Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyevaa Suti na Miwani akiwa katika
tafrija ya pamoja na ujumbe wa viongozi wa Benki ya Dunia na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) ukiwa Zanzibar kukagua miradi ya
maendeleo ya jamii inayosimamiwa na TASAF hapo Hoteli ya Sea Cliff Kama.
Baadhi ya Wakurugenzi na
Mameneja wa Vitengo vya Benki ya Dunia wakishiriki wa tafrija hiyo
iliyojumuisha pia baadhi ya viongozi wa Mfuko wa (TASAF) Zanzibar.
Balozi Seif akiuomba Uongozi wa
Benki ya Dunia kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi ya
Maendeleo mara baada ya tafrija ya pamoja na Uongozi huo.
Mkurugenzi na Mkuu wa Mtandao wa
Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia Bw. Michal Rutkowski
akitoa salamu kwenye tafrija hiyo na kupongeza miradi ya TASAF jinsi
inavyotekelezwa vyema Visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii Tanzania Nd. Ladislaus Mwamanga akisisitiza nia ya
mfuko huo ya kuendelea kuzisaidia Kaya Maskini Nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed akishukuru
ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia unaosaidia
kuzikomboa Kaya Maskini Nchini.
Balozi Seif kati kati waliokaa
vitini akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Benki ya Dunia, TASAF
pamoja na TASAF Zanzibar mara baada ya kumaliza tafrija hapo Sea Cliff
Hoteli Kama.Kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa
masuala ya Kijamii Bw. Michal Rutkowski, Waziri Mohamed Aboud, Mshauri
Mkuu wa Benki ya Dunia Bibi Margaret Grosh, kushoto ya Balozi Seif ni
Mkurugenzi wa TASAF Ladislaus Mwamanga, Mkurugenzi wa Masuala ya Kijamii
wa Benki ya Dunia Bw. Steen Jorgensen na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais Mhe. Mihayo Juma N’hunga.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdallah Hassan Mitawi akitoa neno la
shukrani kwa Ujumbe wa Wakurugenzi wa Benki ya Dunia baada ya kukamilika
kwa Tafrija waliyoandaliwa hapo Sea Cliff Kama.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia pamoja na wale
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Muungano wakiwa katika
Tafrija ya pamoja ya kupongezana baada ya kumalizika kwa ziara ya Ujumbe
huo wa Benki ya Dunia.
Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wa World Bank………………………
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiomba Benki ya Dunia (WB) kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika harakati zake inazozichukuwa za kuimarisha ustawi wa wananchi wake hasa wale wa kipato cha chini.
Alisema ustawi wa jamii unapaswa kujengewa mazingira bora na ya kudumu yatakayowezesha kupatikana kwa nguvu za pamoja ambazo hupatikana kwa mjumuisho wa Serikali Kuu kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo waliopo Nchini na wa nje.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ombi hilo katika tafrija maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya ujumbe wa Benki ya Dunia uliofanya ziara ya siku tatu Zanzibar kukagua miradi ya maendeleo iliyochini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) inayopata msukumo kutoka Benki ya Dunia iliyofanyika Hoteli ya Sea Cliff iliyopo Kama nje kidogo ya kaskazini ya Mji wa Zanzibar.
Alisema Benki ya Dunia imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kuunga mkono miradi ya kiuchumi na kijamii inayoanzishwa na Serikali na taasisi za Kiraia jambo ambalo aliuhakikishia ujumbe wa taasisi hiyo ya kimataifa ya Fedha kwamba Miradi inayoifadhili itaisimamia kwa lengo la kufanikiwa vyema.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema, miradi yote iliyoanzishwa na wananchi katika maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba kupitia TASAF na kupata msukumo wa Benki ya Dunia umeleta ukombozi kwa Wananchi waliowengi nchini.
Alisema hatua hiyo ni mafanikio makubwa yaliyoleta ustawi wa maisha yao katika kujipatia kipato cha uhakika imekua chachu kwa baadhi ya vijiji nchini ambapo vijiji vingine vimeshawishika na kuuomba uongozi wa TASAF kuwaingiza katika Programu za miradi hiyo muhimu.
Balozi Seif alisema awamu ya kwanza ya programu hiyo ya miaka mitano ya miradi ya TASAF iliyoanza Mwaka 2000 ikiwa na jumla ya miradi ya uchumi na maendeleo 75 Unguja na Pemba imegharimu jumla ya T.Sh. bilioni tatu na kushirikisha wananchi laki 135,798.
Alisema mafanikio ya miradi hiyo imewezesha kuongezeka kwa miradi ya TASAF katika awamu ya pili iliyoanza Mwaka 2005 hadi 2013 kwa gharama za T.Sh. bilioni 12.9 kwa kushirikisha wananchi laki 471,346 Unguja na Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza ujumbe huo wa Benki ya Dunia kwamba, Serikali Kuu katika kuwawezesha kiuchumi wananchi wake hasa wale waliopo katika mazingira magumu umelenga kuwapunguzia ukali wa maisha.
Alisema hatua hiyo imepelekea awamu ya Tatu ya TASAF kuwanufaisha wananchi hao, wanaoishi katika mazingira magumu ambapo Shehia 233 zimeingizwa katika mpango huo kwa kuzihusisha Kaya maskini 45,881, kati ya hizo Kaya 33,532 hupokea fedha kila baada ya kipindi cha miezi mitatu.
Balozi Seif alifafanua kwamba mpango huo tayari umeshaanza kuleta mafanikio makubwa kwa familia za Kaya maskini kwa vile hali ya upatianaji wa chakula inaanza kuridhisha sambamba na watoto wa Kaya hizo kuendelea na masomo yao ya msingi na sekondari bila ya vikwazo hasa katika upatikanajiwa sare za skuli.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Nd. Ladislaus Mwamanga alisema kazi kubwa inayofanywa na wananchi wa Zanzibar kwenye miradi ya maendeleo kupitia programu hii zinazosimamiwa na TASAF imeleta mafanikio makubwa.
Nd. Mwamanga alisema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mfuko huo itaendelea kuongeza nguvu mara dufu katika kuona kundi kubwa la wananchi walio na kipato duni hasa vijijini wanaongezewa nguvu za uwezeshaji ili kuondokana na mazingira magumu.
Akitoa salamu kwa niaba ya ujumbe wa viongozi hao wa Benki ya Dunia Mkurugenzi na Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia Bw. Michal Rutkowski alisema Taasisi hiyo ya Kimataifa ya Fedha haina sababu ya kusua sua katika kuongeza nguvu kwenye miradi ya TASAF inayoendelea vizuri katika utekelezaji wake.
Bwana Michal alisema Uongozi wa juu wa Benki ya Dunia umefurahishwa na jitihada kubwa zinazochukuliwa na wananchi walio wengi visiwani Zanzibar katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii inayosimamiwa na mfuko wa TASAF.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika tafrija hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed alisema ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia umesaidia kupunguza umaskini kwa baadhi ya Kaya Nchini Tanzania.
Waziri Aboud alisema ushirikiano huo unaendelea kuwa kigezo tosha kinachotoa majibu ya uwepo wa utulivu wa kimaisha kwa baadhi ya familia za Kaya hizo jambo ambalo limeleta faraja zaidi kwa watoto wao katika kushiriki vyema masomo yao.
Hii ni mara ya pili kwa Mkurugenzi ambae pia ni Mkuu wa Mtandao wa Masuala ya Kijamii na Ajira wa Benki ya Dunia Bw. Michal Rutkowski na Maafisa wake kutembelea miradi ya maendeleo ya kijamii inayosimamiwa na Mfuko wa TASAF Nchini Tanzania.
Ziara ya kwanza ya Bw. Michal na ujumbe wake hapa Tanzania ilifanyika tarehe 8 Novemba mwaka 2017, ambapo pamoja na mambo mengine ujumbe huo uliridhika na mafanikio makubwa ya wananchi katika kuendelesha miradi yao ya maendeleo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni