Naibu Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndugulile akiongea na vyombo vya habari leo jijini Arusha kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2018.
Mkurugenzi wa Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akimkaribisha Naibu Waziri Dk. Faustine Ndugulile kuongea vyombo vya habari leo jijini Arusha kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2018.
……………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali kupitia Jeshi la Polisi imefanikiwa kuwa na madawati ya jinsia zaidi ya 500 nchi nzima yanayosaidia kutatua na kutoa ufumbuzi wa haraka kwa mashauri ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Arusha na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika pamoja na ufunguzi wa mafunzo ya Waandishi wa Habari za watoto yaliyoandaliwa na shirika la Plan International.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali inalinda haki na maendeleo ya mtoto ndio maana imeanzisha Idara, Sera na Sheria zinazomlinda mtoto hivyo haki za msingi za mtoto zikiwemo za kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kutobaguliwa pamoja na kushirikishwa lazima ziheshimiwe na kulindwa.
”Tangu Januari hadi Disemba, 2017 jumla ya matukio 41,000 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa na kati ya hayo 13,457 ni ukatili dhidi ya watoto, matukio hayo ya ukatili wa kijinsia ni mengi kuliko matukio ya ujambazi kwa nchi nzima hivyo Madawati ya jinsia yana umuhimu mkubwa katika kusimamia mashauri haya na ndio sababu kubwa ya Serikali kuyaongeza” alisema Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa mbali na madawati ya kijinsia, Serikali imeboresha huduma za afya kwa kuhakikisha wakina mama wanajifungulia katika vituo vya afya na watoto wanaozaliwa wanapatiwa chanjo stahiki ili kuokoa vifo vya watoto hao.
Vile vile Serikali imekuja na mpango mkakati wa kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto utakaoisha 2022 ambao kati ya mipango yake imeanzisha kituo kimoja (One Stop Centre) ambacho kitajumuisha huduma za kipolisi, ushauri nasaha pamoja na huduma za kimatibabu kwa watoto na wanawake waliofanyiwa ukatili huo.
Aidha, Serikali imeanzisha huduma ya kupiga simu kwa namba 116 kwa ajili ya kutoa taarifa ya ukatili wa kijinsia ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi kutomaliza kesi za ukatili wa watoto kifamilia badala yake kuzifikisha katika vyombo vya kisheria ili hatua za kisheria zichukuliwe kukomesha tabia hizo.
Wakati akifungua mafunzo hayo, Dkt. Ndugulile amewakumbusha wanahabari kuacha kusambaza picha au kumtambulisha mtoto ambaye amedhalilishwa kijinsia kwa sababu ni kosa kisheria.
Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika kilele chake ni Juni 16, 2018 lakini kwa mwaka huu yanafanyika June 13 kwa sababu tarehe husika itaingiliana na ratiba zingine, kitaifa yanafanyikia jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni