Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameokoa
takriban shilingi bilioni 16 za upimaji wa mpaka kati ya Tanzania na
Kenya mara baada kuanza kazi ya upimaji wa mpaka huo wenye urefu wa
jumla za kilomita 760 za nchi kavu.
Akiongea
jana wakati akikagua kazi ya uwekaji wa alama mpya za mipaka iliyowekwa
katika wilaya ya Tarime mkoani Mara Waziri Lukuvi amesema hapo awali
wataalamu wa upimaji wa mpaka huo waliandaa makisio ya bajeti ya kiasi
cha shilingi bilioni 22 ambapo mara baada kuanza kwa zoezi hilo
amegundua kwamba zoezi hilo litagharimu shilingi bilioni 6 hadi
kumalizika kwake.
“tulipanga
kutumia shilingi bilioni 22 zilizokuwa katika makaratasi ambapo katika
uhalisia tangu kuanza kwa kazi hii ya uwekaji alama mpya za mipaka
tumegundua ya kwamba serikali inaweza kutumia shilingi bilioni 6 tu
ambazo zitamaliza kazi hii ya uwekaji wa alama za mipaka kati ya
Tanzania na Kenya” amesema Lukuvi.
Aidha,
Waziri Lukuvi amewapongeza watendaji wa Idara ya Upimaji na Ramani
iliyopo Wizara ya Ardhi inayoongozwa na Dkt. James Mtamakaya kwa kazi
nzuri ya kizalendo iliyopelekea kuokoa fedha za serikali kwa
kushirikiana na wataalam wa Mkoa na Halmashauri.
Ameongeza
kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya mipango ya fedha katika makaratasi
na uhalisia wa kazi katika eneo husika, mara baada ya kuanza kazi katika
maeneo husika ya uwekaji wa alama mpya za mpaka kati ya Tanzania na
Kenya imebainika kiuhalisia kazi hiyo haitatumia kiasi kikubwa cha fedha
kama ilivyokisiwa hapo awali.
Waziri
Lukuvi amefanya ziara hiyo ya ukaguzi wa mpaka wa Tanzania na Kenya
ambapo juzi amekagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la mpaka
lililopo wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na jana amekagua mpaka wa
Tanzania na Kenya katika eneo la mpaka lililopo wilaya ya Tarime Mkoani
Mara.
Tanzania
imeamua kuimarisha mipaka yake yote ya kimataifa kufuatia changamoto
nyingi zinazojitokeza tangu kuasisiwa na wakoloni katika miaka ya 1886
hadi 1890 ambapo alama za mipaka hiyo ziliwekwa kwa umbali wa takribani
kilomita 2 hadi 10 kutoka alama moja na nyingine hivyo kusababisha
wananchi kutoielewa mipaka ya nchi zao kwa urahisi na hatimaye kuleta
migongano.
Kazi
hii ya kuimarisha mipaka ni Azimio la Umoja wa Afrika kwamba nchi zote
ziwe zimekamilisha zoezi la uimarishaji wa mipaka ya kimataifa ifikapo
mwaka 2022. Na baada ya zoezi hili la uwekaji wa alama mpya za mipaka
yatatayarishwa Makubaliano (Protocol) ambayo yatasainiwa rasmi na
viongozi wakuu wa nchi hizi mbili.
Kwa
sasa serikali ya Tanzania na Kenya zimeamua kuweka alama mpya za mpaka
kwa umbali wa mita 100 kutoka alama moja na nyingine ili iwe rahisi kwa
wananchi kuziona alama hizi, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi
wanaoshi katika mpaka huo. Kazi hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na
Marais wote wawili wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Kenya,
Mhe. Uhuru Kenyata.
Uwekaji
wa alama hizo unataraji kutatua changamoto zinazokabili mipaka ya nchi
yetu ambazo, ni baadhi ya wananchi kufanya maendelezo ya ujenzi wa
nyumba na kulima mashamba katika maeneo ya mipaka, hali inayopelekea
migongano.
Aidha,
changamoto hizi zinasababisha ugumu wa utengenezaji wa barabara ya
kuhudumia mipaka ya nchi hizi mbili kwa kuwa watu wamevamia mipaka na
kufanya maendelezo, pia inaleta ugumu wa uwekaji wa miundombinu ya maji
na inaleta ugumu wa udhibiti wa magonjwa ya kuambukizwa ya wanaadamu na
mifugo.
Changamoto
nyingine inayosababishwa na kutokuwepo kwa alama za mipaka inayoonekana
kwa wazi ni ugumu wa kudhibiti njia haramu za kupitisha bidhaa na hivyo
kukosesha serikali mapato na hata katika masuala ya ulinzi na usalama
wa nchi.
Mara
baada ya kumaliza uimarishaji wa mipaka ya nchi hizi mbili Tanzania na
Kenya wenye urefu wa kilometa 760 zikiwa za nchi kavu na kilomita 59.71
zikiwa ni mpaka wa majini. Kwa mwaka ujao wa fedha Serikali kupitia
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaimarisha mpaka wa
Tanzania na Uganda na baadae kuendelea na mipaka mingine
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akikagua alama za mpaka wa Tanzania na Kenya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni