Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wasafirishaji wa Mabasi Tanzania(TABOA) Enea Mrutu amewaomba wamiliki wote wa mabasi nchini kuendelea kutoa huduma za kusafirisha abiria kwa umakini wa hali ya juu kwa kuhakikisha hawasababishi ajali wakati wakiendelea kusubiri kukuona na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili watoe kilio chao.
TABOA iliomba kuonana na Waziri Mkuu kwa ajili ya kutoa malalamiko yao kutokana kwa madai kuna sheria na kanuni za usalama barabarani ambazo ni kandamizi kwao na zimekuwa zikiwaweka katika wakati mgumu katika kutoa huduma ya kusafirisha abiria nchii.
Hata hivyo TABOA bado hawajafanikiwa kuonana naye ingawa tayari ameshawapa maelekezo kuwa wakati wowote atakutana nao na kisha kuwasikiliza ili kupata muafaka kwa kushirikiana na wadau wengine wa usafiri wakiwamo Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra).
Akizungumza na Michuzi Blog leo jijini Dar es Salaam Mrutu amesema wanatambua majukumu aliyonayo Waziri Mkuu hivyo wana imani akipata muda watakutana naye na kisha kuzungumza kwa kina kuhusu changamoto ambazo wanakabiliana nazo watoa huduma ya usafiri nchini.
"Ombi letu kwa wanachama wa Taboa waendelee kutoa huduma bora ikiwa pamoja na kuwa makini barabarani ili kuepuka ajali.Tunamatumaini makubwa na Waziri Mkuu, hivyo tunajua akipata muda atatuita ,nasi tupo tunasubiri.Hivyo wakati tunaendelea kumsubiri tuendelee kutoa huduma ya usafiri bila kuchoka,"amesema Mrutu.
Taarifa za awali ambazo Michuzi Blog ilizipata ni kwamba Taboa walitaliwa kukutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki iliyopita lakini hawakufanikiwa kukutana naye kutokana na majukumu aliyonayo, hivyo aliwahakikisha atapanga ratiba ya kukutana nao.
Hata hivyo kwa muda mrefu sasa Taboa na Sumatra wamekuwa katika mvutano wa hapa na pale uliosababisha Chama hicho kutishia kutotoa huduma kwa madai ya kutoridhishwa na faini kuanzia Sh 200,000 hadi Sh 500,000 zinazotozwa kwa mabasi hayo pindi yawapo safarini.
Taboa kupitia kwa Mrutu amesema wanasikitishwa na faini hizo ambazo kibaya zaidi hata wakati wa mchakato wa kuziandaa Sumatra hawakuwashirikisha wadau wa usafirishaji wakiwamo wao na hivyo kuibua malalamiko.
"Mbali ya kutoshirikishwa wakati wa mchakato wa uandaaji wa faini hizo, pia utaratibu wa faini hizo unakiukwa kwa kuwahusisha wamiliki hata katika makossa yanayowahusu madereva.Pamoja na malalamiko yetu tunaendelea kuwahamisha wanachama wetu waendelee kutoa huduma iliyobora kwa manufaa ya nchi yetu,"amesema.
Wakati huo huo TABOA imesema imesikitishwa na ajali ya basi iliyotokea mkoani Kigoma na kusababisha abiria 10 kupoteza maisha na madereva kuwa makini ili kuepuka ajali za barabarani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni