ya
Bara na Zanzibar.
“Kutokana
na utofauti wa mifumo inayotumika, bidhaa zote za nje zinazoingia
Tanzania Bara kupitia Zanzibar hufanyiwa uhakiki licha ya kuwa
zimethaminiwa Zazibar, iwapo uthamini wa Tanzania Bara utakuwa sawa na
ule uliofanywa Zanzibar hakuna kodi itakayotozwa Tanzania Bara na ikiwa
kodi iliyolipwa Zanzibar ni ndogo, Mamlaka ya Mapato hukusanya tofauti
ya kodi iliyozidi”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisisitiza
kuwa utaratibu wa kukusanya tofauti ya kodi kati ya Zanzibar na Bara
kwa kutumia mifumo ya TANCIS na IECD haina lengo la kuua biashara
Zanzibar, bali hatua hiyo inalenga kuleta usawa wa gharama za kufanya
biashara na ushindani hapa nchini.
Aidha
Naibu Waziri huyo alisema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Ibara ya 63 (2) Bunge ni muhimili unaojitegemea na
hivyo Serikali haina mamlaka ya kuunda Kamati ndogo ya Bunge kwa ajili
ya jambo hilo au jambo lolote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni