Msukuma Kuburuzwa Mahakamani



Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ anaweza kufikishwa mahakamani kwa kushindwa kurejesha mkopo wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), tangu mwaka 2007.
Kwa kushindwa kurejesha mkopo huo ambao pamoja na riba umefikia Sh784.5 milioni, benki hiyo imemwandikia barua mdhamini wake, Martin Nandi ikimjulisha hatua itakazochukua dhidi ya nyumba yake ndani ya siku 60.
Nyumba hiyo iliyoko kiwanja namba 275, kitalu H, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ndiyo ilitumika kama dhamana ya mkopo huo NBC.
Katika barua ya Machi 21, benki inamtaarifu mdhamini huyo kuwa ndani ya siku 60 inaweza kuipiga mnada mali hiyo ya dhamana, kuiweka chini ya mfilisi, kuipangisha au kuiweka chini ya umiliki wake benki.
Nandi baada ya kupata barua ya NBC, kupitia kampuni ya uwakili ya Raymaxx Attorneys, amemwandikia Musukuma taarifa ya kusudio la kumfikisha mahakamani.
Katika taarifa iliyosainiwa Aprili 20 na wakili Rabin Mafuru, Nandi alimpa Musukuma siku saba za kulipa deni la NBC na pia amrejeshee hati ya nyumba yake.
Musukuma alipoulizwa  kuhusu barua hiyo hakuwa tayari kuizungumzia akisema tayari kuna kesi mahakamani.
“Kuna kesi mahakamani sasa mimi nitazungumza kitu gani. Hilo suala liko Mahakama Kuu na yeye amefungua kesi sasa mimi nitazungumza kitu gani?” alisema Musukuma.
Alisema, “Kama unataka kuandika alivyotaka yeye mimi sijui lakini mimi siwezi kuzungumza kitu chochote kilichoko mahakamani.”
Kwa mujibu wa Nandi na nyaraka kuhusu mkopo huo , Juni 16, 2007 aliingia mkataba wa makubaliano ya ubia katika biashara ya simu na Musukuma.
Anadai waliingia mkataba baada ya Musukuma kumuomba ampatie hati ya nyumba yake kwa ajili ya kuchukua mkopo NBC ili kuendeleza biashara hiyo.
Kwa mujibu wa barua ya Juni 16, 2007 Musukuma alikiri kupokea kutoka kwa Nandi hati ya nyumba kwa ajili ya mkopo kutoka NBC.
Nandi alisema hati hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya mkopo wa Sh65 milioni lakini iliendelea kutumika kwa mikopo mingine.
Anadai masharti ya dhamana yalikuwa Nandi kuwa mkurugenzi katika kampuni ya Musukuma ya simu za mkononi baada ya mkopo kutolewa na benki.
Masharti mengine yalikuwa wote wawili kuwa watia saini katika akaunti maalumu ya mkopo huo, kufanya tathmini ya faida halisi ya mauzo kila mwisho wa mwezi na kugawana faida kwa kiwango cha asilimia hamsini kwa hamsini.
Mengine ni kuhuisha mkataba wa mkopo huo kila ifikapo Desemba 31, iwapo wote wataridhika na ustawi wa biashara na faida kwa kuzingatia masharti waliyowekeana. Nandi anadai baada ya mkopo kupatikana, Musukuma alimkwepa na kukataa kusainiana mkataba wa kisheria kulingana na makubaliano yao.
Chanzo: Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni