Mkuu wa Mawasiliano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana
akizungumza na waandishi wa habari Masaki jijini Dar es salaam leo
wakati wa kutiliana saini mkataba wa udhamini na Mwanariadha kinda
Francis Damiano Damasi hayupo pichani kushoto ni Wilhelm Gidabuday
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
Mkuu wa Mawasiliano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana
akimkabidhi mkataba Mwanariadha kinda Francis Damiano Damasi baada ya
kutiliana saini mkataba wa udhamini leo Masaki jijini Dar es salaam
kushoto ni wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kulia ni Meta Petro
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na
kocha.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na kocha akifafanua jambo katika mkutano huo.
Wafanyakazi wa Multichoice
Tanzania kutoka kulia ni Shumbana Walwa Afisa Masoko, Talha na Grace
Mgaya wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla hiyo.
………………………………………………………………
MultiChoice Tanzania imetangaza
kuendelea kudhamini mchezo wa riadha hapa nchini huku ikisaini
makubaliano maalum ya kumdhamini mwanariadha kinda Francis Damiano
Damasi. Udhamini huo unahusisha fedha ya kujikimu kwa mawanariadha huyo
na mafunzo yake na wanariadha wengine katika kambi maalum ya mafunzo
inayotarajiwa kuwa wilayani Mbulu.
Akizungumza wakati wa hafla ya
kusaini mkataba wa udhamini kwa mwanariadha huyo, Mkuu wa Mawasiliano wa
MultiChoice Tanzania Johnson Mshana, amesema kuwa dhamira kubwa ya
MultiChoice ni kuhakikisha kuwa mchezo wa riadha unakuwa na mchango
mkubwa katika kuliletea taifa sifa, kutoa ajira kwa vijana wengi na
kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.
“Tunataka taifa hili lijulikane
ulimwengu mzima kama chimbuko la mabingwa, na tumeanza na riadha.
Tumedhamiria kukuza mchezo huu na kuufanya kama chanzo kikubwa cha ajira
kwa vijana wetu, lakini pia riadha ni mchezo, ni burudani, na ni sekta
nyeti kiuchumi kama ikiendelezwa” alisema Mshana na kuongeza “Tunataka
kuusikia wimbo wetu wa taifa katika mashindano makubwa ya kimataifa,
tunataka kuiona bendera yetu ikipepea juu katika kila mashindano makubwa
ya riadha ya kimataifa, tunataka mamia ya vijana wetu wenye uwezo
mkubwa katika riadha washiriki kwenye mashindano makubwa, waweze
kujipatia kipato, kuwekeza na kuwa chanzo cha maelfu ya ajira na
hatimaye kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu”
Amefafanua kuwa udhamini huo
utakuwa wa mwaka mmoja na utaendelezwa na kuboreshwa kulingana na hali
itakavyokuwa pamoja na mafanikio yatakayopatiokana. “ Huu ni mkakati
wetu endelevu, ni mpango wetu maalum unaojulikana kama ‘Ni Zamu Yetu’!
ambao umejikita katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu
katika riadha.” Amesema Mshana.
Mbali na kumdhamini Damiano,
MultiChoice pia itadhamini kambi maalum ya mafunzo itakayokuwa wilayani
Mbulu ambayo inatarajiwa kuanza mafunzo rasmi hivi karibuni. Amebainisha
kuwa taratibu za kuanza kwa kambi hiyo zipo katika hatua nzuri na kambi
inatarajiwa kuanza rasmi Agosti mwaka huu na itakuwa na wanariadha
kinda wasiopungua sita – wasichana na wavulana.
Kwa upande wake mwanariadha
Damiano ambaye ni mshindi wa medali ya shaba katika mashindano ya vijana
ya Jumuia ya Madola yaliyofanyika visiwa vya Bahamas, amesema udhamini
huo utamfanya aweze kufanya mazoezi yake vizuri kwani sasa hyo ndiyo
itakuwa kazi yake ya kudumu. Amesema kilicho mbele yake ni ushindi tu.
“Nashukuru sana kwa udhamini wa MultiChoice, na mimi naahidi kuwa
nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa siwaangushi MultiChoice na
siwaangushi watanzania.”
Katibu mkuu wa Shirikisho la
Riadha Tanzania Wilhelm Gida-Buday, amesema wamefarijika sana kuona kuwa
MUltiChoice inaendelea kudhamini riadha na akasema udhamini huo siyo tu
utamsaidia mwanariadha husika, bali pia ni chachu hata kwa wanariadha
chipukizi kuwa na moyo na ari ya kushiriki katika mchezo huo.
Amesema Shirikisho la Riadha
Tanzania litahakikisha kuwa udhamini huo unakuwa wa manufaa na unazaa
matunda yaliyotarajiwa ya kuleta medali zaidi kutaka katika mashindano
ya kimataifa. “Ufadhili wa aina hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya
mchezo wa riadha. Tunaahidi ushirikiano wetu wa hali na mali ili
kufanikisha malengo na tutahakikisha kuwa tunatoa ushirikiano
unaostahili kwa wadhamini wetu” alisema Gida.
Mwanariadha Francis Damiano
Damasi, anatarajiwa kushiriki mashindano makubwa ikiwemo Mashindano ya
vijana ya Afrika Mashariki yanayofanyika mwishoni mwa wiki hii jijini
Dar es Salaam, Mashindano ya vijana ya Dunia (World Junior Championship)
mwezi Julai nchini Finland, Mashindao ya vijana ya Olympic kanda ya
Afrika mwezi Julai nchini Algeria, Mashindano ya vijan ya Olympic (Youth
Olympic Games) mwezi Oktoba nchini Argentina, na mashindano ya nyika ya
vijana (World Junior Cross-country) mapema mwakani nchini Denmark.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni