Baadhi ya simba kati ya tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Na Hamza Temba-Dodoma
……………………………………………………
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameagiza Kikosi Kazi
Dhidi ya Ujangili cha Taifa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya wilaya ya Serengeti kuwasaka watu waliohusika na mauaji ya simba tisa
katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Dkt.
Kigwangalla ametoa agizo hilo ofisini kwake Jijini Dodoma jana baada ya
kupokea taarifa rasmi ya mauaji hayo ya kikatili yaliyoripotiwa hivi
karibuni kwa simba hao kulishwa sumu kali katika kijiji hicho huku mmoja
akikatwa miguu, mkia, ngozi ya juu ya mgongo na kuchukuliwa baadhi ya
viungo vyake ambapo amesema mauaji hayo hayavumiliki kwa kuwa yana
athari kubwa kiikolojia, kiutalii na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
“Bahati
mbaya sana ni kuwa anapouawa simba kwa sumu hafi peke yake, inakufa
familia nzima ya simba, na mara nyingi wanakufa pia wanyamapori wengine
wanaodowea nyama na wanaokula mizoga. Walipouawa simba wa Ruaha hivi
karibuni walikufa fisi zaidi ya 70 na ndege mbeshi zaidi ya 100, achilia
mbali wadudu,” amesema Dkt. Kigwangalla kwa masikitiko makubwa.
Amesema
pamoja na faida kubwa za simba kwa Taifa kiuchumi, Kijiji cha Nyichoka
pekee walikouwawa simba hao ni katika sehemu iliyofaidika sana na miradi
ya ujirani mwema kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Wanyama
hawa jamii ya paka wakubwa ni muhimu sana kwa kuweka mizania ya
ikolojia sawa, maana wanadhibiti idadi ya wanyama wala nyasi kwa kuwala,
bila hivyo hifadhi zote zinaweza kugeuka kuwa jangwa.
“Hakuna
mtalii atakayekuja hifadhini asitamani kumuangalia simba, mfalme wa
pori. Wanapouawa maana yake tunashusha hadhi ya hifadhi zetu kiutalii na
hivyo kutishia kupoteza mapato yanayotokana na utalii” amesisitiza Dkt.
Kigwangalla.
Amesema
tukio hilo la kuuwawa kwa Simba wa Ikolojia ya Serengeti sio la kwanza
kutokea hapa nchini ambapo mwishoni mwa mwaka jana simba wengine watano
waliuawa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
“Mwaka
huo huo mwanzoni simba watatu nao walipigwa risasi kikatili wilayani
Serengeti huku mwaka 2015 simba 7 wakauwawa tena kwa sumu, huko huko
Serengeti”.
Akizungumzia
sababu za ujangili huo amesema mara nyingi ni kwa ajili ya kulipiza
kisasi baada ya ng’ombe wa wananchi kuliwa na simba, changamoto ambayo
husababishwa na wananchi wenyewe kusogelea na kuweka makazi karibu
kabisa na mipaka ya hifadhi za wanyamapori kwa lengo la kulisha mifugo
pembezoni na wakati mwingine ndani ya hifadhi hizo kinyemela.
Simba
ambao wanakadiriwa kuwa zaidi kidogo ya 22,000, pamoja na wanyama
wengine jamii ya paka wamepungua sana miaka ya hivi karibuni kiasi cha
kuwekewa tishio la kutoweka hapa duniani. Duma nao wanakadiriwa kubaki
1,200 pekee.
Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika
kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara hivi karibuni kwa
ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.
Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.
Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.