DOKTA KIJAJI AFANYA ZIARA MITAANI JIJINI DODOMA KUKAGUA MASHINE ZA EFD NA KUBAINI BAADHI YA WAFANYABIASHARA HAWAZITUMII


9132
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amefanya ziara katika mitaa ya Jiji la Dodoma, kukagua upatikanaji wa huduma ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs), ambazo mfumo wake ulipata hitilafu hivi karibuni ambao hivi sasa umetengemaa na kubaini kuwa licha ya hitilafu iliyotokea, wafanyabiashara wengi katika jiji hilo hawazitumii ipasavyo mashine hizo.
Dkt. Kijaji aliyeambatana na Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw. Elijah Mwandumbya, amewaonya wafanyabiashara kote nchini wanaokiuka masharti ya matumizi ya mashine hizo kuacha vitendo hivyo mara moja na kuiagiza TRA kuwachukulia hatua kali za kisheria wafanyabiashara wasiotoa risiti za kieletroniki baada ya kuuza bidhaa zao.
“Wanauza mauzo yao vizuri lakini hawatoi risiti, tumeongea nao kuwaeleza kuwa wanapaswa kutoa risiti wanapouza bidhaa na huduma zao kwani suala hilo ni la kisheria, ni lazima litekelezwe” alionya Dkt. Kijaji
Alisema kuwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuelewa kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana bila kukusanywa kwa kodi sahihi.
“Tunadai maji, huduma za afya, barabara nzuri, bila kukusanya na kulipa kodi haiwezekani tukayafikia haya malengo ya kulifikisha Taifa katika uchumi wa kati” aliongeza Dkt. Kijaji
Kwa Upande wake, Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA Bw. Elijah Mwandumbya, amesema kuwa wafanyabiashara wasiotumia ipasavyo mashine za EFD watakabiliwa na adhabu kali inayofikia shilingi milioni nne na nusu kwa kutokutoa risiti huku mteja akikabiliwa na faini ya shilingi elfu thelathini kwa kutokudai risiti inayolingana na thamani ya bidhaa alizonunua.
“Ni kosa kuwa na mauzo ambayo hujayatolea risiti na ndio maana tunawapa fursa hii waweze kuweka kumbukumbu zao sawasawa kwa sababu tumegundua baadhi yao wanayo mauzo lakini hawajatoa risiti” aliongeza Bw. Mwandumbya.
Bw. Mwandumbya ameeleza kuwa ukaguzi wao umeonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya mashine za kieletroniki zinafanyakazi ipasavyo baada ya kutengemaa kwa mfumo wa kuchakata taarifa za mauzo kwa njia ya kieletroniki uliopata hitilafu tangu Mei 11 mwaka huu na kusababisha baadhi ya mashine hizo za EFD kutofanyakazi.
Aliwataka wafanyabiashara kuingiza mauzo yote waliyoyafanya katika kipindi chote ambacho kulikuwa na hitilafu ya kimfumo katika mashine ya EFD na kutoa risiti moja ya mauzo hayo ili yaweze kutambulika katika mfumo wa mapato wa TRA kwa ukadiriaji sahihi wa kodi za biashara zao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni