Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Dk. Edmund Mndolwa akizungumza na
Viongozi wa Jumuiya hiyo, leo mjini Tarime mkoani Mara. Kushoto ni
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Erasto Sima, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoa
wa Mara Samweli Kiboya na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi
Tanzania uoande wa Zanzibar Haidar haji Abdallah na kulia ni Mwenyekiti
wa CCM mkoa wa Mara Mrida Mshota.
Na Bashir Nkoromo, Tarime.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Dk. Edmund Mndolwa ameshangazwa na baadhi
ya wanachama wa CCM na Jumuiya zake kushindwa kulipa ada ya uanachama
ya sh. 1200 kwa mwaka, ambayo ni sawa ya bei ya soda moja.
Dk.
Mndolwa ameelezea kushangazwa huko, wakati akizungumza na viongozi wa
CCM na Jumuiya za CCM kutoka Wilaya za mkoa wa Mara, katika ukumbi wa
CMG mjini Tarime, leo, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.
Kufuatia
hali hiyo Dk. Mndolwa ameagiza viongozi kusimamia ipasavyo ili
kuhakikisha kila mwanachama wa CCM na Jumuiya ya Wazazi Tanzania analipa
ada yake ya kila mwezi, akisisitiza kuwa watakaoshindwa kufanya hivyo
itakuwa ni mfano unaoonyesha kuwa hawafai uongozi kutokana na kushindwa
kusimamia uhai wa Jumuiya hiyo na Chama Cha Mapinduzi.
"Unamkuta
mtu kila mara anajinasibu kuwa ni mwanachama wa CCM au Jumuiya ya
Wazazi, lakini wakati huo huo halipi ada ya uanachama ya kila mwaka
mbayo gharama yake kwa kila mwaka ni sawa na bei ya soda moja ambayo
kila siku anamudu kuinunua", alisema Dk. Mndolwa.
Alisema,
ni jambo la muhimu kwa kila mwanachama kuhakikisha analipa ada yake ya
uanachama kwa sababu kufanya hivyo ndiyo ishara pekee inayodhihirisha
uanachama wake kwa kuwa asipofanya hivyo anakuwa mwanachama mfu
asiyeshiriki katika kuimarisha uhai wa Chama.
Dk.
Mndolwa amewasisitiza wanachama wa CCM kujiunga na Jumuiya za Chama
akisema kwamba kufanya hivyo kunatoa fursa pana zaidi kwa mwanachama
kuijenga CCM na pia hata kuwea kupata nafasi za uongozi kwa wepesi zaidi
kuliko akiwa mwana CCM tu.
"Tazameni,
hivi sasa mimi ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM lakini ni kwa sababu
nimekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Wazazi na kisha nikagombea kupitia
huko na kupata Uenyekiti wa Jumuiya hii ambapo sasa kwa nafasi niliyo
nayo ya Uenyekiti nimekuwa pia Mjumbe wa Kamati Kuu", alisema Dk.
Mndolwa.
Akizungumzia
maadili katika jamii, Dk. Mndolwa aliwatupia lawama wazazi kuwa ndiyo
chanzo kikubwa cha kumomonyoka kwa maadili katika jamii kutokana na
kuwaacha watoto wao kufanya wapendavyo katika masuala ya tabia.
"Unakuta
binti anatoka nyumbani amefaa nguo za kubaka maungo na zinazoacha wazi
baadhi ya maungo yanayostahili kusitiriwa, mzazi anaona lakini anamuacha
bila kumkemea, matokeo yake binti anakuwa mitaani katika namna ya
kutokuwa na maadili bora, ikitokea hivyo jua lawama ni kwa mzazi",
alisema Dk. Mndolwa.
Alisema,
hali kadhalika ni kosa la mzazi pale mtoto wa kiume anapotoka nyumbani
huku amevaa katula au suruali inayoporomoka matakoni, kwa sababu mzazi
anapaswa kukemea uvaaji huo kwa kuwa unatia aibu katika jamii.
"Unakuta
mzazi anampa hela nyingi mtoto wakati anakwenda shuleni huku akisema
kuwa kwa kuwa yeye alisoma katika mazingira ya taabu hataki mwanae asome
kwa taabu, kumbe hajui kuwa kwa kufanya hivyo anamjengea mtoto
vishawishi vya kutumbukia katika utumiaji wa dawa za kulevya na uvutaji
bangi", alisema Dk. Mndolwa.
Dk.
Mndolwa aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele kuwahakikisha wanasaidia
kujenga maadili ya jamii kwa kuwakanya na kuwachukulia hatua thabiti
watoto wao kila wanapowagundua au kuwaona wanajaribu kuanza kuiga tabia
zinazomomonyoa maadili.
Akizungumzia
mshikamano ndani ya Chama, Dk. Mndolwa aliwataka wana CCM kuachana
kabisa na mtindo wa kung'ang'ania makundi kila baada ya uchaguzi na pia
kuachana na tabia ya kuthani mtu fulani ni maarufu kuliko chama.
Dk.
Mndolwa alisema, ikiwa wanachama wataachana na mambo hayo CCM inakuwa
imejihakikishia kupata ushindi kila uchaguzi kwa kuwa inao wanachama na
wapenzi wengi na kinachohitajika ni mshikamano tu.
"Hadi
sasa kuna baadhi ya majimbo au Kata walizoshinda wapinzani katika
uchaguzi uliopita, lakini kwa maoni yangu wapinzani hawakushinda maeneo
hayo eti kwa sababu ni weledi sana, hapana. ukweli ni kwamba walishinda
kwa sababu ya uzembe wa wana CCM wenyewe kung'ang'ania makundi baada ya
kura za maoni", alisema Dk. Mndolwa.
Lengo
la ziara hiyo ya Dk. Mndolwa katika mikoa ya Kanda ya ziwa na mkoa wa
Singida, ni kuwashukuru wananchama wa Jumuiya ya Wazazi kwa kumchagua
kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na pia kuwatambulisha Makamu Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania kwa upande wa Zanzibar Haidar Haji
Abdallah na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Erasto Sima ambao ameambatana
nao katika ziara hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni