WAGONJWA 15 KATI YA 20 WAFANYIWA UPASUAJI WA MOYO KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU YA MOYO INAYOENDELEA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE


Picha no. 1

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bashir Nyangasa akiwaonyesha waandishi wa habari jinsi  upasuaji wa kurekebisa mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili (Aortic Aneurysm Repair) unavyofanyika katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya Mjini Mumbai nchini India. Hadi sasa jumla ya  wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.

Picha na JKCI
……………..
Jumla ya wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku sita  inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya mjini Mumbai nchini India .

Wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji wa   kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass Grafting), kubadili milango miwili hadi mitatu ya  moyo (Valve Replacement) na upasuaji wa kurekebisha mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili (Aortic Aneurysm Repair/Bental Procedure).

Aidha katika kambi hii kwa mara ya kwanza umefanyika  upasuaji wa kuvuna mshipa wa damu ndani ya kifua upande wa kulia na kushoto na kuunganisha kwenye misuli ya moyo ili kuuongezea moyo damu.

Wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na saba kati yao wameruhusiwa kutoka  katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Katika kambi hiyo iliyoanza tarehe 18 na inatarajiwa kumalizika  tarehe 23 mwezi huu  inaenda sambamba na utoaji wa elimu pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa madaktari wetu pamoja na wauguzi. Jumla ya wagonjwa 20 ambao ni watu wazima  wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni