SERIKALI YAWATAKA WAAJIRI NCHINI KUANDAA MAPEMA TAARIFA SAHIHI ZA WATUMISHI ILI WANAPOSTAAFU WAPATE MAFAO KWA WAKATI


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mafao ya wastaafu katika ukumbi wa Habari wa Bunge jijini Dodoma leo.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) katika ukumbi wa Habari wa Bunge jijini Dodoma leo.



Serikali imewataka waajiri nchini kuhakikisha kwamba, nyaraka na taarifa zinazomhusu mtumishi wa umma zinaandaliwa, kutunzwa vizuri, kuhuishwa na kuhakikiwa mara kwa mara kwa lengo la kumuwezesha mtumishi anapostaafu kupata mafao yake kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Habari wa Bunge jijini Dodoma.

Mhe. Mkuchika amewaelekeza Wakuu wa Idara za Usimamizi wa Rasilimaliwatu, kuhakikisha wanakuwa na Tange zilizo hai wakati wote na kuweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia masuala ya Watumishi wanaokaribia kustaafu kwa mujibu wa matakwa ya Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, ni jukumu la mwajiri kumsaidia mstaafu kukamilisha taratibu za kufuatilia mafao yake badala ya kumuacha akihangaika bila usaidizi wowote na kuongeza kuwa wengi wa wastaafu hao wanatoka maeneo ya mbali.
Mhe. Mkuchika ameainisha kuwa, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wastaafu kucheleweshewa mafao yao kutokana na baadhi ya wadau wa mchakato huo kutotekeleza wajibu wao ipasavyo na matokeo yake kusababisha usumbufu kwa watumishi wastaafu kutolipwa mafao yao kwa wakati.

Mhe. Mkuchika amesema, Serikali imeona changamoto hiyo na ndio maana hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameidhinisha mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inaunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuwa na mifuko miwili ambayo itarahisisha usimamizi wa mafao ya watumishi wastaafu wa sekta ya umma na binafsi.

Mhe. Mkuchika amesisitiza kuwa, Serikali imedhamiria kutatua changamoto ya kucheleweshwa kwa mafao ya wastaafu, hivyo, haitakuwa tayari kumvumilia mdau yeyote atakayezembea kuwahudumia wastaafu.

Aidha, Mhe. Mkuchika amewataka watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu kutoa taarifa kwa waajiri wao kuhusu nia yao ya kustaafu angalau miezi 6 kabla ya tarehe ya kustaafu ili kumwezesha mwajiri kuandaa utaratibu wa mafao yao.


Mhe. Mkuchika amewasisitiza watumishi wa umma nchini, kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake kikamilifu ili kuondoa kero kwa watumishi wastaafu pindi wanapofuatilia mafao yao.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni